The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Haroni: Wewe na wanao na mlango wa baba yako pamoja na wewe mtatwikwa maovu yatakayoonekana Patakatifu; tena wewe pamoja na wanao mtatwikwa maovu ya utambikaji wenu.[#2 Mose 28:38; 3 Mose 16:32-33.]
2Nao ndugu wa shina la Lawi lililo shina la baba yako uwachukue, waandamane na wewe na kukutumikia wewe pamoja na wanao, mkifanya kazi zenu mbele ya Hema la Ushahidi.
3Kazi zao zinazowapasa kuziangalia ni kukuangalia wewe na kuliangalia Hema lote, wasikaribie tu vyombo vya Patakatifu na meza ya kutambikia, wasife wao nao pamoja nanyi.
4Sharti waandamane na wewe, waziangalie kazi za Hema la Mkutano ziwapasazo kuziangalia za utumishi wote wa kulitumikia Hema, lakini mgeni asiwakaribie ninyi.
5Kazi zenu zinazowapasa ninyi kuziangalia ni kupaangalia Patakatifu na kuiangalia meza ya kutambikia, makali yangu yasiwatokee tena wana wa Isiraeli.[#4 Mose 16:46.]
6Tazama, mimi nimewatoa ndugu zenu Walawi katikati yao wana wa Isiraeli, nikawapa ninyi kuwa vipaji vya Bwana kwa kuutumikia utumishi wote wa Hema la Mkutano.[#4 Mose 3:12,45.]
7Nawe wewe pamoja na wanao sharti mwuangalie utambikaji wenu, mfanye kazi zote za utumishi za meza ya kutambikia nazo za Chumbani mbele ya pazia, kwani ninawapa utambikaji wenu kuwa kipaji mlichopewa, lakini mgeni atakayeukaribia hana budi kuuawa.[#4 Mose 1:51.]
8Bwana akamwambia Haroni: Tazama, mimi nimekupa kuviangalia vipaji vya tambiko vya kunyanyuliwa, ninavyotolewa; kwa hiyo ninakupa vipaji vitakatifu vyote, wana wa Isiraeli wanavyovitoa, kuwa ujira wako wewe na wa wanao wa kupakwa mafuta. Hii na iwe haki yenu ya kale na kale.[#3 Mose 2:3-10; 6:16-18,26-29; 7:6-10.]
9Vitakavyokuwa vitakatifu vyenyewe vitakuwa vyako, visichomwe moto, navyo ni hivi: matoleo yao yote, vilaji vyao vya tambiko na ng'ombe zao za tambiko za weuo nazo za upozi, watakazonitolea mimi, ni matakatifu yenyewe kuwa yako na ya wanao.
10Na myale mahali palipo patakatifu penyewe; wote walio wa kiume na wayale, na yawe matakatifu yako.
11Tena ninakupa wewe na wanao wa kiume na wa kike kuwa vyenu: vipaji vyao vya tambiko, wanavyovitoa vya kunyanyuliwa, navyo vipaji vya tambiko vya wana wa Isiraeli vya kupitishwa motoni viwe vyako; hii na iwe haki yenu ya kale na kale. Kila atakayekuwa nyumbani mwako, akiwa ametakata, na avile.
12Tena mafuta yote yaliyo mazuri mno nazo mvinyo mbichi zilizo nzuri mno nazo ngano, watakazomtolea Bwana za malimbuko, ninakupa wewe.
13Nayo mazao yote ya kwanza ya nchi yao, watakayomtolea Bwana, yatakuwa yako; kila atakayekuwa nyumbani mwako, akiwa ametakata, na ayale.[#2 Mose 23:19; 5 Mose 18:4.]
14Navyo vyo vyote vitakavyotiwa mwiko wa kuwa vyao Waisiraeli vitakuwa vyako.[#3 Mose 27:28; 2 Mose 13:12-13; 34:19-20.]
15Naye kila mwana wa kwanza wa mama yake, kama ni wa mtu au wa nyama wa kufuga, atakuwa wako kwao wote walio wenye miili ya nyama, watu watakaomtolea Bwana, lakini mwana wa mtu utamtoa, akombolewe, vilevile mwana wa nyama aliye mwenye uchafu utamtoa, akombolewe.
16Akiwa mwenye mwezi mmoja utamtoa, akombolewe kwa hivyo, utakavyompima kiasi chake cha fedha, walipe kama fedha tano, lakini fedha hizo zinazotumika Patakatifu, fedha moja kwa thumuni nane.
17Lakini wana wa kwanza wa ng'ombe au wa kondoo au wa mbuzi usiwatoe kukombolewa, kwani ndio watakatifu; damu zao sharti uzinyunyizie meza ya kutambikia, nayo mafuta yao sharti uyachome moto kuwa mnuko mzuri wa moto wa kumpendeza Bwana.
18Lakini nyama zao zitakuwa zako, kama vidari vilivyo vipaji vya tambiko vya kupitishwa motoni au kama mapaja ya kuume yalivyo yako.
19Tena ninakupa vipaji vitakatifu vyote, wana wa Isiraeli watakavyomtolea Bwana kuwa vipaji vya tambiko vya kunyanyuliwa; hivi ninakupa wewe pamoja na wanao wa kiume na wa kike; hii na iwe haki yenu ya kale na kale. Hili sharti liwe agano la kale na kale lisilochujuka kama chumvi, nalo umewekewa wewe pamoja na wanao mbele ya Bwana.
20Kisha Bwana akamwambia Haroni: Katika nchi yao wewe hutapata fungu la nchi litakalokuwa fungu lako katikati yao; mimi ni fungu lako, utakalolipata kuwa lako katikati ya wana wa Isiraeli.[#4 Mose 35; 5 Mose 10:9; 12:12; Yos. 13:14,33.]
21Tena tazama: Wana wa Lawi ninawapa mafungu ya kumi yote yatakayotolewa nao Waisiraeli kuwa fungu lao, ni ujira wa utumishi wao wa kufanya kazi za utumishi wa Hema la Mkutano.[#3 Mose 27:30.]
22Lakini tangu sasa wana wa Isiraeli wasilifikie tena Hema la Mkutano karibu, wasijikoseshe, wakajipatia kufa.
23Ila Walawi tu na wazifanye kazi za utumishi wa Hema la Mkutano, nao ndio watakaotwikwa manza, watakazozikora. Haya sharti yawe maongozi ya kale na kale ya kuviongoza vizazi vyenu, nanyi hamtapata fungu la nchi kuwa lenu katikati ya wana wa Isiraeli.
24Kwani ninawapa Walawi mafungu ya kumi, wana wa Isiraeli watakayoyatoa kuwa vipaji vya tambiko vya kumnyanyulia Bwana; haya ninawapa Walawi kuwa fungu lao, kwa hiyo ninawaambia: Hamtapata fungu la nchi kuwa lenu katikati ya wana wa Isiraeli.
25Bwana akamwambia Mose kwamba:
26Sema nao Walawi, uwaambie: Mtakapoyachukua mafungu ya kumi kwao wana wa Isiraeli, niliyowapa ninyi kuwa fungu lenu kwao, nanyi sharti mtoe humo vipaji vya tambiko vya kumnyanyulia Bwana, navyo sharti viwe fungu la kumi la hayo mafungu ya kumi.
27Navyo hivyo vpaji vyenu vya tambiko vitawaziwa kuwa ngano zenu za mapurio yenu au mafuriko ya makamulio yenu.
28Nanyi mtakapovitoa hivyo vipaji vya tambiko vya kumnyanyulia Bwana vya mafungu yenu ya kumi, mtakayoyachukua kwa wana wa Isiraeli, sharti m mpe mtambikaji Haroni hivyo vipaji vya tambiko, mtakavyovitoa kwenu vya kumnyanyulia Bwana.
29Katika vipaji vyote, mtakavyopewa, sharti mtoe vipaji vya tambiko vyote viwapasavyo kuvitoa vya kumnyanyulia Bwana, nanyi sharti mtoe vile vitakavyokuwa vizuri zaidi vinavyopasa kutolewa humo kuwa vipaji vitakatifu.
30Kwa hiyo uwaambie: Mtakapotoa humo vilivyo vizuri zaidi kuwa vipaji vyenu vya tambiko vya kunyanyuliwa, vitawaziwa kuwa mapato ya Walawi ya mapurio yao na mapato ya makamulio yao.
31Nanyi na mvile mahali po pote ninyi nao walio wa milango yenu, kwani ni mishahara yenu ya utumishi wenu wa Hema la Mkutano.[#Mat. 10:10.]
32Mtakapovitoa vilivyo vizuri zaidi katika mapato yenu kuwa vipaji vya tambiko, basi, hamtajikosesha kwa ajili yao, wala hamtavichafua vipaji vitakatifu vya wana wa Isiraeli, msife.