4 Mose 20

4 Mose 20

Kufa kwake Miriamu.

1Mkutano wote wa wana wa Isiraeli walipofika katika nyika ya Sini katika mwezi wa kwanza, watu wakakaa Kadesi. Ndiko, Miriamu alikokufa; kisha akazikwa huko.[#4 Mose 13:21.]

Maji ya Magomvi.

2Wao wa mkutano wasipoona maji huko, wakamkusanyikia Mose na Haroni,[#2 Mose 17:1-7.]

3wakamgombeza Mose wakimwambia kwamba: Afadhali tungalizimia roho pamoja na ndugu zetu waliozimia roho mbele ya Bwana!

4Kwa nini mmelileta kundi lake Bwana katika nyika hii, tujifie pamoja na nyama wetu wa kufuga?

5Kwa nini mlitutoa Misri, mkatuleta mahali hapa pabaya? Huku hatuwezi kupanda mbegu, tena hakuna mikuyu wala mizabibu wala mikomamanga, wala maji tu ya kunywa hayako huku.

6Mose na Haroni wakatoka hapo, walipokusanyika, wakaenda hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano; napo hapo, walipoanguka kifudifudi, utukufu wa Bwana ukawatokea.[#4 Mose 14:10.]

7Bwana akamwambia Mose kwamba:

8Ichukue ile fimbo! Kisha wewe na kaka yako Haroni wakusanyeni wao wote wa mkutano, mseme na mwamba huu machoni pao wote, ndipo, utakapowapa maji yake. Ndivyo, utakavyowatolea maji humu mwambani, uwanyweshe wao wa mkutano pamoja na nyama wao wa kufuga.

9Mose akaichukua fimbo iliyokuwa mbele ya Bwana, kama Bwana alivyomwagiza.

10Kisha Mose na Haroni wakalikusanya kundi la watu mbele ya mwamba, akawaambia: Sikieni, ninyi msiotii! Itakuwaje? Tutaweza kuwatolea ninyi maji humu mwambani?[#Sh. 106:33.]

11Kisha Mose akauinua mkono wake, akaupiga mwamba kwa fimbo yake mara mbili; ndipo, maji yalipotoka mengi, wao wa mkutano wakanywa wenyewe nao nyama wao wa kufuga.

12lakini Bwana akamwambia Mose naye Haroni: Kwa kuwa hamkunitegemea na kunitakasa machoni pao wana wa Isiraeli, kwa hiyo hamtaliingiza kundi hili katika ile nchi, nitakayowapa.[#4 Mose 27:14; 5 Mose 1:37; 3:26; 4:21; 32:51.]

13Maji yale yakaitwa Meriba (Magomvi), kwa kuwa wana wa Isiraeli waligombana na Bwana, naye akajitokeza kwao kuwa mtakatifu.[#Sh. 81:8.]

Waedomu wanawakataza Waisiraeli kupita kwao.

14Kule Kadesi Mose akatuma wajumbe kwa mfalme wa Edomu kwamba: Hivi ndivyo, ndugu yako Isiraeli anavyosema: Wewe unayajua masumbuko yote yaliyotupata:[#1 Mose 32:8; Amu. 11:17; 5 Mose 23:7.]

15baba zetu walishuka Misri, wakakaa huko siku nyingi, nao Wamisri wakatufanyizia mabaya sisi na baba zetu.

16Tulipomlilia Bwana, akatusikia, akatuma malaika, akatutoa Misri. Tazama, sisi tumo humo Kadesi, ndio mji wa mpakani kwenye nchi yako.[#2 Mose 23:20.]

17Sasa tunataka kupita katika nchi yako, lakini hatutaki kupita mashambani wala mizabibuni, wala hatutakunywa maji ya visimani, ila tunataka kuishika njia ya mfalme tu, tusiiache kwenda kuumeni wala kushotoni, hata tuupite mpaka wako mwingine.[#4 Mose 21:22.]

18Lakini Mwedomu akamwambia: Hutapita kwangu. Ila nitatoka mwenye upanga, nipigane na wewe.

19Wana wa Isiraeli wakamwambia: Tunataka kushika njia tu, tena tukinywa maji yako sisi na nyama wetu wa kufuga tutakulipa; hakuna jingine, tunalolitaka, ila kupita tu kwa miguu yetu.

20Lakini akasema: Huna ruhusa kupita. Kisha Waedomu wakatoka wenye watu wengi na wenye mikono ya nguvu, wawazuie.

21Ndivyo, Waedomu walivyowakataza Waisiraeli kupita mipakani kwao; ndipo, Waisiraeli walipogeuka, washike njia ya kupitia kando yao.

Kufa kwake Haroni.

22Kisha wana wa Isiraeli wakaondoka Kadesi, wakafika mkutano wao wote kwenye mlima wa Hori.

23Huko kwenye mlima wa Hori kwenye mipaka ya nchi ya Edomu Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba:

24Sasa Haroni atachukuliwa, awe pamoja nao walio wa ukoo wake, kwani hataingia katika nchi ile, nitakayowapa wana wa Isiraeli, kwa kuwa mlikibishia kinywa changu kwenye Maji ya Magomvi.

25Mchukue Haroni pamoja na mwanawe Elazari, uwapeleke mlimani kwa Hori juu.

26Huko umvue Haroni mavazi yake, umvike mwanawe Elazari! Kisha Haroni atachukuliwa, afe huko.[#3 Mose 21:10.]

27Mose akafanya, kama Bwana alivyomwagiza, wakaupanda mlima wa Hori machoni pao wote walio wa mkutano.

28Kisha Mose akamvua Haroni mavazi yake, akamvika mwanawe Elazari; ndipo, Haroni alipokufa huko juu mlimani, kisha Mose na Elazari wakashuka mlimani.[#4 Mose 33:38; 5 Mose 10:6.]

29Wote wa mkutano walipoona, ya kuwa Haroni amekwisha kufa, wakamwombolezea Haroni siku thelathini wao wote wa mlango wa Isiraeli.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania