4 Mose 3

4 Mose 3

Wanawe Haroni.

1Hivi ndivyo vizazi vya Haroni na vya Mose vya siku zile, Bwana aliposema na Mose mlimani kwa Sinai.[#2 Mose 6:23.]

2Haya ndiyo majina ya wanawe Haroni: wa kwanza ni Nadabu, tena Abihu na Elazari na Itamari.

3Haya ndiyo majina ya wanawe Haroni waliopakwa mafuta kuwa watambikaji na kujazwa magao yao, wapate kufanya kazi ya utambikaji.

4Lakini Nadabu na Abihu walikufa mbele ya Bwana walipomtolea Bwana moto mgeni wa mavukizo nyikani kwa Sinai, nao hawakuwa na wana; kwa hiyo Elazari na Itamari walifanya kazi ya utambikaji na kuangaliwa na baba yao Haroni.[#3 Mose 10:1-2.]

Kazi za Walawi.

5Bwana akamwambia Mose kwamba:

6Wafikishe hawa wana wa shina la Lawi, uwasimamishe mbele ya mtambikaji Haroni, wamtumikie.[#2 Mose 32:29.]

7Tena na waziangalie hizo kazi zinazompasa yeye kuziangalia, nazo kazi zinazoupasa mkutano wote kuziangalia mbele ya hema la Mkutano na kuutumikia utumishi wa Kaoni.

8Na waviangalie vyombo vyote vya Hema la Mkutano na kuziangalia kazi zinazowapasa wana wa Isiraeli kuziangalia na kuutumikia utumishi wa kaoni.[#4 Mose 4.]

9Hawa Walawi umpe Haroni na wanawe, wawe vipaji vyao walivyopewa na wana wa Isiraeli.

10Nao akina Haroni na wanawe uwaweke kuuangalia utambikaji wao. Lakini mgeni atakayejitia humo hana budi kuuawa.[#4 Mose 1:51.]

11Bwana akasema na Mose kwamba:

12Tazama, mimi nimewachagua Walawi na kuwatoa katikati ya wana wa Isiraeli kuwa makombozi ya wana watakaozaliwa wa kwanza na mama zao kwa wana wa Isiraeli, kwa hiyo Walawi watakuwa wangu.[#4 Mose 8:16; 2 Mose 13:2.]

13Kwani wana wa kwanza wote ni wangu, kwani siku hiyo, nilipompiga kila mwana wa kwanza katika nchi ya Misri, nilijitakasia kila mwana wa kwanza kwa Waisiraeli, kama ni wa mtu au kama ni wa nyama wa kufuga, wawe wangu mimi Bwana.

Vizazi vya Walawi.

14Bwana akamwambia Mose nyikani kwa Sinai kwamba:

15Wakague wana wa Lawi milango ya baba zao mlango kwa mlango na udugu kwa udugu ukiwahesabu waume wote walio wenye mwezi mmoja na zaidi.

16Kisha Mose akawakagua kwa hiyo amri ya bwana, kama alivyoagizwa.

17Nao wana wa lawi walikuwa hawa kwa majina yao: Gersoni na Kehati na Merari.[#2 Mose 6:16-19; 4 Mose 26:57-64.]

18Nayo haya ndiyo majina ya wanawe Gersoni wenye udugu wao: Libuni na Simei.

19Nao wanawe Kehati wenye udugu wao ni Amuramu na Isihari, Heburoni na Uzieli.

20Nao wanawe Merari wenye udugu wao ni Mahali na Musi. Hawa ndio ndugu za Lawi za milango ya baba zao.

21Wa Gersoni walikuwa wao wa udugu wa Libuni nao wa udugu wa Simei; hawa ndio ndugu zao wa Gersoni.

22Walipohesabiwa waume wote wenye mwezi mmoja na zaidi jumla yao walikuwa watu 7500.

23Hawa ndugu zao wa Gersoni wakaambiwa, wapige makambi nyuma ya Kao upande wa baharini.

24Naye mkuu wao wa mlango wa baba yao Gersoni awe Eliasafu, mwana wa Laeli.

25Nazo kazi zao wana wa Gersoni za kuziangalia Hemani mwa Mkutano ziwe kuliangalia Kao lenyewe na Hema na chandalua chake na lile guo kubwa la pazia lililoko pa kuliingilia Hema la Mkutano,

26nazo nguo za uani na lile guo kubwa la pazia lililoko pa kuuingilia ua, unaolizunguka Kao na meza ya kutambikia, tena kamba zake nayo yote yanyoupasa utumishi huu.

27Wa Kehati walikuwa wao wa udugu wa Amuramu nao wa udugu wa Isihari nao wa udugu wa Heburoni nao wa udugu wa Uzieli. Hawa ndio ndugu zao wa Kehati.

28Walipohesabiwa waume wote wenye mwezi mmoja na zaidi jumla yao walikuwa watu 8600 wa kuziangalia kazi za kupaangalia Patakatifu.

29Hawa ndugu zao wa Kehati wakaambiwa, wapige makambi upande wa kusini wa Kao.

30Naye mkuu wao wa mlango wa baba yao Kehati awe Elisafani, mwana wa Uzieli.[#3 Mose 10:4.]

31Nazo kazi zake ziwe kuliangalia Sanduku na meza ya mikate na kinara na meza ya kuvukizia nayo ya kuteketezea ng'ombe za tambiko, navyo vyombo vya Patakatifu, watakavyovitumia, na pazia la Hemani, tena wafanye kazi zote za utumishi uwapasao.

32Naye mkuu wa wakuu wa Walawi alikuwa Elazari, mwana wa mtambikaji Haroni, awakague wote wanaoangalia kazi za Patakatifu.

33Wa Merari walikuwa wao wa udugu wa Mahali nao wa udugu wa Musi. Hawa ndio ndugu zao wa Merari.

34Walipohesabiwa waume wote wenye mwezi mmoja na zaidi jumla yao walikuwa watu 6200.

35Nao wakaambiwa, mkuu wao wa mlango wa baba yao Merari awe Surieli, mwana wa Abihaili, nao wapige makambi upande wa kaskazini wa Kao.

36Nazo kazi zao wana wa Merari za kuangalia walizopewa ziwe hizo za mbao za Kao na misunguo yao na nguzo zao na miguu yao na vyombo vyao vyote, wafanye kazi zote za utumishi ziwapasazo,

37tena kazi za kuziangalia nguzo zilizouzunguka ua na miguu yao na mambo zao na kamba zao.

38Nao waliopiga makambi mbele ya Kao upande wa mashariki, ndio mbele ya Hema la Mkutano upande wa maawioni kwa jua walikuwa Mose na Haroni na wanawe waliongoja zamu za kupaangalia Patakatifu mahali pao wana wa Isiraeli. Lakini mgeni aliyejitia katika kazi hizi hakuwa na budi kuuawa.[#4 Mose 3:10.]

39Jumla yao Walawi wote, Mose na Haroni waliowakagua kwa amri ya Bwana, waume wote wenye mwezi mmoja na zaidi wa udugu wao walikuwa watu 22000.

Ukombozi wa wana wa kwanza.

40Bwana akamwambia Mose: Wakague waume wote wa wana wa Isiraeli wenye mwezi mmoja na zaidi walio wana wa kwanza, ufanye hesabu ya majina yao.

41Uwachukue Walawi kuwa wangu mimi Bwana, wakiwakomboa wana wote wa kwanza kwa wana wa Isiraeli, nao nyama wa kufuga wa Walawi na wawakomboe wana wa kwanza wa nyama wa kufuga wa wana wa Isiraeli.

42Ndipo, Mose alipowakagua wana wote wa kwanza wa Waisiraeli, kama Bwana alivyomwagiza.

43Nao waume wote waliokuwa wana wa kwanza wenye mwezi mmoja na zaidi walipohesabiwa majina, jumla yao walikuwa watu 22273.

44Bwana akamwambia Mose kwamba:

45Wachukue Walawi kuwa makombozi ya wana wote wa kwanza kwa wana wa Isiraeli, nao nyama wa kufuga wa Walawi kuwa makombozi ya nyama wao, Walawi wawe wangu mimi Bwana.[#4 Mose 3:12.]

46Nayo makombozi yao wale 273 waliozidi kwa wana wa kwanza wa wana wa Isiraeli kuwa wengi kuliko Walawi,[#4 Mose 3:39,43.]

47uwatoze kila mmoja fedha (sekeli) tano tano kichwa kwa kichwa, nazo hizi fedha, utakazowatoza, ziwe fedha zinazotumika Patakatifu, kila fedha moja iwe ya gera ishirini, ndio thumuni nane.

48Hizi fedha mpe Haroni na wanawe kwa kuwa makombozi yao wale waliozidi kuwa wengi.

49Ndipo, Mose alipowatoza fedha za makombozi wale waliozidi kuwa wengi kuliko wale waliokombolewa na Walawi.

50Nazo hizi fedha, alizozitoza za kuwakomboa wana wa kwanza wa wana wa Isiraeli, zikawa 1365, zikipimwa kwa fedha za Patakatifu.

51Kisha Mose akampa Haroni na wanawe hizo fedha kwa ile amri ya Bwana, kama Bwana alivyomwagiza Mose.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania