Mateo 4

Mateo 4

Kujaribiwa.

(1-11: Mar. 1:12-13; Luk. 4:1-13)

1Kisha Yesu akapelekwa na Roho nyikani, ajaribiwe na Msengenyaji.[#Ebr. 4:15.]

2Akafunga siku 40 mchana na usiku, kisha akaona njaa.[#2 Mose 34:28; 1 Fal. 19:8.]

3Mjaribu akamjia, akamwambia: Kama ndiwe Mwana wa Mungu, yaambie mawe haya, yawe chakula![#1 Mose 3:1-7.]

4Naye akamjibu: Imeandikwa:

Mtu hataishi kwa chakula tu,

ila kwa kila neno linalotoka kinywani mwa Mungu.

5Kisha Msengenyaji akampeleka katika mji mtakatifu, akamsimamisha juu pembeni hapo Patakatifu,[#Mat. 27:53.]

6akamwambia: Kama ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini! Kwani imeandikwa:

Atakuagizia malaika zake, nao wakakuchukua mikononi mwao

usije kujikwaa mguu wako katika jiwe.

7Yesu akamwambia: Tena imeandikwa:

Usimjaribu Bwana Mungu wako!

8Kisha Msengenyaji akampeleka, akampandisha mlima mrefu sana, akamwonyesha ufalme wote pia wa ulimwengu huu na utukufu wake,[#Yoh. 18:36.]

9akamwambia: Haya yote nitakupa, ukiniangukia na kuninyenyekea.[#Mat. 16:26.]

10Hapo Yesu akamwambia: Nenda zako, Satani! Kwani imeandikwa:

Umwangukie Bwana Mungu wako na kumtumikia peke yake!

11Ndipo, Msengenyaji alipomwacha. Mara malaika wakaja, wakamtumikia.*[#Yoh. 1:51; Ebr. 1:6,14.]

Yesu anakaa Kapernaumu.

(12-17: Mar. 1, 14.15 Luk. 4, 14.15)

12Yesu aliposikia, ya kwamba Yohana amefungwa, akaondoka akaenda mpaka Galilea.[#Mat. 14:3.]

13Akahama Nasareti, akaenda kukaa Kapernaumu ulioko pwani mipakani kwa Zebuluni na Nafutali,

14kusudi neno, mfumbuaji Yesaya alilolisema, lipate kutimizwa:[#Yes. 9:1-2.]

15Nchi ya Zebuluni na nchi ya Nafutali zilizoko upande

wa pwani na ng'ambo ya Yordani, Galilea ya wamizimu

iliko,

16huko watu waliokaa gizani wameona mwanga mkuu,

waliokaa penye kivuli kuacho mwanga umemulika juu yao.

17Tangu hapo ndipo, Yesu alipoanzia kupiga mbiu akisema: Juteni! Kwani ufalme wa mbingu umekaribia.[#Mat. 3:2; Rom. 12:2.]

Wanafunzi wa kwanza.

(18-22: Mar. 1:16-20; Luk. 5:1-11.)

18Basi, Yesu alipokuwa akitembea kandokando ya bahari ya Galilea akaona watu wawili waliokuwa ndugu, ni Simoni aitwaye Petero na nduguye, Anderea. Aliwaona, wakitupa nyavu zao baharini, kwani walikuwa wavuvi.[#Yoh. 1:40.]

19Akawaambia: Njoni, mnifuate! Nami nitawafanya kuwa wavua watu.[#Mat. 13:47; 28:19-20; Ez. 47:10.]

20Papo hapo wakaziacha nyavu, wakamfuata.[#Mat. 19:27.]

21Alipoendelea mbele, akaona wengine wawili walikuwa ndugu, ni Yakobo wa Zebedeo na nduguye, Yohana. Aliwaona pamoja na baba yao Zebedeo chomboni, wakizitengeneza nyavu zao, akawaita.

22Papo hapo wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata.

Yesu katika Galilea

23Yesu akazunguka katika nchi yote ya Galilea, akawafundisha katika nyumba zao za kuombea, akautangaza Utume mwema wa ufalme na kuwaponya watu wote waliokuwa wagonjwa na wanyonge.[#Mar. 1:39; Luk. 4:15,44; Tume. 10:38.]

24Uvumi wake ukaienea nchi yote ya Ushami. Wakampelekea wote walikuwa hawawezi, walioshikwa na magonjwa na maumivu yo yote, nao wote waliokuwa wenye pepo na wenye kifafa na wenye kupooza, naye akawaponya.[#Mar. 6:55.]

25Wakamfuata makundi mengi ya watu waliotoka Galilea na upande wa ile Miji Kumi na Yerusalemu na Yudea na ng'ambo ya Yordani.[#Mar. 3:7-8; Luk. 6:17-19.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania