Marko 14

Njama ya kumkamata Yesu.

(1-2: Mat. 26:1-5; Luk. 22:1-2.)

1Palikuwa pamesalia siku mbili kuwa sikukuu ya Pasaka na ya mikate isiyotiwa chachu. Nao watambikaji wakuu na waandishi wakatafuta kumkamata kwa werevu, wapate kumwua;

2lakini walisema: Kwanza sikukuu ipite, watu wasije, wakafanya fujo!

Yesu anamiminiwa mafuta.

(3-9: Mat. 26:6-13; Yoh. 12:1-8.)

3Naye alipokuwa Betania nyumbani mwa Simoni Mkoma akikaa chakulani, akamjia mwanamke mwenye kichupa chepe cha jiwe kilichojaa mafuta ya maua yanayoitwa Narada; ni yenye bei kubwa, nayo yalikuwa hayakuchanganywa na mengine. Akakivunja kile kichupa, akayamiminia kichwani pake.[#Luk. 7:36-38.]

4Mlikuwamo waliochukiwa mioyoni mwao kwamba: Upotevu huu wa haya mafuta mazuri sana ni wa nini?

5Kwani mafuta haya yangaliwezekana kuuzwa kwa shilingi 300 na kupita, wakapewa maskini! Kwa hiyo wakamfokea sana.

6Lakini Yesu akasema: Mwacheni! Mbona mnamsikitisha? Amenitendea tendo zuri.

7Kwani maskini mnao kwenu siku zote, kila mnapotaka mweze kuwafanyia vema; lakini mimi hamwi nami siku zote.[#5 Mose 15:11.]

8Amefanya, alivyoweza; ameanza kuupaka mwili wangu mafuta haya, autengenezee kuzikwa.

9Kweli nawaambiani: Po pote katika ulimwengu wote, patakapotangazwa huu Utume mwema, patasemwa nacho hiki, alichokitenda yeye, naye akumbukwe.

Yuda Iskariota.

(10-11: Mat. 26:14-16; Luk. 22:3-6.)

10Kisha Yuda Iskariota aliyekuwa mwenzao wale kumi na wawili akaenda zake kwa watambikaji wakuu, amtie mikononi mwao.

11Nao walipoyasikia wakafurahi, wakaagana naye kumpa fedha. Ndipo, alipotafuta njia iliyofaa, amtoe.

Kondoo ya Pasaka.

(12-16: Mat. 26:17-19; Luk. 22:7-13.)

12Siku ya kwanza ya kula mikate isiyotiwa chachu, watu walipochinjia kondoo ya Pasaka, wanafunzi wake wakamwuliza: Unataka, twende, tukuandalie wapi, uile kondoo ya Pasaka?

13Akawatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia: Nendeni mjini! Humo mtakutana na mtu anayechukua mtungi wa maji, mfuateni!

14Mle atakamoingia mwambieni mwenye nyumba: Mfunzi anauliza: Kiko wapi chumba cha kukaa mimi, ndimo niile kondoo ya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?[#Mar. 11:3.]

15Ndipo, mwenyewe atakapowaonyesha chumba kikubwa kilichokwisha kutandikwa; namo mle tuandalieni!

16Wale wanafunzi wakatoka, wakaenda, wakaingia mjini, wakaona, kama alivyowaambia, wakaiandaa kondoo ya Pasaka.

(17-25: Mat. 26:20-29; Luk. 22:14-23; Yoh. 13:21-26.)

17Ilipokuwa jioni, akaja pamoja na wale kumi na wawili.[#Sh. 41:10.]

18Walipokaa wakila, Yesu akasema: Kweli nawaambiani: Mwenzenu mmoja anayekula pamoja nami atanichongea.

19Wakaanza kusikitika na kumwuliza mmoja mmoja: Ni mimi?

20Naye akawaambia: Ninyi kumi na wawili mwenzenu aliyetowelea pamoja nami bakulini ndiye.

21Mwana wa mtu anakwenda njia yake, kama alivyoandikiwa; lakini yule mtu, ambaye Mwana wa mtu atachongewa naye, atapatwa na mambo. Ingalimfalia yule mtu, kama-asingalizaliwa.

Chakula cha Bwana.

