The chat will start when you send the first message.
1Ndipo, wao wote wa mkutano walipozipaza sana sauti zao, watu wakalia usiku kucha.
2Wana wote wa Isiraeli wakamnung'unikia Mose na Haroni, nao wote walio wa mkutano wao wakawaambia: Afadhali tungalikufa katika nchi ya Misri au tungekufa huku nyikani![#2 Mose 16:3.]
3Kwa nini Bwana anatupeleka katika nchi ile, tuuawe kwa panga, wake zetu nao watoto wetu watekwe? Haitatufalia zaidi kurudi Misri?[#Sh. 106:24.]
4Wakasemezana wao kwa wao: Na tujipatie mkuu, turudi Misri?
5Ndipo, Mose na Haroni walipojiangusha nyusoni pao mbele ya huo mkutano wote wa wana wa Isiraeli uliokusanyika.[#4 Mose 16:4.]
6Nao Yosua, mwana wa Nuni, na Kalebu, mwana wa Yefune, waliokuwa pamoja nao walioipeleleza hiyo nchi, wakayararua mavazi yao,[#4 Mose 13:16,30.]
7wakauambia mkutano wote wa wana wa Isiraeli kwamba; Ile nchi, tuliyoipita na kuipeleleza, ni nchi njema sanasana.
8Bwana akipendezwa nasi, atatuingiza katika nchi hiyo, atupe, iwe yetu; nayo ni nchi ichuruzikayo maziwa na asali.[#4 Mose 13:27.]
9Ni hili tu, msimpingie Bwana! Tena wale watu wa nchi hiyo msiwaogope, kwani watakuwa kama chakula chetu, nacho kivuli, walichokikimbilia, kimeondoka kwao, naye Bwana yuko pamoja na sisi, kwa hiyo msiwaogope!
10Wao wote wa huo mkutano walipotaka kuwaua na kuwatupia mawe, ndipo, utukufu wa Bwana ulipotokea penye Hema la Mkutano mbele ya wana wote wa Isiraeli.[#2 Mose 16:10; 17:4.]
11Bwana akamwambia Mose: Watu hawa watanitukana mpaka lini? Watakataa mpaka lini kunitegemea? Nami nimevifanya hivyo vielekezo vyote kwao!
12Nitawapiga kwa ugonjwa mbaya uuao, niwatoweshe, kisha nitakufanya wewe kuwa kabila kubwa lenye nguvu kuliko hawa.[#2 Mose 32:10-14.]
13Lakini Mose akamwambia Bwana: Wamisri watavisikia; kwani wewe umewatoa watu hawa kwa nguvu yako katikati yao, ukawaleta huku.
14Nao wenyeji wa nchi hii watasimuliwa, kwani nao wamesikia, ya kuwa wewe Bwana uko katikati ya watu hawa, uliowatokea, wakuone macho kwa macho wewe Bwana, tena ya kuwa wingu lako huwasimamia, ukiwatangulia mchana kwa wingu linalofanana na nguzo, nao usiku kwa wingu le moto linalofanana na nguzo
15Kama ungewaua watu hawa kama mtu mmoja, ndipo, wamizimu waliousikia uvumi wako watakaposema kwamba:
16Kwa kuwa Bwana hakuweza kuwaingiza watu hawa katika nchi hiyo, aliyoiapia kuwapa, kwa hiyo amewachinja nyikani.[#5 Mose 9:28.]
17Sasa nguvu ya Bwana wangu na ionekane kuwa kuu, kama ulivyosema kwamba:
18Bwana ni mwenye uvumilivu na upole mwingi, huondoa manza na mapotovu, lakini mbele yake hakuna asiye mkosaji; nazo manza, baba walizozikora, huzilipisha wtoto, akifikishe kizazi cha tatu na cha nne.[#2 Mose 34:6-7.]
19Waondolee watu hawa manza kwa ukubwa wa upole wako, kama ulivyowaondolea watu hawa makosa yao kutoka Misri mpaka hapa!
20Ndipo, Bwana aliposema: Nimewaondolea makosa kwa hivyo, ulivyowaombea.
21Kwa hivyo, nilivyo Mwenye uzima, ulimwengu wote utaenezwa utukufu wangu.[#2 Mose 9:16.]
22Kwani watu hawa wote waliouona utukufu wangu na vielekezo vyangu, nilivyovifanya Misri na nyikani, wakanijaribu sana mara kumi wakikataa kuisikiliza sauti yangu,
23hawa wote hawataiona nchi, niliyowaapia baba zao kuwapa, kweli wao wote walionitukana hawataiona kabisa.[#Sh. 95:11; Ebr. 3:17-19.]
24Ni mtumishi wangu Kalebu tu aliye mwenye roho nyingine moyoni mwake, akanifuata kwa moyo wote, basi, yeye nitamwingiza katika nchi hiyo, aliyoiingia kwanza, nao wa uzao wake wataichukua kuwa yao,[#Yos. 14:6,9.]
25lakini Waamaleki na Wakanaani watakaa bondeni. Kesho geukeni na kujiendea nyikani mkishika njia ya kwenda kwenye Bahari Nyekundu.
26Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba:
27Itakuwa mpaka lini, watu wa mkutano huu mbaya wakininung'unikia? Nimeyasikia manung'uniko ya wana wa Isiraeli, wao waliponinung'unikia.
28Waambie: Ndivyo, asemavyo Bwana: Kwa hivyo, nilivyo Mwenye uzima, nitawafanyizia yayo hayo, mliyoyasema masikioni mwangu:
29Huku nyikani itaanguka mizoga yenu ninyi nyote mliokaguliwa na kuhesabiwa, mlio wenye miaka ishirini na zaidi, mlioninung'unikia.
30Ninyi nyote hamtaiingia kabisa ile nchi, niliyoiapia na kuuinua mkono wangu, ya kwamba nitawakalisha huko. Kalebu, mwana wa Yefune, na Yosua, mwana wa Nuni, hawa tu wataiona.
31Lakini watoto wenu, mliowasema, ya kama watakuwa mateka, nitawaingiza huko waijue nchi ile, mliyoikataa.
32Lakini mizoga yenu ninyi itaanguka huku nyikani.
33Lakini kwanza wana wenu watakuwa wachungaji nyikani miaka 40, watwikwe ugoni wenu, mpaka mizogo yenu imalizike nyikani.
34Kwa hesabu ya zile siku 40, mlizoipeleleza ile nchi, kila siku moja itahesabiwa kuwa mwaka mmoja; hivyo ndivyo, watakavyotwikwa miaka 40 manza, mlizozikora, mpate kutambua, mambo yanavyoendelea, nikiondoka kwenu.
35Mimi Bwana nimesema, nami nitawafanyizia haya wao wote walio wa mkutano huu mbaya waliokusanyika, wanipingie: huku nyikani watamalizika, kwani huku ndiko, watakakofia.
36Kisha wale watu, Mose aliowatuma kuipeleleza nchi ile, ni wao waliounung'unisha mkutano wote waliporudi na kutoa habari za nchi ile,[#1 Kor. 10:5,10; Yuda 5.]
37hao watu waliozitoa zile habari mbaya za nchi ile wakafa kwa kupigwa na Bwana.
38Lakini Yosua, mwana wa Nuni, na Kalebu, mwana wa Yefune, ndio waliokaa wenye uzima miongoni mwao waliokwenda kuipeleleza ile nchi.[#4 Mose 14:30.]
39Mose alipowaambia wana wote wa Isiraeli maneno haya, wakasikitika sana.
40Kesho yake wakaamka na mapema, wakapanda mlimani juu kileleni na kusema: Basi, tumekwisha kufika huku, sasa twende kupanda mahali pale, Bwana alipotuelekeza! Kwani tumekosa.[#4 Mose 13:17.]
41Lakini Mose akasema: Mbona ninyi mwataka kuitangua amri ya Bwana? Hamtafanikiwa.
42Msipande! Kwani Bwana hamnaye katikati yenu, msipigwe na adui zenu.
43Kwani Waamaleki na Wakanaani wako mbele yenu, nanyi mtaangushwa kwa panga, kwa kuwa mmerudi nyuma na kumwacha Bwana; kwa hiyo Bwana hatakuwa nanyi.
44Lakini kwa kujivuna wakapanda mlimani juu kileleni, lakini Sanduku la Agano la Bwana na Mose hawakutoka makambini.
45Ndipo, Waamaleki na Wakanaani waliokaa huko mlimani walipotelemka, wakawapiga, wakawatawanya mpaka Horma.[#4 Mose 21:3.]