The chat will start when you send the first message.
1Lakini watu wakanuna, vikawa vibaya masikioni mwa Bwana; naye Bwana alipovisikia, makali yake yakawaka moto, nao moto wa Bwana ukawawakia, ukayala makambi yaliyokuwa pembeni.[#3 Mose 10:2.]
2Ndipo, watu walipomlilia Mose; naye Mose alipomlalamikia Bwana, moto ukakoma.
3Wakapaita mahali pale Tabera (Wakio la Moto), kwa kuwa moto wa Bwana uliwawakia hapo.
4Wafuasi waliokuwa katikati yao wakaingiwa na tamaa kabisa; ndipo, nao wana wa Isiraeli walipolia tena na kusema: Yuko nani atakayetupa nyama, tule?[#2 Mose 16:3.]
5Tunazikumbuka samaki, tulizokula bure tu katika nchi ya Misri, nayo matango na matikiti na mabogaboga na vitunguu na vitunguu somu.
6Lakini sasa roho zetu zimekauka, kwani hivyo vyote haviko, macho yetu huona Mana tu.
7Nazo Mana zilikuwa kama punje za mtama mweupe, tena ukizitazama zilifanana na magwede.[#2 Mose 16:14-31.]
8Watu wakazungukazunguka na kuziokota, wakazisaga kwa mawe ya kusagia, au wakazitwanga katika vinu, kisha wakazipika katika nyungu au wakatengeneza mikate, nayo walipoila ilikuwa kama maandazi penye mafuta matamu.
9Umande ulipoanguka usiku makambini, Mana nazo zikaanguka pamoja nao.
10Mose alipowasikia watu, wakilia ndugu na ndugu pamoja, kila mtu pa kuliingilia hema lake, nayo makali ya Bwana yalipowaka sana, vikawa vibaya machoni pake Mose.
11Kwa hiyo Mose akamwambia Bwana: Mbona unamfanyizia mtumishi wako vibaya? Mbona sioni upendeleo machoni pako? Mbona unanitwika mizigo ya watu hawa wote?
12Je? Aliyewazaa watu hawa wote kwa kuwachukua mimba ni mimi? Unaniambiaje: Wachukue kifuani pako, kama mnyonyeshaji anavyobeba mtoto mchanga, uwapeleke katika nchi, uliyowaapia baba zao kuwapa?
13Nitoe wapi nyama za kuwapa hao watu wote? Kwani wananililia kwamba: Tupe nyama, tule!
14Mimi peke yangu siwezi kuwatunza watu hawa wote, ni mzigo unaonilemea na kunishinda.
15Ukitaka kunifanyizia hivi, niue kabisa, kama nimeona upendeleo machoni pako, nisiendelee kuyaona haya mabaya yaliyonipata.[#2 Mose 32:32.]
16Bwana akamwambia Mose: Toa katika wazee wa Waisiraeli watu 70, uwakusanye kwangu, nao wawe watu, unaowajua, ya kuwa ndio wazee wa watu walio wenye amri, uwapeleke penye Hema la Mkutano, wajipange hapo pamoja na wewe.[#2 Mose 18:21; 24:1.]
17Nami nitashuka, niseme hapo na wewe, nayo roho inayokukalia nitaichukua nusunusu na kuiweka juu yao, wajitwike pamoja na wewe mzigo wa kuwatunza watu hawa, usiuchukue peke yako tena.
18Nao watu hawa waambie: Jitakaseni kuwa tayari kesho, mpate nyama! Kwani mmelia masikioni mwa Bwana kwamba: Yuko nani atakayetupa nyama, tule? kwani huko Misri tuliona mema. Bwana ndiye atakayewapa nyama, mle.[#2 Mose 19:10.]
19Nanyi hamtazila siku moja tu wala siku mbili wala siku tano wala siku kumi wala siku ishirini,
20ila na mzile mwezi mzima, hata zitoke puani mwenu, hata ziwatapishe, kwa kuwa mmemkataa Bwana anayekaa katikati yenu, mlipomlilia kwamba: Kwa nini tumetoka Misri?
21Mose akasema: Watu hawa, nilio nao hapa, ni watu 600000 wanaokwenda kwa miguu, nawe unasema: Nitawapa nyama, wale mwezi mzima!
22Je? Itawezekana kuwachinjia kondoo na mbuzi na ng'ombe, wapate nyama za kutosha? Au inawezekana kuwakusanyia samaki wote wa baharini, wapate samaki nazo za kutosha?[#Yoh. 6:7.]
23Ndipo, Bwana alipomwambia Mose: Je? Mkono wa Bwana umegeuka kuwa mfupi? Sasa utaona, kama neno langu linakupatia kitu, au kama ni la bure.[#Yes. 50:2; 59:1.]
24Kisha Mose akatoka, akawaambia watu hayo maneno ya Bwana; akatoa katika wazee wa Waisiraeli watu 70, akawakusanya, akawapanga, walizunguke Hema.
25Ndipo, Bwana aliposhuka winguni kusema naye, nayo roho iliyomkalia akaichukua nusunusu, akawagawia hao wazee 70; ikawa, roho ilipotua juu yao, ndipo, walipofumbua mambo, lakini hawakuendelea.
26Kulikuwa na watu wawili waliosalia makambini, mmoja jina lake Eldadi, wa pili jina lake Medadi, nao roho ikatua juu yao, kwani walikuwa wameandikwa, lakini hawakutokea Hemani, nao wakafumbua mambo makambini.
27Ndipo, kijana alipopiga mbio kumpasha Mose habari kwamba: Eldadi na Medadi wamo makambini wakifumbua mambo.
28Yosua, mwana wa Nuni, aliyekuwa mtumishi wake Mose tangu ujana wake, akajibu na kusema: Bwana wangu Mose, wakomeshe![#4 Mose 13:16; 2 Mose 24:13.]
29lakini Mose akamwambia: Wewe unaona wivu kwa ajili yangu mimi? Laiti watu wote wa Bwana wangekuwa wafumbuaji, Bwana akiwagawia roho yake![#Mar. 9:39; Yoe. 2:28.]
30Kisha Mose akarudi tena makambini yeye pamoja na hao wazee wa Waisiraeli.
31Ndipo, upepo ulipotoka kwake Bwana, ukatoa tombo upande wa baharini, ukawatawanya po pote penye makambi, kupita katikati yao ulikuwa mwendo wa siku moja upande wa huku, nao upande wa huko ulikuwa mwendo wa siku moja, vivyo hivyo kuyazunguka makambi yote, tena juu ya nchi ilikuwa mikono miwili kuupima wingi wao.[#2 Mose 16:13.]
32Watu wakaondoka, wakawa wakiwaokota hao tombo mchana kutwa na usiku kucha, tena mchana wa kesho; aliyeokota machache aliokota frasila mia, wakawaanika pande zote za kuyazunguka makambi.
33Lakini nyama zilipokuwa zingaliko vinywani mwao, zilipokuwa hazijaisha kutafunwa, ndipo, makali ya Bwana yalipowawakia hao watu, naye Bwana akawapiga hao watu pigo kubwa mno.
34Kwa hiyo walipaita mahali pale Makaburi ya uchu, kwa kuwa walizika hapo watu waliouawa na Uchu mwingi.[#1 Kor. 10:6.]
35Watu walipoondoka hapo penye Makaburi ya Uchu wakaenda Haseroti, wakakaa Haseroti.