4 Mose 32

4 Mose 32

Kuzigawanya nchi za ng'ambo ya Yordani ya maawioni kwa jua.

(Taz. 5 Mose 3:12-22.)

1Wana wa Rubeni na wana wa Gadi walikuwa na nyama wa kufuga wengi sanasana; walipoitazama nchi ya Yazeri na nchi ya Gileadi wakaziona kuwa zenye mahali pengipengi panapofaa pa kufugia nyama.

2Kwa hiyo wana wa Gadi na wana wa Rubeni wakamjia Mose na mtambikaji Elazari na wakuu wa mkutano, wakawaambia:

3Ataroti na Diboni na Yazeri na Nimura na Hesiboni na Elale na Sibamu na Nebo na Beoni,

4hizi nchi, Bwana alizozipiga mbele ya mkutano wa Isiraeli, ni nchi zifaazo kwa kufuga nyama, nasi watumishi wako tunao nyama wa kufuga.

5Wakasema: Kama tumeona upendeleo machoni pako, sisi watumishi wako, na tupewe nchi hizi, tuzichukue, usituvukishe mto wa Yordani!

6Ndipo, Mose alipowaambia wana wa Gadi na wana wa Rubeni: Mbona mnataka, ndugu zenu waende vitani, ninyi mkikaa hapo?

7Mbona mnataka kuikataza mioyo ya wana wa Isiraeli, wasivuke na kuiingia nchi, Bwana aliyowaapia?

8Hivi ndivyo, baba zenu walivyofanya, nilipowatuma toka Kadesi-Barnea kwenda kuitazama nchi hii.[#4 Mose 13.]

9Walipokwisha kupanda na kufika kwenye kijito cha Eskoli na kuiona nchi hii, wakaikataza mioyo yao wana wa Isiraeli, wasiingie katika nchi hiyo, Bwana aliyowapa.

10Siku hiyo makali ya Bwana yakawaka, akaapa kwamba:

11Watu hawa waliotoka Misri kufika huku walio wenye miaka ishirini na zaidi hawataiona kabisa nchi hiyo, niliyowaapia Aburahamu na Isaka na Yakobo, kwa kuwa hawakunifuata kwa mioyo yote.[#4 Mose 14:22-38; 26:65.]

12Ila Kalebu, mwana wa Mkenizi Yefune, na Yosua, mwana wa Nuni, hawa tu wataiingia, kwa kuwa wamemfuata Bwana kwa mioyo yote.

13Kwa kuwa makali ya Bwana yaliwawakia wana wa Isiraeli, akawatembeza nyikani miaka 40, mpaka kimalizike kile kizazi chao chote walioyafanya hayo yaliyokuwa mabaya machoni pake Bwana.

14Sasa ninawaona ninyi, ya kama mmeinuka mahali pa baba zenu na kujitokeza kuwa wana wao wale wakosaji, mwuongeze moto wa makali ya Bwana, uzidi kuwawakia wana wa Isiraeli.

15Mkirudi nyuma na kumwacha, naye atawaacha tena siku nyingi nyikani; ndivyo, mtakavyowaangamiza hawa watu wote pia.

16Ndipo, walipomkaribia, wakamwambia: Tunataka tu kujenga huku mazizi ya nyama wetu wa kufuga na miji ya watoto wetu.

17Kisha sisi wenyewe tutajitengeneza upesi kuwatangulia wana wa Isiraeli, mpaka tuwaingize mahali pao, watoto wetu wakikaa katika miji yenye maboma kwa ajili ya wenyeji wa nchi hii.

18Hatutarudi nyumbani kwetu, mpaka wana wa Isiraeli watakapokwisha kupata kila mtu fungu lake mwenyewe.

19Kwani sisi hatutapata mafungu pamoja nao ng'ambo ya huko ya Yordani pande hizo za huko, kwani mafungu yetu sisi yametuangukia ng'ambo ya huku ya Yordani upande wa maawioni kwa jua.

20Ndipo, Mose alipowaambia: Mkilifanya neno hili na kujitengeneza kwenda vitani mbele ya Bwana,[#Yos. 1:13-15.]