22Walipokuwa wakila, akatwaa mkate, akauombea, akaumega, akawapa, akasema: Twaeni! Huu ndio mwili wangu.[#1 Kor. 11:23-25.]

23Kisha akatwaa kinyweo, akashukuru, akawapa, wakanywa wote humo,

24akawaambia: Hii ndiyo damu yangu ya Agano Jipya inayomwagwa kwa ajili ya wengi.[#2 Mose 24:8; Zak. 9:11.]

25Kweli nawaambiani: Tangu sasa sitayanywa tena mazao ya mizabibu mpaka siku ile, nitakapoyanywa mapya katika ufalme wa Mungu.

(26-31: Mat. 26:30-35; Luk. 22:31-34,39.)

26Walipokwisha kuimba wakatoka kwenda mlimani pa michekele.[#Sh. 115—118.]

27Yesu akawaambia: Nyote mtajikwaa, kwani imeandikwa:

Nitampiga mchungaji, kondoo watawanyike;

28lakini nitakapokwisha kufufuliwa nitawatangulia kwenda Galilea.[#Mar. 16:7.]

29Ndipo, Petero alipomwambia: Ijapokuwa, wote wajikwae, lakini mimi sio.

30Yesu akamwambia: Kweli nakuambia: Usiku huu wa leo jogoo atakapokuwa hajawika mara mbili, utakuwa umenikana mara tatu.[#Yoh. 13:38.]

31Naye akakaza mno kusema: Hata ijaponipasa kufa pamoja nawe, sitakukana kabisa. Nao wote wakasema vivyo hivyo.[#Yoh. 11:16.]

Getisemane.

(32-42: Mat. 26:36-46; Luk. 22:40-46.)

32Walipofika mahali, jina lake Getisemane, akawaambia wanafunzi wake: Kaeni hapa, mpaka niishe kuomba![#Yoh. 18:1.]

33Akamchukua Petero na Yakobo na Yohana, akaenda nao, akaanza kuingiwa na kituko na kuhangaika,

34akawaambia: Roho yangu inaumizwa sana na masikitiko, imesalia kufa tu. Kaeni papa hapa, mkeshe![#Sh. 43:5; Yoh. 12:27.]

35Akaendelea mbele kidogo, akaanguka chini, akaomba, ikiwezekana, saa hiyo impite, isimfikie.

36Akasema: Aba baba, yote yanawezekana kwako; kipitishe kinyweo hiki, nisikinywe! Lakini yasifanyike, niyatakayo mimi, ila yafanyike, uyatakayo wewe![#Mar. 10:38.]

37Alipokuja akawakuta, wamelala usingizi, akamwambia Petero: Simoni, umelala usingizi? Hukuweza kukesha saa moja tu?

38Kesheni na kuomba, msije kuingia majaribuni! Roho inataka kuitikia, lakini mwili ni mnyonge.

39Akaenda tena, akaomba na kusema maneno yaleyale.

40Alipokuja tena akawakuta, wamelala usingizi, kwani macho yao yalikuwa mazito, hawakujua ya kumjibu.

41Alipokuja mara ya tatu akawaambia: Mwafuliza kulala usingizi, uchovu uwatoke? Pametimia, saa imefika; tazameni, Mwana wa mtu anatiwa mikononi mwa wakosaji!

42Inukeni, twende! Tazameni, mwenye kunichongea yuko karibu![#Yoh. 14:31.]

Kukamatwa kwa Yesu.

(43-54: Mat. 26:47-58; Luk. 22:47-55; Yoh. 18:2-18.)

43Angali akisema, papo hapo akaja Yuda, mmoja wao wale kumi na wawili, pamoja na kundi la watu wengi wenye panga na rungu waliotoka kwa watambikaji wakuu na kwa waandishi na kwa wazee.

44Lakini mwenye kumchongea alikuwa amewapa kielekezo akisema: Nitakayemnonea ndiye, mkamateni, mwende naye mkimwangalia sana!

45Naye alipofika, mara akamjia, akasema: Mfunzi mkuu! akamnonea;

46ndipo, walipomkamata kwa mikono yao.

47Lakini mmoja wao waliosimama hapo akauchomoa upanga wake, akampiga mtumwa wa mtambikaji mkuu, akamkata sikio.

