Nehemia 2

Nehemia 2

Nehemia anapata ruhusa kwa mfalme kuujenga Yerusalemu.

1Ikawa katika mwezi wa Nisani wa mwaka wa ishirini wa mfalme Artasasta; hapo, mvinyo ilipowekwa mbele yake, nikaichukua hiyo mvinyo, nikampa mfalme; lakini mpaka hapo sijawa nikinuna mbele yake.

2Mfalme akaniuliza: Mbona uso wako unanuna, ukiwa huugui? Hili si jingine, ila ni sikitiko la moyo. Ndipo, nilipoingiwa na woga mwingi sana,

3nikamjibu mfalme: Mfalme na awe mwenye uzima kale na kale! Je? Uso wangu usinune, mji ulio na makaburi ya baba zangu ukiwa umebomoka, nayo malango yake yakiwa yameteketezwa kwa moto?

4Mfalme akaniuliza: Sasa wewe unatakaje? Ndipo, nilipomwomba Mungu wa mbinguni,

5nikamwambia mfalme: Vikiwa vema machoni pako, mfalme, mtumwa wako naye akiwa mwema machoni pako, nitume, niende katika nchi ya Yuda mle mjini mlimo na makaburi ya baba zangu, miujenge!

6Mfalme akaniuliza, naye mkewe alikuwa amekaa kando yake, kwamba: Safari yako itakuwa ya siku ngapi? Utarudi lini? Basi, mfalme akaviona kuwa vema, akanituma, nami nikaagana naye siku za kurudi.

7Kisha nikamwambia mfalme: Vikiwa vema kwake mfalme, na wanipe barua za kuwapelekea wenye amri walioko ng'ambo ya huko ya jito kubwa, waniache, nipite, mpaka nitakapofika Yuda.

8Tena barua kwa Asafu, mtunza miitu ya mfalme, anipe miti ya kutengeneza nguzo za malango ya boma lililoko penye hiyo Nyumba, nayo ya ukuta wa mji na ya nyumba yangu, nitakamoingia. Mfalme akanipa, kwa kuwa mkono wa Mungu wangu ulio mwema ulikuwa na mimi.[#Ezr. 7:6.]

9Nilipofika kwao wenye amri ng'ambo ya huku ya jito kubwa, nikawapa zile barua za mfalme. Tena mfalme alikuwa amenipa hata wakuu wenye vikosi vya askari nao wapanda farasi.

10Sanibalati wa Horoni na mtumishi Tobia wa Waamoni walipoyasikia haya, wakakasirika sanasana, ya kuwa amekuja mtu aliyetaka kuwatafutia wana wa Isiraeli mema.

11Nilipofika Yerusalemu nikakaa huko siku tatu.

12Kisha nikainuka usiku mimi na watu wachache, niliokuwa nao; lakini hakuwako mtu, niliyemwambia Mungu wangu aliyonitia moyoni, niyafanyize Yerusalemu, hata nyama sikuwa naye, isipokuwa yule, niliyempanda.

13Nikatoka usiku huo katika lango la Bondeni, nikashika njia ya kwenda penye kisima cha Joka na penye lango la Jaani, nikawa nikizichungulia kuta za Yerusalemu zilizokuwa zimebomolewa, nayo malango yaliyokuwa yameliwa na moto.

14Nikaendelea, nikafika penye lango la Jicho la Maji, hata penye ziwa la mfalme, lakini nyama, niliyempanda, hakuona mahali pa kupitia.[#Neh. 3:15.]

15Ndipo, nilipokwea katika bonde la kijito usiku uleule, nikawa nikiuchungulia ukuta; kisha nikarudi, nikafika tena kwenye lango la Bondeni, nikarudi nyumbani.

16Lakini wakuu hawakujua, wala nilikokwenda, wala niliyoyafanya; nami mpaka hapo sikuwaambia Wayuda neno lo lote, wala watambikaji, wala wakuu wa mji, wala watawalaji, wala wao wengine, niliowatakia kazi.

17Nikawaambia: Mnayaona haya mabaya yaliyotupata, ya kuwa Yerusalemu ni mabomoko, nayo malango yake yameteketezwa kwa moto. Haya! Njoni, na tulijenge boma la Yerusalemu, tusiendelee kutukanwa!

18Nikawasimulia, mkono wa Mungu ulio mwema ulivyonisaidia, nayo yale maneno, mfalme aliyoniambia. Ndipo, walipoitikia kwamba: Na tuinuke, tujenge! Nayo mikono yao wakaishupaza kufanya kazi njema.

19Lakini Sanibalati wa Horoni na mtumishi Tobia wa Waamoni na Mwarabu Gesemu walipoyasikia, wakatucheka na kutubeza wakisema: Hii kazi yenu, mnayoifanya, ni ya nini? Mwataka kumkataa mfalme na kuacha kumtii?

20Nikawajibu neno nikiwaambia: Mungu wa mbinguni atatupa kuimaliza kazi hii; sisi tulio watumwa wake tutainuka, tujenge. Lakini ninyi hamna fungu humu Yerusalemu wala cho chote kilicho chenu wala ukumbusho tu.[#Ef. 2:12.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania