The chat will start when you send the first message.
1Yasikieni, Bwana anayoyasema:
Haya! Bisheni mbele ya milima, vilima vizisikie sauti zenu!
2Ninyi milima, yasikieni masuto ya Bwana!
Yasikieni nanyi miamba mlio misingi ya nchi!
Kwani Bwana ana shauri nao walio ukoo wake,
hana budi kuumbuana na Waisiraeli!
3Ninyi mlio ukoo wangu, nimewafanyizia nini?
Nimewachokoza kwa nini? Nijibuni!
4Kwani niliwatoa katika nchi ya Misri, nikawaleta huku,
nikawakomboa katika nyumba, mlimokuwa watumwa,
nikamtuma Mose na Haroni na Miryamu, wawatangulie.
5Mlio ukoo wangu, yakumbukeni,
Balaka, mfalme wa Moabu, aliyowawazia,
nayo Bileamu, mwana wa Beori, aliyomjibu!
Yakumbukeni nayo yaliyofanyika toka Sitimu mpaka Gilgali,
mpate kujua, ya kuwa Bwana ni mwongofu.
6Nimtokee Bwana na kumpa nini
nikimnyenyekea Mungu Alioko huko juu?
nimtolee ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima,
kama ndama za mwaka mmoja
7Je? Bwana atapendezwa na maelfu ya madume ya kondoo?
Au atapendezwa na maelfu kumi ya vijito vya mafuta?
Au nimpe mwanangu wa kwanza,
awe ng'ombe ya tambiko ya kuondolea mapotovu yangu?
Je? Zao la tumbo langu liyalipe makosa ya roho yangu?
8Umeambiwa, wewe mtu, yaliyo mema,
nayo Bwana anayoyatafuta kwako:
Yafanye yapasayo
ukipenda kuwahurumia wenzako,
tena ukiendelea kushikamana na Mungu wako
na kujinyenyekeza.
9Sauti ya Bwana inawaita waliomo mjini,
- nako kulitazamia Jina lako ni ujuzi -
inasema: Isikieni fimbo iwapigayo!
Msikieni naye aliyeiagiza!
10Je? Nyumbani mwao wasiomcha Mungu
yangalimo bado malimbiko yaliyopatwa kwa uovu?
nazo zile pishi nyembamba zilizoapizwa?
11Niwawazie kuwa wametakata,
ijapo watumie mizani za kuchukulia mali za watu bure?
au ijapo watie mishipini vijiwe vya kupimia vidanganyavyo watu?
12Matajiri ya kwao huzidi ukorofi, nao wenyeji wao husema uwongo,
nazo ndimi zao vinywani mwao hudanganya watu.
13Kwa hiyo nami nitakupiga, usipone;
nitakuangamiza kwa ajili ya makosa yako.
14Wewe utakula, lakini hutashiba, njaa ikae tumboni mwako.
Utakayoyapeleka pengine hutayaponya;
nayo utakayoyaponya, nitayatolea panga.
15Wewe utapanda, lakini hutavuna;
wewe utakamua chekele, lakini hutajipaka mafuta;
utakamua zabibu, lakini hutakunywa mvinyo.
16Kwani mmeyashika maongozi ya Omuri,
mkayafanya matendo yote ya mlango wa Ahabu,
mkayafuata mashauri yao,
niigeuze nchi yenu, iwe mapori matupu,
nao watakaokaa huku wazomelewe.
Hivyo ndivyo, mtakavyotwikwa matusi yao walio ukoo wangu.