4 Mose 25

4 Mose 25

Ukosaji wa Waisiraeli unapatilizwa.

1Waisiraeli walipokaa Sitimu, watu wakaanza kufanya ugoni na wanawake wa Kimoabu.

2Nao walipowaalikia matambiko ya miungu yao, nao hao watu wakala nyama za tambiko, hata miungu yao wakaiangukia.[#4 Mose 31:16.]

3Lakini Waisiraeli walipojiunganisha hivyo na Baali-Peori, ndipo, makali ya Bwana yalipowawakia Waisiraeli.[#5 Mose 4:3.]

4Kwa hiyo Bwana akamwambia Mose: Wachukue wakuu wote wa watu hawa, uwanyonge juani mbele ya Bwana, haya makali ya Bwana yawakayo moto yapate kupoa na kuwaondokea Waisiraeli.[#5 Mose 21:22-23; 2 Sam. 21:6,9.]

5Naye Mose akawaambia waamuzi wa Waisiraeli: Waueni kila mtu watu wake waliojiunganisha na Baali-Peori!

6Papo hapo akaja mmoja wao wana wa Isiraeli, akapeleka kwa ndugu zake mwanamke wa Kimidiani machoni pake Mose napo machoni pao mkutano wote wa wana wa Isiraeli, hawa walipokuwa wakilia hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano.

7Pinehasi, mwana wa Elazari, mwana wa mtambikaji Haroni, alipoyaona akaondoka katikati ya mkutano, akachukua mkuki mkononi mwake,

8akamfuata yule mtu wa Kiisiraeli na kuingia chumbani, walimolala, akawachoma wote wawili tumboni, yule mtu wa Kiisiraeli na huyo mwanamke; ndipo, pigo lilipokomeshwa kwao wana wa Isiraeli.

9Nao waliouawa na hilo pigo walikuwa watu 24000.[#1 Kor. 10:8.]

10Kisha Bwana akamwambia Mose kwamba:

11Pinehasi, mwana wa Elazari, mwana wa mtambikaji Haroni, ameyarudisha nyuma machafuko yangu makali, yawaondokee wana wa Isiraeli; kwani wivu, niliokuwa nao, uo huo ameuona naye katikati yao, kwa hiyo sikuwamaliza wana wa Isiraeli kwa wivu wangu.

12Kwa sababu hii umwambie: Vivi hivi ninamwekea agano la kumpatia utengemano.[#1 Mambo 9:20.]

13Yeye nao wa uzao wake watakaokuwako nyuma yake watakuwa wenye agano la utambikaji wa kale na kale, kwa kuwa aliona wivu kwa ajili ya Mungu wake, akawapatia wana wa Isiraeli upozi.[#Sh. 106:30-31.]

14Jina lake yule Mwisiraeli aliyekufa kwa kuuawa pamoja na yule mwanamke wa Kimidiani alikuwa Zimuri, mwana wa Salu, naye alikuwa mkuu wa mlango wa baba yake kwao Wasimeoni.

15Nalo jina lake yule mwanamke wa Kimidiani aliyeuawa alikuwa Kozibi, binti Suri aliyekuwa mkuu wa ukoo wa milango ya baba yake kwao Wamidiani.[#4 Mose 31:8.]

16Kisha Bwana akamwambia Mose kwamba:

17Wainukieni Wamidiani, mwapige![#4 Mose 31:2-10.]

18Kwani ndio wanaowachukia ninyi kwa madanganyo yao walipowadanganya na matambiko ya Baali-Peori, tena wamewadanganya na kuwapa ndugu yao mke, yule Kozibi, binti mkuu wa Wamidiani, ni yule aliyeuawa siku hiyo, pigo lilipowapata kwa ajili ya Peori.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania