4 Mose 1

4 Mose 1

Hesabu ya wapiga vita wa Kiisiraeli.

1Siku ya kwanza ya mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya kutoka kwao katika nchi ya Misri Bwana akamwambia Mose katika nyika ya Sinai Hemani mwa Mkutano kwamba:

2Toeni jumla yao wote walio mkutano wa wana wa Isiraeli kwa ndugu zao na kwa milango ya baba zao, mkiyahesabu majina ya wana waume wote kichwa kwa kichwa.

3Kuanzia kwao wenye miaka ishirini na zaidi wewe na Haroni mwakague wote pia wanaoweza kwenda vitani kwao Waisiraeli, kikosi kwa kikosi.

4Tena mchukue kuwa nanyi kwa kila shina moja mtu mmoja aliye kichwa chao walio wa mlango wa baba yake.

5Nayo haya ndiyo majina yao, ninaowataka, wasimame pamoja nanyi: wa Rubeni Elisuri, mwana wa Sedeuri;

6wa Simeoni Selumieli, mwana wa Surisadai;[#2 Mose 6:23.]

7wa Yuda Nasoni, mwana wa Aminadabu;

8wa Isakari Netaneli, mwana wa Suari;

9wa Zebuluni Eliabu, mwana wa Heloni;[#1 Mambo 7:26.]

10wa wana wa Yosefu: wa Efuraimu Elisama, mwana wa Amihudi, wa Manase Gamulieli, mwana wa Pedasuri;

11wa Benyamini Abidani, mwana wa Gideoni;

12wa Dani Ahiezeri, mwana wa Amisadai;

13wa Aseri Pagieli, mwana wa Okrani;

14wa Gadi Eliasafu, mwana wa Deueli;

15wa Nafutali Ahira, mwana wa Enani.

16Hawa ndio wateule wa mkutano walio wakuu wa mashina ya baba zao, nao ndio waliokuwa vichwa vya maelfu ya Waisiraeli.

17Mose na Haroni wakawachukua watu hawa waliotajwa majina yao,

18wakaukusanya mkutano wote siku ya kwanza ya mwezi wa pili; ndipo, walipoandikwa katika vitabu vya vizazi kwa ndugu zao na kwa milango ya baba zao; yakahesabiwa kichwa kwa kichwa majina yao waliokuwa wenye miaka ishirini na zaidi;

19kama Bwana alivyomwagiza Mose, ndivyo, alivyowakagua nyikani kwa Sinai.

20Wana wa Rubeni, mwanawe wa kwanza wa Isiraeli, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina kichwa kwa kichwa, waume wote wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani,

21jumla yao wa shina la Rubeni walikuwa watu 46500.

22Wana wa Simeoni, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, walipokaguliwa na kuhesabiwa majina kichwa kwa kichwa, waume wote wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani,

23jumla yao wa shina la Simeoni walikuwa watu 59300.

24Wana wa Gadi, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani,

25jumla yao wa shina la Gadi walikuwa watu 45650.

26Wana wa Yuda, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwanda vitani,

27jumla yao wa shina la Yuda walikuwa watu 74600.

28Wana wa Isakari, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani,

29jumla yao wa shina la Isakari walikuwa watu 54400.

30Wana wa Zebuluni, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani,

31jumla yao wa shina la Zebuluni walikuwa watu 57400.

32Wanawe Yosefu wana wa Efuraimu, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani,

33jumla yao wa shina la Efuraimu walikuwa watu 40500.

34Wana wa manase, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani,

35jumla yao wa shina la Manase walikuwa watu 32200.

36Wana wa Benyamini, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani,

37jumla yao wa shina la Benyamini walikuwa watu 35400.

38Wana wa Dani, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani,

39jumla yao wa shina la Dani walikuwa watu 62700.

40Wana wa Aseri, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani,

41jumla yao wa shina la Aseri walikuwa watu 41500.

42Wana wa Nafutali, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani,

43jumla yao wa shina la Nafutali walikuwa watu 53400.

44Hizi ndizo jumla zao, nao waliowakagua ni Mose na Haroni na wale wakuu kumi na wawili wa Waisiraeli waliokuwa kila mmoja wa milango ya baba zao.

45Nao wana wa Isiraeli wote wa milango ya baba zao waliokaguliwa kuwa wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani kwao Waisiraeli,

46jumla yao yote walikuwa watu 603550.[#4 Mose 2:32; 2 Mose 12:37.]

47Lakini Walawi hawakuhesabiwa katikati yao kwa hivyo, shina la baba zao lilivyokuwa.

Kutengwa kwao Walawi.

48Bwana akamwambia Mose kwamba:

49Wao wa shina la Lawi usiwakague, wala jumla yao usiitie katika hiyo ya wana wa Isiraeli.[#4 Mose 2:33; 3:15.]

50Ila utawaweka Walawi kuliangalia Kao l Ushahidi na vyombo vyake vyote nayo yote yaliyomo. Wao ndio watakaolichukua kao na vyombo vyake vyote, nao ndio watakaolitumikia, nao wakipiga makambi yao, hayo na yalizunguke.[#4 Mose 3:23-38; 4.]

51Kao litakapoondoka, wao Walawi ndio watakaolishusha chini; tena Kao litakapofika makambini, Walawi ndio watakaolisimamisha; lakini mgeni atakayelikaribia hana budi kuuawa.

52Wana wa Isiraeli watakapopiga makambi, kila mtu na apige hema katika kambi lake penye bendera ya kikosi cha kwao.

53Lakini Walawi na wapige makambi kulizunguka Kao la Ushahidi, makali yangu yasiwajie wao wa mkutano wa wana wa Isiraeli; kwa hiyo Walawi na wangoje zamu ya kuliangalia Kao la Ushahidi.

54Wana wa Isiraeli wakayafanya yote; kama Bwana alivyomwagiza Mose, ndivyo, walivyofanya kuwa sawasawa.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania