The chat will start when you send the first message.
1Wana wa Isiraeli walipoondoka huko wakapiga makambi kwenye mbuga za Moabu ng'ambo ya huku ya Yordani, Yeriko ukiwa ng'ambo ya pili.
2Balaka, mwana wa Sipori, alipoyaona yote, Waisiraeli waliyowafanyizia Waamori,
3Wamoabu wakaingiwa na woga mwingi sana wa hao watu kwa kuwa wengi sana, nao Wamoabu wakawastukia sana wana wa Isiraeli.
4Ndipo, Wamoabu walipowaambia wazee wa Wamidiani: Makundi hayo yatameza yote yanayotuzunguka, kama ng'ombe anavyomeza majani ya porini. Ndipo, Balaka, mwana wa Sipori, aliyekuwa mfalme wa Wamoabu siku zile
5alipotuma wajumbe kwenda Petori kwa Bileamu, mwana wa Beori, aliyekaa kwenye lile jito kubwa katika nchi yao walio ukoo wake, wamwite na kumwambia: Tazama, wako watu waliotoka Misri, nao wanaifunika nchi hii pote, unapotazama, tena wanakaa kunielekea mimi.[#Yos. 24:9; Mika 6:5.]
6Sasa njoo, uniapizie watu hawa! Kwani wako na nguvu za kunishinda mimi. Hivyo labda nitaweza kuwapiga na kuwafukuza katika nchi hii, kwani ninajua: Utakayembariki atakuwa amebarikiwa, naye utakayemwapiza atakuwa ameapizwa.
7Ndipo, wazee wa Wamoabu na wazee wa Wamidiani walipokwenda wakiushika mshahara wa uaguaji mikononi mwao; nao walipofika kwa Bileamu wakamwambia maneno ya Balaka.[#2 Petr. 2:15.]
8Akawaambia: Laleni huku usiku huu! Nami na niwarudishie neno, kama Bwana atakavyoniambia. Kwa hiyo wale wakuu wa Wamoabu wakakaa kwake Bileamu.
9Mungu akaja kwake Bileamu, akamwuliza: Watu hawa wanaokaa kwako ni watu gani?
10Bileamu akamwambia Mungu: Balaka, mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu
11kwamba: Tazama, wako watu waliotoka Misri, nao wanaifunika nchi pote, unapotazama; sasa njoo, uniapizie watu hawa! Labda hivyo nitaweza kupigana nao na kuwafukuza.
12Lakini Mungu akamwambia Bileamu: Usiende nao! Wala usiwaapize watu hao, kwani wamebarikiwa.
13Bileamu alipoamka asubuhi akawaambia wakuu wa Balaka: Nendeni zenu katika nchi yenu, kwani Bwana amekataa kunipa ruhusa kwenda nanyi.
14Ndipo, wakuu wa Wamoabu walipoondoka; walipofika kwa Balaka wakamwambia: Bileamu amekataa kwenda na sisi.
15Ndipo, Balaka alipotuma tena wakuu wengi wenye utukufu zaidi kuliko wale wa kwanza.
16Walipofika kwa Bileamu wakamwambia: Hivi ndivyo, anavyosema Balaka, mwana wa Sipori: Usikatae kuja kwangu!
17Kwani nitakuheshimu sanasana, nayo yote, utakayoniambia, nitayafanya; njoo tu, uniapizie hawa watu!
18Bileamu akajibu, akawaambia watumishi wa Balaka: Ijapo Balaka anipe nyumba yake ijaayo fedha na dhahabu, sitaweza kukipita kinywa cha Bwana Mungu wangu, nifanye jambo dogo au kubwa.[#1 Fal. 13:8.]
19Sasa nanyi kaeni hapa usiku huu, nijue, Bwana atakayoniambia tena!
20Mungu akaja kwake Bileamu na usiku, akamwambia: Kama hawa watu wamekuja kukuita, inuka, uende nao! Lakini sharti ulifanye neno, nitakalokuambia.
21Bileamu alipoondoka asubuhi akamtandika punda wake, akaenda nao wakuu wa Moabu.
22Makali ya Mungu ayakawaka moto, kwa kuwa amekwenda; kwa hiyo malaika wa Bwana akaja, akajisimamisha njiani, ampinge; naye alikuwa amempanda punda wake, nao vijana wake wawili walikuwa naye.
23Punda alipomwona malaika wa Bwana, akisimama njiani na kushika mkononi upanga uliochomolewa, punda akaondoka njiani na kuingia porini, naye Bileamu akampiga punda, amrudishe njiani.[#1 Mose 3:24; Yos. 5:13.]
24Kisha malaika wa Bwana akasimama tena njiani penye mizabibu palipokuwa pembamba, kwa kuwa pande zote mbili palikuwa na kuta za mawe.
25Punda alipomwona malaika wa Bwana akajisonga ukutani na kuuchubua mguu wa Bileamu; ndipo, alipompiga tena.
26Naye malaika wa Bwana akapita tena, akaenda kusimama mahali pafinyu sana pasipowezekana kupitia wala kuumeni wala kushotoni.
27Punda alipomwona malaika wa Bwana akalala chini, naye Bileamu alikuwa juu yake. Ndipo, makali ya Bileamu yalipomwakia, akampiga punda kwa fimbo.
28Ndipo, Bwana alipokifumbua kinywa cha punda, akamwambia Bileamu: Nimekukosea nini, ukinipiga sasa mara ya tatu?[#2 Petr. 2:16.]
29Bileamu akamwambia punda: Kumbe unanifyoza! Kama ningekuwa na upanga mkononi mwangu, ningekuua sasa hivi.
30Naye punda akamwambia Bileamu: Je? Mimi si punda wako, uliyempanda siku zote za maisha yako hata siku hii ya leo? Nimezoa kukufanyizia hivyo? Akasema: La!
31Ndipo, Bwana alipoyafumbua macho yake Bileamu, akamwona malaika wa Bwana, alivyosimama njiani na kushika mkononi upanga uliochomolewa; ndipo, alipomwinamia na kumwangukia kifudifudi.
32Naye malaika wa Bwana akamwambia: Kwa nini umempiga punda wako sasa mara ya tatu? Tazama, mimi nimetoka, nikupinge. Kwani safari hii ni ya kuangamiza machoni pangu.
33Punda aliponiona akaondoka njiani mbele yangu sasa mara ya tatu; kama asingaliondoka njiani mbele yangu, ningalikwisha kukuua wewe mwenyewe na kumponya yeye.
34Ndipo, Bileamu alipomwambia malaika wa Bwana: Nimekosa, kwani sikujua, ya kuwa wewe umesimama njiani, unipinge; sasa kama safari hii ni mbaya machoni pako, nitarudi.
35Naye malaika wa Bwana akamwambia Bileamu: Jiendee pamoja na watu hawa! Lakini sharti uliseme neno hilo tu, nitakalokuambia. Kisha Bileamu akaenda na wale wakuu wa Balaka.
36Balaka aliposikia, ya kama Bileamu anakuja, akatoka kumwendea njiani mpaka kwenye mji wa Moabu ulioko mahali penye mto wa Arnoni ulioko kwenye mapeo ya mpaka.
37Balaka akamwuliza Bileamu: Sikutuma kwako vizuri, nikuite? Mbona hukuja kwangu? Labda unaniwazia kuwa mtu asiyeweza kukupa macheo?
38Naye Bileamu akamwambia Balaka: Tazama, nimefika kwako! Lakini sasa je? nitaweza kusema lo lote? Neno hilo tu, Mungu atakalolitia kinywani mwangu, ndilo, nitakalolisema.
39Kisha Bileamu akaenda na Balaka, wakaingia Kiriati-Husoti (Mji wenye Mabarabara).
40Balaka akachinja ng'ombe na kondoo kuwa ng'ombe za tambiko, akamgawia hata Bileamu nyama, hata wakuu waliokuwa naye.
41Ilipokuwa asubuhi, Balaka akamchukua Bileamu, akampeleka juu vilimani kwa Baali; huko ndiko, alikowaona watu hao hata mwisho wa makambi yao.[#4 Mose 23:28.]