21nanyi nyote mkiuvuka Yordani mbele ya Bwana na kushika mata ya vita, mpaka awafukuze adui zake mbele yake,

22nayo nchi hiyo itiishwe mbele ya Bwana, basi, baadaye mtarudi mkiwa watu wasiomkosea Bwana, wasiowakosea nao Waisiraeli; ndipo, nchi hii itakapokuwa yenu, mwichukue mbele ya Bwana, iwe yenu kabisa.

23Lakini msipovifanya hivyo, mtajiona kuwa watu waliomkosea Bwana, tena mtajua, ya kuwa makosa yenu yatawapata!

24Basi, wajengeeni watoto wenu miji nayo makundi yenu mazizi, kisha yafanyeni mliyoyasema kwa vinywa vyenu!

25Ndipo, wana wa Gadi na wana wa Rubeni walipomwambia Mose kwamba: Watumishi wako watafanya, kama bwana wetu anavyoagiza.

26Watoto wetu na wake zetu na mbuzi na kondoo wetu na nyama wetu wengine wa kufuga watakaa huku katika miji ya Gileadi,

27lakini watumishi wako wote wanaoweza kushika mata na kwenda vitani watavuka machoni pa Bwana kwenda kupigana, kama bwana wetu alivyosema.

28Kisha Mose akamwagiza mtambikaji Elazari na Yosua, mwana wa Nuni, na wakuu wa milango ya mashina ya wana wa Isiraeli,

29yeye Mose akiwaambia: Wana wa Gadi na wana wa Rubeni, ni kwamba: wote wa kwao wanaoweza kushika mata ya vita wakiuvuka Yordani pamoja nanyi machoni pa Bwana, basi, nchi itakapokuwa imetiishwa mbele yenu, sharti mwape nchi hii ya Gileadi, waichukue, iwe yao.[#Yos. 4:12.]

30Lakini wa kwao wanaoweza kushika mata wasipovuka pamoja nanyi, basi, na wapate mafungu yao katikati yenu katika nchi ya Kanaani.

31Nao wana wa Gadi na wana wa Rubeni wakaitikia kwamba: Kama Bwana alivyowaambia watumishi wako, ndivyo, tutakavyofanya.

32Sisi tunaoweza kushika mata tutavuka machoni pa Bwana kuingia katika nchi ya Kanaani, lakini mafungu yetu sisi, tutakayoyachukua, yawe yetu wenyewe, yatakuwa ng'ambo ya huku ya Yordani.

33Ndipo, Mose alipowapa wana wa Gadi na wana wa Rubeni nao wa nusu ya shina la Manase, mwana wa Yosefu, ufalme wa Sihoni, mfalme wa Waamori, na ufalme wa Ogi, mfalme wa Basani; nchi hii yote pamoja na miji yake yote pia iliyokuwamo katika mipaka yake iliyoizunguka nchi hiyo.[#Yos. 13:8-31.]

34Ndipo, wana wa Gadi walipoijenga miji ya Diboni na Ataroti na Aroeri,

35na Ataroti-Sofani na Yazeri na Yogibeha

36na Beti-Nimura na Beti-Harani; nayo ilikuwa miji yenye maboma na mazizi ya makundi.

37Nao wana wa Rubeni wakaijenga miji ya Hesiboni na Elale na Kiriataimu

38na Nebo na Baali-Meoni, wakiligeuza jina lake, na Sibuma; ndiyo majina, waliyoiita hiyo miji, waliyoijenga.

39Nao wana wa Makiri, mwana wa Manase, wakaenda Gileadi, wakauteka wakiwafukuza Waamori waliokaa humo.

40Kisha Mose akampa Makiri, mwana wa Manase, mji wa Gileadi, akakaa humo.

41Naye Yairi, mwana wa Manase, akaenda, akaviteka vijiji vyao vya mahema, akaviita vijiji vya Mahema ya Yairi.[#5 Mose 3:14.]

42Naye Noba akaenda, akauteka Kenati na mitaa yake, akauita kwa jina lake Noba.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania