The chat will start when you send the first message.
1Haya ni mambo ya Nehemia, mwana wa Hakalia. Ikawa katika mwezi wa Kisilewu wa mwaka wa ishirini, nilipokuwa Susani mlimo na jumba la mfalme.
2Ndipo, alipokuja Hanani, mmoja wao ndugu zangu, pamoja na watu waliotoka Yuda. Nikawauliza habari za Wayuda waliopona, ndio wale waliosalia, wenzao walipohamishwa, na habari za Yerusalemu.
3Wakaniambia: Yale masao ya watu waliosalia kule jimboni, wenzao walipohamishwa, wamo katika mabaya mengi yawatiayo soni: boma la Yerusalemu lingaliko limebomolewa, nayo malango yake yako vivyo hivyo, yalivyoteketezwa kwa moto.[#2 Mambo 36:19.]
4Nilipoyasikia maneno haya, nikakaa siku zile na kulia machozi kwa kusikitika, nikawa mikifunga mfungo na kumwomba Mungu wa mbinguni,[#Neh. 9:1; Ezr. 9:3.]
5nikasema: E. Bwana Mungu wa mbinguni, u Mungu mkubwa, unaogopesha, lakini wao wakupendao na kuyashika maagizo yako unawatimilizia Agano lako na upole wako.[#Neh. 4:14; Dan. 9:4.]
6Sasa sikio lako na liwe limetegwa, nayo macho yako na yawe wazi, uyasikilize malalamiko ya mtumwa wako, nikulalamikiayo mimi leo mchana na usiku kwa ajili ya wana wa Isiraeli walio watumwa wako, nikikutolea makosa yao wana wa Isiraeli, tuliyokukosea, mimi nami nao wa mlango wa baba yangu tumekosa.
7Tumekufanyizia maovu mengi, hatukuyashika maagizo, wala maongozi, wala maamuzi yako, uliyomwagiza mtumishi wako Mose.
8Likumbuke lile neno, ulilomwagiza mtumishi wako Mose la kwamba: Mtakapoyavunja maagano, mimi nitawatapanya kwenye makabila yote;
9lakini mtakaporudi kwangu na kuyashika maagizo yangu, myafanye, nitawakusanya, ijapo mwe mmekimbizwa mpaka kwenye mapeo ya mbingu; huko nako nitawatoa na kuwapeleka mahali hapo, nilipopachagua, pawe pa kulikalishia Jina langu.[#5 Mose 30:4.]
10Nao ndio watumwa wako na ukoo wako, uliowakomboa kwa nguvu zako kuu na kwa mkono wako unaoshupaa.
11E Bwana, sasa sikio lako na liwe limetegewa maombo ya mtumwa wako na malalamiko ya watumwa wako wanaopendezwa na kulicha Jina lako! Umfanikishe leo mtumwa wako na kumhurumia machoni pa mtu huyu! Kwani nilikuwa mtunza vinywaji kwake mfalme.