Nahumu 1

Nahumu 1

Mapatilizo ya Niniwe na ya Asuri.

1Hili ndilo tamko zito la kuuambia Niniwe yatakayoupata, ni kitabu cha maono, Nahumu wa Elkosi aliyoyaona.

2Bwana ni Mungu mwenye wivu alipizaye;

kwani Bwana ni mlipizaji mwenye makali,

Bwana huwalipiza wapingani wake,

nao wachukivu wake huwashikia makali.

3Bwana ni mvumilivu, mwenye nguvu kuu,

lakini aliye mkosaji hamwachilii, asimpatilize.

Njia yake Bwana imo katika kimbunga na katika upepo

mkali,

nayo mawingu ndiyo mavumbi ya miguu yake.

4Akiikaripia bahari, anaipwelesha,

nayo mito mikubwa yote anaikausha.

Nchi za Basani na za Karmeli zimezimia,

nayo majani na maua ya Libanoni yamezimia.

5Milima hutetemeka mbele yake,

navyo vilima hutikisika;

nayo nchi huinukia usoni pake

pamoja na ulimwengu nao wote wakaamo.

6Yuko nani awezaye kusimama, akimkasirikia?

Au yuko nani awezaye kukaa katika makali yake yenye moto?

Hasira yake ichomayo humwagika kama moto wenyewe,

nayo miamba hupasuliwa nayo.

7Bwana ni mwema, ni ngome siku ya masongano,

huwajua wamkimbiliao.

8Lakini kwa mafuriko ya maji yatosayo

atapamaliza mahali pao wengine,

nao wachukivu wake atawakimbiza gizani.

9Mwawaziaje kumpingia Bwana? Yeye ndiye atakayewamaliza,

masongano yasitokee mara ya pili.

10Ingawa washikamane kama miiba iliyosukwa,

au ingawa waloe kwa mvinyo, wawe majimaji kama mvinyo

zao,

wote pia wataliwa na moto kama majani makavu.

11Mwako wewe ametoka awazaye mabaya ya kumpinga Bwana

kwa mashauri maovu, aliyoyatoa.

12Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Ingawa wakae na kutulia kwa kuwa wengi hivyo, watakatwa, watoweke. Lakini wewe, kama nimekunyenyekeza, sitakunyenyekeza tena.

13Sasa nitayavunja makongwa yao, yakuondokee, nayo mafungo uliyofungwa nitayararua.

14Lakini kwa ajili yako (Asuri) Bwana ameagiza, wenye jina lako wasipewe tena kuzaa, namo nyumbani mwa mungu wako nitavitowesha vinyago vya kuchonga navyo vya kuyeyusha, nawe nitakuchimbia kaburi lako, kwani umeonekana kuwa mwepesi zaidi.[#Dan. 5:27,30.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania