The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose kwamba:[#4 Mose 31:6.]
2Jifanyizie matarumbeta mawili ya fedha, nayo uyatengeneze kwa kufuafua fedha, uyatumie kuwa ya kuwaitia wao wa mkutano, tena ya kuwatangazia, wavunje makambi.
3Yatakapopigwa yote mawili, watu wote wakusanyike kwako hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano.
4Lakini litakapopigwa moja tu, na wakusanyike kwako wakuu tu walio vichwa vyao maelfu ya Waisiraeli.
5Lakini mtakapoyapiga kwa sauti kuu za kushangilia, makambi yaliyoko upande wa maawioni kwa jua na yavunjwe.
6Mtakapoyapiga mara ya pili kwa sauti kuu za kushangilia, makambi yaliyoko upande wa kusini na yavunjwe. Yatakapopigwa kwa sauti kuu za kushangilia yatakuwa ya kuvunjia makambi.
7Lakini kwa kuukusanya mkutano mtayapiga tu pasipo kuzitumia sauti kuu za kushangilia.
8Nao wana wa Haroni walio watambikaji ndio watakaoyapiga hayo matarumbeta. Haya na yawe maongozi ya kale na kale kwenu na kwa vizazi vyenu.
9Napo hapo, mtakapokwenda vitani katika nchi yenu kupigana na adui watakaowasonga, na mshangilie na kuyapiga hayo matarumbeta; ndipo, mtakapokumbukwa mbele ya Bwana Mungu wenu, mwokolewe katika adui zenu.
10Nazo siku za furaha zenu na za sikukuu zenu na za miandamo ya mwezi na myapige, mkizitoa ng'ombe zenu za tambiko za kuteketezwa nzima na za shukrani; ndipo, yatakaposaidia, mkumbukwe mbele ya Mungu wenu. Mimi Bwana ni Mungu wenu.[#3 Mose 23:24; 2 Fal. 11:14; 2 Mambo 7:6.]
11Ikawa siku ya ishirini ya mwezi wa pili katika mwaka wa pili, ndipo, lile wingu lilipoondoka penye Kao la Ushahidi.
12Nao wana wa isiraeli wakaondoka kwenda safari yao na kutoka nyikani kwa Sinai, nalo wingu likatua tena katika nyika ya Parani.
13Kama Bwana alivyoviagiza kinywani mwa Mose, ndivyo, wa kwanza walivyoondoka.[#4 Mose 1—4.]
14Kwanza ikaondoka bendera ya makambi ya wana wa Yuda, vikosi kwa vikosi, naye mkuu wa vikosi vyao alikuwa Nasoni, mwana wa Aminadabu.
15Naye mkuu wa shina la wana wa Isakari alikuwa Netaneli, mwana wa Suari.
16Naye mkuu wa vikosi vya shina la wana wa Zebuluni alikuwa Eliabu, mwana wa Heloni.
17Kisha Kao likashushwa, nao wana wa Gersoni na wana wa Merari wakaondoka na kulichukua Kao.
18Kisha bendera ya makambi ya Rubeni ikaondoka, vikosi kwa vikosi, naye mkuu wa vikosi vyao alikuwa Elisuri, mwana wa Sedeuri.
19Naye mkuu wa vikosi vya shina la wana wa Simeoni alikuwa Selumieli, mwana wa Surisadai.
20Naye mkuu wa vikosi vya shina la wana wa Gadi alikuwa Eliasafu, mwana wa Deueli.
21Kisha wakaondoka Wakehati wakivichukua vyombo vitakatifu; hao walipofika, wale walikuwa wamekwisha kulisimamisha Kao.
22Kisha bendera ya makambi ya wana wa Efuraimu ikaondoka, vikosi kwa vikosi, naye mkuu wa vikosi vyao alikuwa Elisama, mwana wa Amihudi.
23Naye mkuu wa vikosi vya shina la wana wa Manase alikuwa Gamulieli, mwana wa Pedasuri.
24Nye mkuu wa vikosi vya shina la wana wa Benyamini alikuwa Abidani, mwana wa Gideoni.
25Kisha bendera ya makambi ya wana wa Dani ikaondoka, vikosi kwa vikosi; nao walikuwa wanyuma wa makambi yote, naye mkuu wa vikosi vyao alikuwa Ahiezeri, mwana wa Amisadai.
26Naye mkuu wa vikosi vya shina la wana wa Aseri alikuwa Pagieli, mwana wa Okrani.
27Naye mkuu wa vikosi vya shina la wana wa Nafutali alikuwa Ahira, mwana wa Enani.
28Hivyo ndivyo, wana wa Isiraeli walivyokwenda safarini, vikosi kwa vikosi, walipoondoka kwenda safari yao.
29Mose akamwambia Hobabu, mwana wa Reueli wa Midiani, mkwewe Mose: Sisi tunaondoka kwenda mahali, Bwana aliposema: Hapo ndipo, nitakapowapa ninyi; nenda pamoja nasi, tutakufanyizia mema, kwani Bwana amewaambia wana wa Isiraeli, ya kuwa atawapa mema.[#2 Mose 2:18; Amu. 1:16.]
30Lakini akamwambia: Sitakwenda, ila nitarudi kwetu kwa ndugu zangu wa kuzaliwa nao.
31Akamjibu: Usituache! Kwa kuwa unajua mahali, tunapoweza kupiga makambi nyikani, kwa hiyo utakuwa kama macho yetu sisi.
32Ukienda na sisi, tutakufanyizia mema yote, Bwana atakayotufanyizia sisi.
33Walipoondoka mlimani kwa Bwana, wakasafiri siku tatu, nalo Sanduku la Agano la Bwana likawatangulia safari ya hizo siku tatu, liwatafutie mahali pa kupumzikia.
34Nalo wingu la Bwana lilikuwa juu yao mchana, walipoondoka makambini.[#2 Mose 13:21.]
35Kila mara Sanduku lilipoondoka, Mose akasema: Inuka, Bwana, adui zako watawanyike, nao wachukivu wako waukimbie uso wako![#Sh. 68:2; 132:8.]
36Tena lilipotua husema: Rudi, Bwana, kwenye maelfu na maelfu ya Isiraeli!