The chat will start when you send the first message.
1Utume mwema wa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, ulianza,[#Mal. 3:1; Mat. 11:10.]
2kama ulivyoandikwa na mfumbuaji Yesaya:
Utaniona mimi, nikimtuma mjumbe wangu,
akutangulie, aitengeneze njia yako.
3Iko sauti ya mtu apigaye mbiu nyikani:
Itengenezeni njia ya Bwana! Yanyosheni mapito yake!
4Yohana Mbatizaji alikuwa nyikani akibatiza na kutangaza ubatizo wa kujutisha, wapate kuondolewa makosa.
5Wakamtokea wote wa Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu, wakabatizwa naye katika mto wa Yordani wakiyaungama makosa yao.
6Naye Yohana alikuwa amevaa nguo ya manyoya ya ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni pake, akala nzige na asali ya mwituni.
7Akatangaza akisema: Nyuma yangu anakuja aliye na nguvu kunipita mimi, nami sifai kuinama, nimfungulie kanda za viatu vyake.
8Mimi nimewabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho takatifu.
9Ikawa siku zile, Yesu akaja toka Nasareti wa Galilea, akabatizwa na Yohana mle Yordani.[#Luk. 2:51.]
10Papo hapo alipotoka majini akaona, mbingu zikipasuka, akamwona Roho, anavyomshukia kama njiwa.
11Sauti ikatoka mbinguni: Wewe ndiwe mwanangu mpendwa, nimependezwa na wewe.[#Mar. 9:7.]
12Papo hapo Roho akamchukua, akampeleka nyikani.[#Sh. 91:13; Yoh. 1:51.]
13Akawa huko nyikani siku 40 akijaribiwa na Satani, tena wenzake walikuwa nyama wa porini. Kisha malaika wakamtumikia.
14Yohana alipokwisha fungwa, Yesu akaja Galilea, akautangaza Utume mwema wa Mungu,
15akasema: Siku zimetimia, nao ufalme wa Mungu umekaribia. Juteni, mwutegemee Utume mwema![#Gal. 4:4.]
16Naye alipokuwa akitembea kandokando ya bahari ya Galilea, akamwona Simoni na Anderea, nduguye Simoni, wakitupa nyavu zao baharini, kwani walikuwa wavuvi.
17Yesu akawaambia: Njoni, mnifuate! Nami nitawafanya kuwa wavua watu.[#Mat. 13:47.]
18Papo hapo wakaziacha nyavu, wakamfuata.
19Alipoendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo, mwana wa Zebedeo, na Yohana nduguye; nao walikuwa chomboni wakizitengeneza nyavu.
20Mara akawaita, nao wakamwacha baba yao Zebedeo mle chomboni pamoja na wafanya kazi, wakaja, wakamfuata nyuma yake.
21Wakaenda, wakaingia Kapernaumu. Ilipokuwa siku ya mapumziko, akaiingia nyumba ya kuombea, akafundisha.
22Wakashangazwa na mafundisho yake; kwani alikuwa akiwafundisha kama mwenye nguvu, si kama waandishi.[#Mat. 7:28-29.]
23Humo nyumbani mwao mwa kuombea mkawa na mtu aliyekuwa na pepo mchafu; akapaza sauti
24akisema: Tuko na jambo gani sisi na wewe, Yesu wa Nasareti? Umekuja kutuangamiza. Nakujua, kama u nani; ndiwe Mtakatifu wa Mungu.[#Mar. 5:7; Sh. 16:10; Mat. 8:29.]
25Yesu alipomkaripia akisema: Nyamaza, umtoke!
26ndipo, yule pepo mchafu alipomsukumasukuma, akalia kwa sauti kuu, kisha akamtoka.[#Mar. 9:26.]
27Wote wakaingiwa na kituko, hata wakaulizana wao kwa wao wakisema: Hilo ni jambo gani? Ni ufundisho mpya wa kinguvu. Anawaagiza hata pepo wachafu, nao humtii.
28Huo uvumi wake ukatoka, ukaenea upesi po pote katika nchi zote zilizozunguka Galilea.
29Hapo walipotoka nyumbani mwa kuombea wakaingia pamoja na Yakobo na Yohana nyumbani mwao Simoni na Anderea.
30Naye mama ya mkewe Simoni alikuwa amelala kwa kuwa na homa. Papo hapo, walipomwambia, alivyokuwa,
31akamjia, akamwinua na kumshika mkono; ndipo, homa ilipomwacha, akawatumikia.
32Ilipokuwa jioni, jua lilipokwisha kuchwa, wakampelekea wote waliokuwa hawawezi, nao waliopagawa na pepo,
33mji wote ukawa umekusanyika mlangoni.
34Akawaponya wengi waliokuwa hawawezi, wenye magonjwa mengi, akafukuza pepo wengi akiwakataza pepo kusema, ya kuwa walimjua.[#Luk. 4:41; Tume. 16:17-18.]
(35-36: Luk. 4:42-44.)35Asubuhi na mapema sana akainuka, akatoka, akaenda zake mahali palipokuwa pasipo watu; hapo ndipo, alipomwomba Mungu.
36Naye Simoni na wenziwe wakamfuata mbio;
37walipomwona wakamwambia: Wote wanakutafuta.
38Akawaambia: Twendeni pengine penye vijiji vya pembenipembeni, nipate kupiga mbiu humo namo! Kwani hiyo ndiyo, niliyojia.
39Akaenda katika nchi yote ya Galilea, akapiga mbiu katika nyumba zao za kuombea, akafukuza pepo.
40Mwenye ukoma akaja kwake, akambembeleza na kumpigia magoti akimwambia: Ukitaka waweza kunitakasa.
41Ndipo, alipomwonea uchungu, akanyosha mkono, akamgusa, akamwambia: Nataka, utakaswe.
42Mara ukoma ukamwondoka, akatakaswa.[#Mar. 3:12; 7:36.]
43Papo hapo akamkimbiza na kumkemea[#3 Mose 14:2-32.]
44akimwambia: Tazama, usimwambie mtu neno! Ila uende zako, ujionyeshe kwa mtambikaji, uvitoe vipaji kwa ajili ya kutakaswa kwako, Mose alivyoviagiza, vije vinishuhudie kwao!
45Lakini alipotoka akaanza kutangaza mengi na kulisimulia jambo hilo po pote. Kwa hiyo Yesu hakuweza tena kuingia mjini waziwazi, ila alikuwa akikaa nje mahali palipokuwa pasipo watu, lakini watu wakamwendea toka pande zote.