Nehemia 4

Nehemia 4

Jengo linaendelea, ijapo adui wajaribu kulizuia.

1Ikawa, Sanibalati aliposikia, ya kuwa sisi tunalijenga boma, ndipo, makali yake yalipowaka moto, akakasirika sana, akawafyoza Wayuda.[#Neh. 2:19.]

2Akasema mbele ya ndugu zake na mbele ya vikosi vya Samaria kwamba: Hawa Wayuda wasio na nguvu wanafanya nini? Je Wanajijengea wenyewe? Watatoa hapo ng'ombe za tambiko? Je? Siku itafika, watakapozimaliza kazi hizo? Nayo mawe watawezaje kuyafufua katika machungu ya mavumbini? Nayo yamekwisha kuteketea kale!

3Baadaye Mwamoni Tobia aliyesimama kando yake akasema: Yo yote, watakayoyajenga, kama mbwa wa mwitu tu atayapandia, atayatawanya mawe ya boma lao.

4Mungu wetu, sikia, jinsi sisi tulivyowageukia kuwa wa kubezwa tu! Kawarudishie matusi yao vichwani pao ukiwatoa, wanyang'anywe mali zao katika nchi, watakakotekwa![#Sh. 7:17.]

5Wala usizifunike manza zao, walizozikora, wala makosa yao yasifutwe usoni pako! Kwani mbele yao hawa wanaojenga wamesema maneno ya kukasirisha.

6Basi, tukalijenga boma; kuta zote za boma zilipopandishwa na kufika katikati ya urefu wa juu, watu wakajikaza kujenga.

7Ikawa, Sanibalati na Tobia na Waarabu na Waamoni na Waasdodi waliposikia, ya kuwa jengo la kuta za boma la Yerusalemu linaendelea, ya kuwa wameanza kupaziba palipokuwa pamebomoka, makali yao yakawaka moto.

8Wakaapiana wote pamoja kuja Yerusalemu kupigana nao na kuwafanyia matata.

9Tukamlalamikia Mungu, tukaweka walinzi po pote, wawalindie mchana na usiku.

10Wayuda wakasema: Nguvu za wachukuzi zimekwisha, hujikwaa tu, nayo mavumbi ni mengi, kwa hiyo hatuwezi kuendelea kulijenga boma.

11Nao wapingani wetu wakasema: Wasijue, wala wasituone, mpaka tutokee katikati yao na kuwaua, wazikomeshe kazi zao!

12Lakini Wayuda waliokaa kandokando yao walipotuambia hata mara kumi wakitoka po pote vijijini mwao: Sharti mrudi kwetu,

13ndipo, nilipoweka watu nyuma ya boma mahali pakavu palipokuwa chini kidogo, hapo nikawaweka milango kwa milango wenye panga na mikuki na pindi zao.

14Nikawatazama, kisha nikaondoka, nikawaambia wakuu wa miji na watawalaji na watu wote wengine pia: Msiwaogope! Ila mkumbukeni Bwana aliye mkuu mwenye kuogopesha! Wapiganieni ndugu zenu na wana wenu wa kiume na wa kike na wake zenu na nyumba zenu![#Neh. 1:5.]

15Adui zetu walipokwisha kusikia, ya kuwa tumeyajua mambo yao, ya kuwa Mungu amelivunja shauri lao, basi, sisi tukarudi sote kwenye boma kila mtu kwa kazi yake.[#Iy. 5:12.]

16Tangu siku hiyo waliofanya kazi walikuwa nusu tu ya vijana wangu, nusu yao wengine walishika mikuki na ngao na pindi na shati zao za vyuma, nao wakuu wakawasimamia watu wote wa mlango wa Yuda,

17waliolijenga boma. Lakini wachukuzi waliopagaa mizigo kwa mkono mmoja wakafanya kazi, kwa mkono mwingine wakashika mata.

18Nao waliojenga kila mtu akawa amejifunga upanga wake kiunoni pake, naye mpiga baragumu akawa amesimama kando yangu.

19Nikawaambia wakuu wa miji na watawalaji na watu wengine wote pia: Hapa, tunapofanyia kazi zetu za kujenga, ni parefu mno, nasi tuko tumetawanyika ukutani, tunasimama mbali kidogo, kila mtu na mwenziwe;

20kwa hiyo hapo, mtakaposikia, baragumu likilia mahali, paendeeni, mkusanyike kwetu sisi! Naye Mungu wetu atatupigia vita hivi.

21Ndivyo, tulivyozifanya kazi zetu, nusu yao wakishika mikuki tangu hapo, jua lilipokucha, hata nyota zilipotokea.

22Hapo ndipo, nilipowaambia watu: Kila mtu na kijana wake sharti walale humu Yerusalemu, na usiku wawe walinzi, tena mchana wafanye kazi!

23Hapo wala mimi wala ndugu zangu wala vijana wangu wala walinzi walionifuata, sisi sote hatukuzivua nguo zetu; hata tulipokwenda mtoni, kila mtu alishika mata yake.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania