4 Mose 12

4 Mose 12

Miriamu anapatwa na ukoma kwa kumkataa Mose.

1Miriamu na Haroni wakamteta Mose kwa ajili ya mke wa Kinubi, aliyemwoa; kwani Mose alioa mwanamke wa Kinubi.[#2 Mose 2:21.]

2Wakasema: Je? Bwana alisema na Mose peke yake tu? Hakusema na sisi nasi? Naye Bwana akayasikia.

3Lakini Mose alikuwa mtu mpole sana kuliko watu wote walioko huku nchini.

4Mara Bwana akamwambia Mose, nao Haroni na Miriamu: Tokeni ninyi watatu, mfike penye Hema la Mkutano! Ndipo, walipotoka wao watatu.

5Bwana akashuka katika lile wingu lililokuwa kama nguzo, akasimama hapo pa kuliingilia Hema, akamwita Haroni na Miriamu, nao wakatokea wote wawili.[#2 Mose 16:10.]

6Akasema: Yasikieni maneno yangu! kama kwenu yuko mfumbuaji, mimi Bwana nitajijulisha kwake kwa maono, niseme naye kwa ndoto.

7Lakini vya mtumishi wangu Mose sivyo vilivyo, kwani yeye ni mwelekevu katika nyumba yangu yote nzima.[#Ebr. 3:2.]

8Nasema naye kinywa kwa kinywa, naye huniona mimi Bwana, nilivyo, haoni kivulivuli tu au mfano tu; kwa nini ninyi hamkuogopa kuteta na mtumishi wangu Mose?[#2 Mose 33:11,23.]

9Makali ya Bwana yakawawakia, naye akaenda zake,

10nalo wingu likaondoka juu ya Hema; walipotazama, Miriamu alikuwa mwenye ukoma uliokuwa mweupe kama chokaa juani. Haroni naye alipomgeukia Miriamu akamwona, ya kuwa ni mwenye ukoma.[#5 Mose 24:9.]

11Ndipo, Haroni alipomwambia Mose: E Bwana wangu, usitutwike hilo kosa letu, tulilolikosa kwa upumbavu!

12Huyu umbu letu asiwe kama mfu aliyekwisha kuliwa nusu ya nyama za mwili wake hapo, alipotoka tumboni mwa mama yake.

13Mose akamlilia Bwana kwamba: E Mungu, ninakuomba sana, umponye.[#2 Mose 15:26.]

14Bwana akamwambia Mose: Kama baba yake angalimtemea mate usoni pake, hangaliona soni siku saba? Na afungiwe siku saba nje ya makambi, baadaye na arudishwe tena.[#3 Mose 13:46.]

15Kwa hiyo Miriamu akafungiwa nje ya makambi siku saba, nao watu hawakuondoka kwenda safari yao, mpaka Miriamu akarudishwa.

16Kisha watu wakaondoka Haseroti kwenda safari yao, wakapiga makambi katika nyika ya Parani.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania