The chat will start when you send the first message.
1Tamko zito la Bwana, alilowaambia Waisiraeli kinywani mwa Malaki.[#1 Mose 25:23; Rom. 9:13.]
2Ndivyo, Bwana anavyosema: Nimewapenda ninyi, nanyi husema: Umetupenda namna gani? Ndivyo, asemavyo Bwana: Je? Esau siye kaka yake Yakobo? Nami nilimpenda Yakobo.
3Lakini Esau nilimchukia, milima yake nikaigeuza kuwa mapori matupu, nalo fungu lake nikawapa mbwa wa nyikani.[#Yes. 34:13.]
4Sasa Edomu akisema: Tumepondwa, lakini tutayajenga tena mabomoko, Bwana Mwenye vikosi atawajibu: Ijapo wao wajenge, mimi nitajengua, nao watu watawaita: Nchi yao wasiomcha Mungu, tena: Ukoo wao, Bwana anaowakasirikia kale na kale.
5Macho yenu yatayaona, nanyi mtasema: Bwana hutukuka kuipita mipaka ya Isiraeli.
6Mwana humheshimu baba yake, hata mtumwa humheshimu bwana wake; kama mimi na Baba yenu, heshima yangu iko wapi? Ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyowauliza ninyi watambikaji mnaolibeza Jina langu, kisha mnasema: Jina lako tumelibeza kwa nini?[#2 Mose 20:12; Yoh. 8:49.]
7Ninyi huleta mezani pangu pa kutambikia vilaji vya tambiko vichafu na kusema: Tumekutia uchafu kwa nini? Ni kwa kusema kwenu: Meza ya Bwana hubezeka.
8Tena mkileta nyma kipofu kuwa ng'ombe ya tambiko, si vibaya? Au mkileta achechemeaye au aliyeugua, si vibaya? Haya! Umpelekee mtawala nchi vyako vilivyo hivyo, uone, kama atapendezwa na wewe, akupendelee! ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema.[#3 Mose 22:20,23.]
9Sasa ulalamikieni uso wa Mungu, atuhurumie! Ikiwa vipaji kama hivyo vimetolewa na mikono yenu, je? Atawapendelea? Ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema:
10Vingekuwa vyema, kama mtu wa kwenu angeifunga milango, msije kuwasha moto bure mezani pangu pa kutambikia! Sipendezwi kabisa nanyi, wala sipendezwi na vipaji vya tambiko vitokavyo mikononi mwenu; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema.[#Mal. 2:13; Yes. 1:13.]
11Kwani kutoka maawioni kwa jua mpaka machweoni kwake Jina langu ni kuu kwa wamizimu, tena kila mahali Jina langu linatolewa mavukizo na vipaji vya tambiko vitakatavyo, kwani Jina langu ni kuu kwa wamizimu; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema.[#Yes. 60:1-7.]
12Lakini ninyi hulipatia uchafu kwa kusema kwenu: Meza ya Bwana hubezeka, nayo inayotupatia ni chakula kinachobeuliwa.
13Tena anasema Bwana Mwenye vikosi: Mwasema: Tazameni, tunavyosumbuka! kisha mwazinung'unikia kazi zenu na kuleta nyama aliyenyang'anywa au achechemeaye au auguaye, mmtoe kuwa ng'ombe ya tambiko; basi, nipendezwe na vipaji hivyo vitokavyo mikononi mwenu? ndivyo, Bwana anavyosema.
14Na awe ameapizwa huyu mdanganyifu anayekuwa na nyama wa kiume katika kundi lake! Lakini akiapa kutoa mmoja, anapeleka aliye mbaya kumchinjia Bwana kuwa ng'ombe ya tambiko. Kwani mimi ni mfalme mkuu, nalo Jina langu huogopwa kwa wamizimu; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema.[#3 Mose 22:19.]