48Lakini Yesu akajibu, akawaambia: Mmetoka wenye panga na rungu, mnikamate mimi, kama watu wanavyomwendea mnyang'anyi.

49Kila siku nilikuwa kwenu hapo Patakatifu nikifundisha, lakini hamkunikamata; lakini yamekuwapo, Maandiko yatimizwe.

50Hapo waliokuwa naye wakamwacha, wakakimbia wote.

51Kulikuwa na kijana mmoja aliyefuatana naye, alikuwa ameufunika uchi wake kwa kitambaa cha bafta tu. Lakini walipomkamata,

52akakiacha kile kitambaa cha bafta, akakimbia mwenye uchi.

Yesu mbele ya Kayafa.

53Wakampeleka Yesu kwa mtambikaji mkuu. Wakakusanyika wote, watambikaji wakuu na wazee na waandishi.

54Naye Petero akamfuata mbalimbali, mpaka akaingia uani kwa mtambikaji mkuu, akakaa pamoja na watumishi penye mwangaza akiota moto.

(55-65: Mat. 26:59-68; Luk. 22:63-71; Yoh. 18:19-24.)

55Lakini watambikaji wakuu na baraza ya wakuu wote wakamtafutia Yesu ushuhuda, wapate kumwua, lakini hawakuupata.

56Kwani wengi walimshuhudia ya uwongo, lakini ushuhuda wao haukupatana.

57Kisha wakainuka wengine, wakamshuhudia ya uwongo na kusema:[#Yoh. 2:19; 4:21,23.]

58Sisi tumesikia, alivyosema: Mimi nitalivunja Jumba hili la Mungu lililojengwa na mikono, tena nitajenga jingine muda wa siku tatu lisilojengwa na mikono.

59Lakini hata hivyo ushuhuda wao haukupatana.

60Ndipo, mtambikaji mkuu alipoinuka, akaja katikati, akamwuliza Yesu akisema: Hujibu neno, hawa wanayokusimangia?

61Lakini akanyamaza kimya, asimjibu neno. Mtambikaji mkuu akamwuliza tena akimwambia: Wewe ndiwe Kristo, mwana wake Mtukufu?[#Mar. 15:5; Yes. 53:7.]

62Yesu akasema: Mimi ndiye. Nanyi mtamwona Mwana wa mtu, anavyokaa kuumeni kwa nguvu, tena atakavyokuja na mawingu ya mbinguni.[#Sh. 110:1; Dan. 7:13-14.]

63Ndipo, mtambikaji mkuu alipozirarua nguo zake, akasema: Mashahidi tunawatakia nini tena?

64Mmesikia, anavyombeza Mungu. Mwaonaje? Nao wote wakamhukumu kwamba: Amepaswa na kufa.[#Yoh. 19:7.]

65Kisha wengine wakaanza kumtemea mate, tena wakamfunika uso, wakampiga makonde, wakamwambia: Fumbua! Nao watumishi wakamchukua, wakampiga makofi.

Kukana kwa Petero.

(66-72: Mat. 26:69-75; Luk. 22:56-62; Yoh. 18:17,25-27.)

66Naye Petero alipokuwa amekaa chini uani, akaja mmoja wao vijakazi wa mtambikaji mkuu.

67Alipomwona Petero, alivyoota moto, akamchungulia, akasema: Hata wewe ulikuwa pamoja na yule Yesu wa Nasareti.

68Akakana akisema: Sijui, wala sitambui, wewe unayoyasema. Kisha akatoka kufika nje ukumbini.

69Yule kijakazi alipomwona, akaanza tena kuwaambia waliosimama pale: Huyu ni mwenzao.

70Lakini akakana tena. Tena punde kidogo waliosimama pale wakamwambia Petero: Kweli u mwenzao, kwani nawe u Mgalilea.

71Ndipo, alipoanza kujiapiza na kuapa akisema: Simjui mtu huyo, mnayemsema.

72Mara hiyo jogoo akawika mara ya pili. Hapo Petero akalikumbuka lile neno, kama Yesu alivyomwambia: Jogoo atakapokuwa hajawika mara mbili, utakuwa umenikana mara tatu. Alipovifikiri akaanza kulia.[#Mar. 14:30.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania