Nehemia 3

Nehemia 3

Boma la Yerusalemu linajengwa.

1Ndipo, alipoondokea mtambikaji mkuu Eliasibu pamoja na ndugu zake waliokuwa watambikaji, wakalijenga lango la Kondoo. Kisha wakalieua, wakaitia milango yake, kisha wakajenga kufikia penye mnara wa Hamea, wakaueua, wakaendelea kujenga kufikia penye mnara wa Hananeli.

2Mkononi kwake kumoja wakajenga watu wa Yeriko, mkononi kwake kungine akajenga Zakuri, mwana wa Imuri.

3Lango la Samaki wakalijenga wana wa Senaa; walipokwisha kuiunga mihimili yake, wakaitia milango yake na makomeo yake na miti yake ya kukingia.

4Mkononi kwao kumoja akafanya kazi Meremoti, mwana wa Uria, mwana wa Hakosi, mkononi kwao kungine akawa Mesulamu, mwana wa Berekia, mwana wa Mesezabeli, akifanya kazi, kando yao akawa Sadoki, mwana wa Baana, akifanya kazi.

5Kando yao hao Watekoa wakafanya kazi, lakini watukufu wa kwao hawakuziinamisha shingo zao kumfanyizia bwana wao kazi.

6Lango la Kale wakalitengeneza Yoyada, mwana wa Pasea, na Mesulamu mwana wa Besodia; walipokwisha kuiunga mihimili yake wakaitia milango yake na makomeo yake na miti yake ya kukingia.

7Kando yao wakafanya kazi: Melatia wa Gibeoni na Yadoni wa Meronoti na watu wa Gibeoni na wa Misipa, wakapatengeneza hapo penye kiti cha kifalme cha mwenye amri wa nchi zilizoko ng'ambo ya huku ya jito kubwa.

8Kando yao wakafanya kazi Uzieli, mwana wa Harihaya, pamoja na wafua dhahabu; kando yake akafanya kazi Hanania, mwana wa chama cha watengeneza manukato; nao wakaujenga Yerusalemu mpaka penye Ukuta Mpana.

9Kando yake akafanya kazi Refaya, mwana wa Huri, aliyekuwa mkuu wa nusu ya mtaa wa Yerusalemu.

10Kando yake akafanya kazi Yedaya, mwana wa Harumafu, hapo palipoielekea nyumba yake; kando yake akafanya kazi Hatusi, mwana wa Hasabunia.

11Kipande kingine wakakifanyizia kazi Malkia, mwana wa Harimu, na Hasabu, mwana wa Pahati-Moabu, wakautengeneza nao mnara wa Tanuru.

12Kando yake akafanya kazi Salumu, mwana wa Halohesi, aliyekuwa mkuu wa nusu ya pili ya mtaa wa Yerusalemu, yeye na wanawe wa kike.

13Lango la Bondeni wakalitengeneza Hanuni na wenyeji wa Zanoa; walipokwisha kulijenga, wakaitia milango yake na makomeo yake na miti yake ya kukingia, kisha wakatengeneza mikono elfu ya boma mpaka lango la Jaani.

14Lango la Jaani akalitengeneza Malkia, mwana wa Rekabu, aliyekuwa mkuu wa mtaa wa Beti-Keremu, alipokwisha kulijenga, akalitia milango yake na makomeo yake na miti yake ya kukingia.

15Lango la Jicho la Maji akalitengeneza Saluni, mwana wa Koli-Hoze, aliyekuwa mkuu wa mtaa wa Misipa; alipokwisha kulijenga na kulifunika juu, akaitia milango yake na makomeo yake na miti yake ya kukingia; kisha akaujenga ukuta penye ziwa la Sela karibu ya bustani ya mfalme mpaka penye ngazi inayoshuka toka mjini kwa Dawidi.[#Yoh. 9:7.]

16Nyuma yake akafanya kazi Nehemia, mwana wa Azibuku, aliyekuwa mkuu wa nusu ya mtaa wa Beti-Suri mpaka hapo panapoyaelekea makaburi ya Dawidi penye lile ziwa lililotengenezwa hapo, tena mpaka nyumba ya mafundi wa vita.

17Nyuma yake wakafanya kazi Walawi: Rehumu, mwana wa Bani; kando yake akafanya kazi Hasabia, mkuu wa nusu ya mtaa wa Keila, ni kazi iliyoupasa mtaa wake.

18Nyuma yake wakafanya kazi ndugu zao: Bawai, mwana wa Henadadi, aliyekuwa mkuu wa nusu ya pili ya mtaa wa Keila.

19Kando yake akafanya kazi Ezeri, mwana wa Yesua, aliyekuwa mkuu wa Misipa, akatengeneza kipande kingine kielekeacho pa kupandia penye nyumba ya mata huko pembeni.

20Nyuma yake akafanya kazi na kujihimiza Baruku, mwana wa Zabai, akatengeneza kipande kingine kutoka hapo pembeni kufikia mlango wa nyumba ya mtambikaji mkuu Eliasibu.[#Neh. 3:1.]

21Nyuma yake akafanya kazi Meremoti, mwana wa Uria, mwana wa Hakosi, akatengeneza kipande kingine kutoka mlango wa nyumba ya Eliasibu kufikia mwisho wa nyumba ya Eliasibu.[#Ezr. 8:33.]

22Nyuma yake wakafanya kazi watambikaji waliokaa katika nchi ya tambarare.

23Nyuma yao wakafanya kazi Benyamini na Hasubu, wakapatengeneza panapoielekea nyumba yao; nyuma yao wakafanya kazi Azaria, mwana wa Masea, mwana wa Anania, kando ya nyumba yake.

24Nyuma yake akafanya kazi Binui, mwana wa Henadadi, akatengeneza kipande kingine kutoka nyumba ya Azaria mpaka pembeni panapogeuka.

25Palali, mwana wa Uzai, akapajenga panapoelekea hapo pembeni na mnara wa juu unaotokea penye nyumba ya mfalme karibu ya uani pa kifungoni. Nyuma yake akajenga Pedaya, mwana wa Parosi.[#Yer. 32:2; 33:1.]

26Watumishi wa Nyumbani mwa Mungu walikuwa wanakaa Ofeli kufikia hapo panapoelekea lango la Maji lililoko upande wa maawioni kwa jua, ni hapo panapotokea mnara.

27Nyuma yao wakafanya kazi Watekoa, wakatengeneza kipande kingine kutoka panapoelekea ule mnara mkubwa unapotokea kufikia ukuta wa Ofeli.

28Juu ya lango la Farasi wakafanya kazi watambikaji, kila mmoja akapatengeneza panapoielekea nyumba yake.[#2 Fal. 11:16.]

29Nyuma yao akafanya kazi Sadoki, mwana wa Imeri, akapatengeneza panapoielekea nyumba yake; nyuma yake akafanya kazi semaya, mwana wa Sekania, mlinzi wa lango lielekealo upande wa maawioni kwa jua.

30Nyuma yake wakafanya kazi Hanania, mwana wa Selemia, na Hanuni, mwana wa sita wa Salafu, wakatengeneza kipande kingine. Nyuma yake akafanya kazi Mesulamu, mwana wa Berekia, akapatengeneza panapokielekea chumba chake.

31Nyuma yake akafanya kazi Malkia, mwana wa chama cha wafua dhahabu, akatengeneza kipande kuifikia nyumba ya watumishi wa Nyumbani mwa Mungu na ya wachuuzi, ni hapo panapoelekea lango la Ukaguzi hata pa kupandia pembeni.

32Tena hapo katikati ya kupandia pembeni na lango la Kondoo wakapatengeneza wafua dhahabu na wachuuzi.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania