The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose kwamba:
2Tuma watu kwenda kuipeleleza nchi ya Kanaani, mimi ninayotaka kuwapa wana wa Isiraeli. Kila shina la baba zao na litoe mtu mmoja, mtakayemtuma, nao wote wawe wakuu kwao.
3Kwa kuagizwa na Bwana Mose akawatuma kutoka kule nyikani kwa Parani, nao watu hao wote walikuwa vichwa vya wana wa Isiraeli.
4Nayo haya ndiyo majina yao: wa shina la Rubeni Samua, mwana wa Zakuri,
5wa shina la Simeoni Safati, mwana wa Hori,[#Yos. 14:7.]
6wa shina la Yuda Kalebu, mwana wa Yefune,
7wa shina la Isakari Igali, mwana wa Yosefu,
8wa shina la Efuraimu Hosea, mwana wa Nuni,[#4 Mose 13:16; 1 Mambo 7:27.]
9wa shina la Benyamini Palti, mwana wa Rafu,
10wa shina la Zebuluni Gadieli, mwana wa Sodi,
11wa shina la Yosefu wa shina la Manase Gadi, mwana wa Susi,
12wa shina la Dani Amieli, mwana wa Gemali,
13wa shina la Aseri Seturi, mwana wa Mikaeli,
14wa shina la Nafutali Nabi, mwana wa Wofusi,
15wa shina la Gadi Gueli, mwana wa Maki.
16Haya ndiyo majina ya wale watu, Mose aliowatuma kuipeleleza nchi. Lakini Hosea, mwana wa Nuni, Mose akamwita Yosua.[#4 Mose 11:28.]
17Mose alipowatuma kwenda kuipeleleza nchi ya Kanaani akawaambia: Pandeni huku kusini, kisha mpande milimani.
18Mwitazame hiyo nchi, ilivyo, nao watu wanaokaa huko, kama ni wanguvu, au kama ni wanyonge, kama ni wachache, au kama ni wengi.
19Itazameni hiyo nchi, wale watu wanayoikaa, kama ni jema, au kama ni mbaya, nayo miji, wale watu wanayoikaa, itazameni, itazameni, kama ni makambikambi tu, au kama ni miji yenye maboma.
20Nchi itazameni, kama ni yenye wiva, au kama haizai, kama iko miti, au kama hakuna. Tena jipeni mioyo, mchukue matunda ya nchi hiyo! Nazo siku zile zilikuwa siku za malimbuko ya mizabibu.
21Kisha wakaenda kupanda huko, wakaipeleleza nchi toka nyika ya Sini mpaka Rehobu kwenye njia ya kwenda Hamati.
22Kisha wakapanda upande wa nchi ya kusini, wakafika Heburoni; ndiko, walikokaa Ahimani, Sesai na Talmai, wana wa Anaki. Nao Heburoni ulikuwa umejengwa miaka saba kabla ya Soani wa Misri.
23Walipofika penye kijito cha Eskoli, wakakata huko tawi la mzabibu lenye kichala, wakalichukua mpikoni watu wawili, wakachukua hata komamanga na kuyu.
24Mahali pale wakapaita Kijito cha Eskoli (Kichala) kwa ajili ya hicho kichala, wana wa Isiraeli walichokikata huko.
25siku 40 zilipopita, wakarudi, kwa kuwa walikwisha kuipeleleza hiyo nchi.
26Wakaja, wakafika kwa Mose na Haroni na kwa mkutano wote wa wana wa Isiraeli katika nyika ya Parani kule Kadesi, wakawasimulia wao nao mkutano wote waliyoyaona, wakawaonyesha nayo yale matunda ya hiyo nchi.
27Wakawasimulia kwamba: Tumeiingia nchi, mliyotutuma, ichuruzikayo maziwa na asali, nayo haya ni matunda yake.[#2 Mose 3:8,17.]
28Lakini wale wanaokaa katika hiyo nchi wako na nguvu, nayo miji yao ni mikubwa sana yenye maboma magumu; nao wana wa Anaki tumewaona huko.
29Waamaleki wanakaa katika nchi ya kusini; nao Wahiti na Wayebusi na Waamori wanakaa milimani, nao Wakanaani wanakaa upande wa baharini na kando ya Yordani.
30Naye Kalebu akawatuliza mioyo wale watu mbele ya Mose akisema: Haya! Na tupande, tuichukue hiyo nchi! Kwani tutaweza kuishinda kabisa.[#4 Mose 13:6; 14:6.]
31Lakini wale watu wengine waliopanda naye wakasema: Hatuwezi kupanda, tupigane na hao watu, kwani ndio wenye nguvu kuliko sisi.
32Wakazidi kuisingizia nchi ile, waliyoipeleleza, wakiwaambia wana wa Isiraeli: Hiyo nchi, tuliyoipita kuipeleleza, ndiyo nchi inayowala wenyeji wake, nao watu wote, tuliowaona huko, ni watu warefu mno.
33Huko tumeona hata wale Majitu, ni wana wa Anaki wa mlango wa hao Majitu, nasi tukawa machoni petu kama panzi, tena ndivyo, tulivyokuwa machoni pao.[#5 Mose 9:2.]