The chat will start when you send the first message.
1Bwana akawambia Mose na Haroni kwamba:[#3 Mose 22:20; Ebr. 9:13.]
2Haya ndiyo maongozi ya mafunzo, Bwana aliyoyaagiza kwamba: Waambie wana wa Isiraeli, wakupatie ng'ombe mwekundu jike asiye na kilema wala doadoa lo lote, asiyefungwa bado kuvuta gari.
3Kisha mpe mtambikaji Elazari, ampeleke kufika nje ya makambi, ndipo wamchinje machoni pake.
4Kisha mtambikaji Elazari achukue kwa kidole chake damu yake kidogo, ainyunyizie mara saba hapo panapolielekea Hema la Mkutano.[#3 Mose 4:6,17.]
5Kisha wamteketeze machoni pake, nao sharti wateketeze ngozi yake na nyama zake na damu yake pamoja na mavi yake.
6Naye mtambikaji na achukue kipande cha mwangati na kivumbasi na nyuzi nyekundu, azitupe katika huo moto unaomteketeza huyo ng'ombe.[#3 Mose 14:6.]
7Kisha mtambikaji na azifue nguo zake pamoja na kuuogesha mwili wake majini, kisha aingie makambini, lakini atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.
8Naye aliyemteketeza sharti azifue nguo zake majini na kuuogesha mwili wake majini, lakini naye atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.
9Kisha mtu mwenye kutakata na ayazoe majivu yake huyo ng'ombe, ayaweke nje ya makambi mahali palipo penye kutakata, yakae hapo hapo na kuangaliwa, yawe tayari, mkutano wa wana wa Isiraeli watakapoyatumia ya kutengeneza maji ya kunyunyiza, kwani ni ng'ombe ya tambiko ya weuo.
10Naye aliyeyazoa hayo majivu ya huyo ng'ombe sharti azifue nguo zake, lakini atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.
Haya yawe maongozi ya kale na kale kwa wana wa Isiraeli na kwa wageni watakaokaa ugenini katikati yao.
11Atakayegusa mfu wa mtu ye yote atakuwa mwenye uchafu siku saba.
12Naye ajieue kwa yale maji ya kunyunyiza siku ya tatu, ndipo, atakapokuwa siku ya saba mwenye kutakata; lakini asipojieua siku ya tatu wala siku ya saba hatakuwa mwenye kutakata.
13Kila mtu atakayegusa mfu, ni kwamba maiti ya mtu ye yote aliyekufa, asipojieua hulichafua Kao la Bwana; mtu aliye hivyo sharti ang'olewe kwao Waisiraeli. Kwa kuwa hakunyunyiziwa hayo maji ya kunyunyiza, ni mwenye uchafu, nao huo uchafu wake utamkalia vivyo hivyo.[#3 Mose 15:31.]
14Nayo haya maonyo sharti yaangaliwe, mtu akifa hemani: kila atakayeingia humo hemani naye kila atakayekuwamo humo hemani atakuwa mwenye uchafu siku saba.
15Nacho kila chombo kilicho wazi kisichofunikwa na kifuniko cha kukifungia kabisa ni chenye uchafu.
16Hata kila mtu atakayegusa porini mtu aliyeuawa kwa upanga au mfu au mfupa wa mtu au kaburi atakuwa mwenye uchafu siku saba.
17Mtu akiwa mwenye uchafu hivyo, na wachukue majivu machache ya hiyo ng'ombe ya weuo iliyoteketezwa, wayatie chomboni, kisha watie humo maji ya mtoni.
18Kisha mtu mwenye kutakata na achukue kivumbasi, akichovye katika hayo maji, ayanyunyizie lile hema na vyombo vyote vilivyomo nao watu wote waliokuwamo naye yule mtu aliyegusa mfupa wa mzoga wa mtu aliyeuawa kwa upanga au mfu au kaburi.
19Ndivyo, mwenye kutakata atakavyomnyunyizia mwenye uchafu siku ya tatu na siku ya saba; akiisha kumweua hiyo siku ya saba sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, ndivyo, atakavyokuwa jioni mwenye kutakata.
20Lakini mtu akiwa mwenye uchafu pasipo kujieua, basi, aliye hivyo hana budi kung'olewa katika mkutano huu, kwani hupachafua Patakatifu pa Bwana, kwani asiponyunyiziwa hayo maji ya kunyunyiza, ni mwenye uchafu vivyo hivyo.
21Haya yawe kwao maongozi ya kale na kale. Naye yule aliyemnyunyizia mwenzake hayo maji ya kunyunyiza sharti azifue nguo zake. Naye atakayeyagusa hayo maji ya kunyunyiza atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.
22Navyo vyote, mwenye uchafu atakavyovigusa, vitakuwa vyenye uchafu, naye kila mtu, atakayemgusa, atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.