The chat will start when you send the first message.
1Siku zile mfalme Herode alipousikia uvumi wa Yesu,
2akawaambia watoto wake: Huyo ndiye Yohana Mbatizaji, amefufuka katika wafu, kwa sababu hii nguvu hizo humtendesha kazi.
3Kwani Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia kifungoni kwa ajili ya Herodia, mke wa nduguye, Filipo.[#Mat. 11:2.]
4Kwani Yohana alimwambia: Ni mwiko kwako kuwa naye.[#3 Mose 18:16.]
5Naye alitaka kumwua, lakini aliwaogopa watu, kwani walimwona Yohana kuwa mfumbuaji.[#Mat. 21:26.]
6Ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia akacheza ngoma mbele yao, akampendeza Herode.
7Ndipo, alipomwapia kumpa cho chote, atakachomwomba.
8Naye kwa hivyo, alivyokwisha kuhimizwa na mama yake, akasema: Nipe sasa hivi katika chano kichwa chake Yohana Mbatizaji!
9Mfalme akasikitika, lakini kwa ajili ya viapo vyake na kwa ajili ya wale waliokaa naye chakulani akaagiza, apewe.
10Akatuma mtu, akamkata Yohana kichwa kifungoni.
11Kisha hicho kichwa chake kikaletwa katika chano, msichana akapewa, akampelekea mama yake.
12Kisha wanafunzi wake wakaja, wakautwaa mwili wake, wakauzika; kisha wakaenda, wakampasha Yesu habari.
13Yesu alipoyasikia akaingia chomboni, akaondoka huko kwenda peke yake mahali palipokuwa pasipo watu.
14Nayo makundi ya watu walipovisikia wakamfuata kwa miguu toka mijini. Yesu alipotoka chomboni akaona, watu ni wengi sana, akawaonea uchungu, akawaponya waliokuwa hawawezi.[#Mat. 9:36.]
15Ilipokuwa jioni, wanafunzi wake wakamjia, wakasema: Hapa tulipo ni nyika, nazo saa za mchana zimepita; basi, waage hawa watu wengi, waende zao vijijini, wajinunulie vyakula!
16Yesu akawaambia: Waendeje? Wapeni ninyi vyakula!
17Nao wakamwambia: Hatuna kitu hapa ila mikate mitano na visamaki viwili.
18Naye akasema: Nileteeni hapa!
19Akawaagiza hao watu wengi, wakae chini majanini. Akaitwaa ile mikate mitano na vile visamaki viwili, akatazama juu mbinguni akaviombea, akawamegea, akawapa wanafunzi ile mikate; nao wanafunzi wakawapa wale watu wengi.
20Wakala wote, wakashiba. Kisha wakayaokota makombo ya mikate yaliyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili.[#2 Fal. 4:44.]
21Nao waliokula walikuwa waume tu kama 5000 pasipo wanawake na watoto.
22Kisha Yesu akawashurutisha wanafunzi waingie chomboni, wamtangulie kwenda ng'ambo, mpaka yeye kwanza awaage makundi ya watu.
23Naye alipokwisha kuwaaga makundi ya watu akapanda mlimani peke yake kuomba. Jua lilipokwisha kuchwa, akawa huko peke yake.[#Luk. 6:12; 9:18.]
24Nacho chombo kilikuwa kimeendelea kitambo kirefu kikahangaishwa na mawimbi, kwani upepo uliwatokea mbele.
25Ilipofika zamu ya nne ya usiku, akawajia akienda juu ya bahari.
26Wanafunzi walipomwona, anavyokwenda juu ya bahari, wakatetemeka wakisema: ni mzimu! wakalia kwa woga.[#Luk. 24:37.]
27Papo hapo Yesu akawaambia akisema: Tulieni! Ni miye, msiogope!
28Petero akamjibu akisema: Bwana, ukiwa ni wewe, agiza nije kwako majini juujuu!
29Alipomwambia: Njoo! Petero akashuka chomboni, akaenda juu ya maji, amfikie Yesu.
30Lakini alipotazama, upepo ulivyo na nguvu, akaogopa, akaanza kuzama majini, akapiga kelele akisema: Bwana, niokoa!
31Mara Yesu akaunyosha mkono, akamshika, akamwambia: Mbona unanitegemea kidogo tu? Mbona umeingiwa na wasiwasi?[#Mat. 8:26.]
32Walipopanda chomboni, upepo ukakoma.
33Nao waliokuwamo chomboni wakamwangukia wakisema: Kweli ndiwe Mwana wa Mungu!
34Walipokwisha vuka wakafika nchini kwa Genesareti.
35Wenyeji wa huko walipomtambua wakatuma watu kwenda katika nchi zote za pembenipembeni, wakamletea wote waliokuwa hawawezi.
36Wakambembeleza, wamguse pindo la kanzu yake tu; nao wote walioligusa wakapona kabisa.[#Mat. 9:21; Luk. 6:19.]