The chat will start when you send the first message.
1Siku ya ishirini na nne ya mwezi huo wana wa Isiraeli wakakusanyika wakifunga mfungo na kuvaa magunia na kujitia mchanga vichwani.
2Waliokuwa wa uzao wa Kiisiraeli wenyewe wakajitenga na wenzao wote wa kabila jingine, kisha wakasimama wakiyaungama makosa yao na maovu, baba zao waliyoyafanya.
3Wakainuka, wasimame hapohapo, walipokuwa, wakasoma katika kitabu cha Maonyo ya Bwana Mungu wao saa tatu, saa tatu nyingine wakaungama na kumwangukia Bwana Mungu wao.
4Kisha Yesua na Banai, Kadimieli, Sebania, Buni, Serebia, Bani na Kenani wakatokea wakisimama hapo juu, Walawi wanaposimama, wakamlilia Bwana Mungu wao kwa kupaza sauti sana.
5Kisha Walawi Yesua nao Kadimieli, Bani, Hasabunia, Serebia, Hodia, Sebania na Petaya wakawaambia: Inukeni, mtukuzeni Bwana aliye Mungu wenu tangu kale hata kale! Watu na walitukuze Jina lako tukufu lililo kuu kupita matukuzo yote na sifa zote.
6Bwana, wewe ndiwe peke yako; wewe uliziumba mbingu, hizo mbingu zilizoko juu kuliko mbingu zote na vikosi vyao vyote, hata nchi nayo yote yaliyoko, hata bahari nayo yote yaliyomo; wewe ndiwe unayewapa wao wote kuwa wenye uzima, navyo vikosi vya mbinguni hukuangukia.
7Bwana Mungu, wewe ndiwe uliyemchagua Aburamu, ukamtoa Uri kwao Wakasidi, ukampa jina la Aburahamu.[#1 Mose 11:31; 17:5.]
8Ulipouona moyo wake kuwa mwelekevu mbele yako, ukafanya agano naye la kumpa nchi za Wakanaani na za Wahiti na za Waamori na za Waperizi na za Wayebusi na za Wagirgasi, uwape wao wa uzao wake, ukalitimiza neno lako, kwani wewe ndiwe mwongofu.[#1 Mose 15:18-21.]
9Ulipoyaona mateso ya baba zetu katika nchi ya Misri, ukavisikia vilio vyao kwenye bahari ya Ushami,[#2 Mose 3:7.]
10ndipo, ulipotoa vielekezo na vioja kwake Farao na kwa watumishi wake wote na kwa watu wote wa nchi yake, kwani ulijua, ya kuwa waliwakorofisha, ukajipatia Jina, kama lilivyo hata leo hivi.
11Ukaitenganisha bahari mbele yao, wakapita pakavu baharini katikati, nao waliowakimbiza ukawatupa vilindini, kama jiwe linavyotupwa katika maji yenye nguvu.[#2 Mose 14:21; 15:5,10.]
12Ukawaongoza mchana kwa wingu jeusi, tena usiku kwa wingu lenye moto kuwamulikia hiyo njia, waliyoishika.[#2 Mose 13:21.]
13Mlimani kwa Sinai ulishuka kusema nao toka mbinguni, ukawapa maamuzi yanyokayo na Maonyo ya kweli na maongozi na maagizo mema.[#2 Mose 19:18; 20:1.]
14Ukawajulisha siku yako takatifu ya kupumzikia, ukawaagiza magizo na maongozi na maonyo kinywani mwa mtumishi wako Mose.
15Ukawapa vyakula toka mbinguni vya kuzikomesha njaa zao, ukatoa maji miambani ya kuzikomesha kiu zao, ukawaambia, ya kama wataingia katika nchi hii, waichukue, iwe yao, kwa kuwa uliuinua mkono wako, kwamba utawapa.[#2 Mose 16:4,14; 17:6.]
16Lakini wao baba zetu wakajikuza, wakazishupaza kosi zao, hawakuyasikia maagizo yako.[#2 Mose 32:9.]
17Wakakataa kabisa kusikia, hawakuvikumbuka vioja vyako, ulivyovifanya kwao, wakazishupaza kosi zao, kwa upingani wao wakajitakia mkuu, wapate kurudi utumwani mwao. Lakini wewe Mungu huwaondolea watu makoa, u mwenye utu na huruma, tena mwenye uvumilivu na upole mwingi, kwa hiyo hukuwaacha.[#2 Mose 34:6; 4 Mose 14:4.]
18Hata hapo, walipojitengenezea ndama ya dhahabu kwa kuziyeyusha na kusema: Huyu ndiye Mungu wako aliyekutoa Misri, waliposema masimango makuu,[#2 Mose 32:4.]
19hapo napo hukuwaacha kule nyikani kwa huruma zako nyingi, wala wingu jeusi halikuondoka mchana kwao kuwaongoza njiani, wala wingu lenye moto halikuondoka usiku kuwamulikia hiyo njia, waliyoishika.
20Ukawapa nayo roho yako njema ya kuwaerevusha, tena hukuwanyima Mana zako vinywani mwao, ukawapa nayo maji ya kuzikomesha kiu zao.[#4 Mose 11:25.]
21Ukawatunza vema miaka arobaini njiani, wasikose kitu; mavazi yao hayakuchakaa, wala miguu yao haikuvimba.[#5 Mose 8:4.]
22Ukawapa nchi za kifalme pamoja na watu wao, ukawagawia nchi huko na huko, ziwe mafungu yao, wakaichukua nchi ya Sihoni na nchi ya mfalme wa Hesiboni na nchi ya Ogi, mfalme wa Basani.[#4 Mose 21:24,35.]
23Ukazidisha wana wao kuwa wengi kama nyota za mbinguni, ukawaingiza katika nchi hii, uliyowaambia baba zao, ya kuwa wataiingia, iwe yao.
24Wana wao wakaiingia nchi hii, wakaichukua, iwe yao, ukawanyenyekeza wenyeji wa nchi hii mbele yao, wale Wakanaani, ukawatia mikononi mwao wafalme wao pamoja na watu wa nchi hii, wawafanyizie, kama walivyotaka.[#Yos. 12.]
25Wakateka miji yenye maboma na nchi yenye manono, wakachukua nyumba zilizojaa mema yote, ziwe zao, hata visima vilivyochimbuliwa miambani, nayo mizabibu na michekele na miti mingi ya matunda, wakala, wakashiba, wakanenepa, wakaufurahia wema wako ulio mkubwa.[#5 Mose 6:10-11; 32:15.]
26Lakini wakakataa kutii, wakakuinukia, wakayatupa Maonyo yako nyuma yao, nao wafumbuaji wako wakawaua, kwa kuwa waliwaumbua kwa ushuhuda wao, wawarudishe kwako, wakasema masimango makuu.
27Kwa hiyo ukawatoa na kuwatia mikononi mwao waliowasonga, wakawasonga kweli; lakini hizo siku za kusongeka kwao walipokulilia, ukawasikia toka mbinguni, tena kwa huruma zako nyingi ukawapatia waokozi, wakawaokoa mikononi mwao waliowasonga.[#Amu. 3:9,15.]
28Walipopata utulivu wakarudia kuyafanya yaliyo mabaya machoni pako, ukawaacha tena mikononi mwa adui zao, wawatawale. Lakini walipokulilia tena, ndipo, wewe ulipowasikia toka mbinguni, ukawaponya kwa huruma zako mara nyingi.[#Amu. 2:8-21.]
29Nawe ukawaumbua kwa ushuhuda wako, upate kuwarudisha, wayafuate Maonyo yako, lakini wao wakajikuza, hawakuyasikia maagizo yako, nayo maamuzi yako wakayakosea, tena mtu akiyafanya hujipatia kuishi. Wakakutolea mabega makatavu, nazo kosi zao wakazishupaza, hawakusikia.[#3 Mose 18:5.]
30Lakini wewe ukawavumilia miaka mingi, ukawaumbua kwa ushuhuda wa Roho yako iliyowatokea vinywani mwa wafumbuaji wako, lakini hawakusikiliza; ndipo, ulipowatia mikononi mwao makabila ya nchi hizi.[#Yer. 7:25-26; 44:4-6.]
31Lakini kwa huruma zako nyingi hukuwaangamiza kabisa, wala hukuwaacha, kwani wewe ndiwe Mungu mwenye utu na huruma.[#Omb. 3:22.]
32Sasa Mungu wetu uliye Mungu mkuu mwenye uwezo wa kutia woga, unashika maagano ya upole! Yasiwe madogo mbele yako masumbuko yote yaliyotupata sisi, wafalme wetu na wakuu wetu na watambikaji wetu na wafumbuaji wetu na baba zetu nao wote walio ukoo wako tangu hapo, wafalme wa Asuri walipotujia hata siku hii ya leo.[#Neh. 1:5.]
33Wewe u mwongofu katika hayo yote yaliyotujia, kwani ulifanya yaliyo kweli, lakini sisi tukafanya maovu.[#Ezr. 9:15; Dan. 9:5,7.]
34Nao wafalme wetu na wakuu wetu na watambikaji wetu na baba zetu hawakuyafanya Maonyo yako, masikio yao hawakuyategea maagizo yako wala ushuhuda wako, uliowashuhudia.
35Ijapo uliwapa ufalme wao, ukawatolea wema wako mwingi, ukawapa nchi kubwa yenye vinono, waione na macho yao, lakini wao hawakukutumikia, wala hawakurudi na kuyaacha matendo yao mabaya.
36Kwa hiyo sisi tu watumwa katika nchi, uliyowapa baba zetu, wayale mazao yake na mema yake, tazama, kuku huku sisi tu watumwa.
37Mapato yake mengi ni yao wafalme, uliotupa, watutawale kwa ajili ya makosa yetu, nao wanaitawala hata miili yetu na nyama wetu wa kufuga, kama inavyowapendeza. Kweli sisi tumo katika masongano makubwa.
38Kwa ajili ya haya yote sisi tunafanya agano la kweli, tunaliandika na kulitia muhuri ya wakubwa wetu na ya Walawi wetu na ya watambikaji wetu.