4 Mose 36

4 Mose 36

Yapasayo wanawake wenye mafungu ya nchi.

1Wakuu wa milango ya ndugu za wana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, wa ndugu zao wana wa Yosefu, wakamkaribia Mose, wakasema mbele yake na mbele yao wakuu waliokuwa baba za milango ya wana wa Isiraeli,

2wakawaambia: Bwana amekuagiza wewe, bwana wetu, kuwapa wana wa Isiraeli nchi hiyo na kuwapigia kura, wapate mafungu ya nchi kuwa yao; nawe bwana wetu, umeagizwa na Bwana kuwapa wana wa kike wa ndugu yetu Selofuhadi fungu lake.[#4 Mose 26:55; 27:6-7.]

3Itakapotukia, mmoja miongoni mwa wana wa mashina mengine ya wana wa Isiraeli awaoe, ndipo, fungu lao litakapotoweka katika mafungu ya baba zetu, litiwe katika mafungu ya shina jingine litakalokuwa lao, wakiisha kuolewa; hivyo ndivyo, mafungu, tuliyoyapata kwa kupigiwa kura kuwa yetu, yatakavyopunguzwa.

4Nao mwaka wa shangwe utakapotimia kwa wana wa Isiraeli, fungu lao litatiwa vivyo hivyo katika mafungu ya shina jingine litakalokuwa lao kwa kuolewa kwao; ndivyo, hilo fungu lao litakavyotoweka katika mafungu ya shina la baba zetu.[#3 Mose 25:10-13.]

5Ndipo, Mose alipowaagiza wana wa Isiraeli kwa kuagizwa na Bwana kwamba: Hayo, wao wa shina la wana wa Yosefu waliyoyasema, ni ya kweli.

6Hili ndilo neno, Bwana analowaagiza wana wa kike wa Selofuhadi kwamba: Mtu, watakayemwona kuwa mwema, wataolewa naye, lakini watakayeolewa naye sharti awe mtu wa ndugu za shina la baba yao.

7Ni kwa kwamba mafungu yao wana wa Isiraeli yasiondolewe katika shina moja na kutiwa katika shina jingine, ila wana wa Isiraeli sharti wagandamane kila mmoja na mafungu yaliyo ya shina la baba zao.

8Wana wa kike wote walio wenye fungu la nchi ya mashina ya wana wa Isiraeli sharti waolewe na mtu aliye wa ndugu za shina la baba yao, kusudi wana wa Isiraeli washike kila mmoja fungu lake la nchi, alilolipata kwa baba zake, liwe lake,

9kusudi mafungu ya nchi yasiondolewe katika shina moja na kutiwa katika shina jingine, ila mashina ya wana wa Isiraeli sharti wagandamane, kila mmoja akae katika fungu lake.

10Kama Bwana alivyomwagiza Mose, ndivyo, wana wa kike wa Selofuhadi walivyofanya.

11Hao Mala, Tirsa na Hogla na Milka na Noa, wale wana wa kike wa Selofuhadi, wakaolewa na wana wa ndugu za baba yao.[#4 Mose 26:33.]

12Wao waliookuwa ndugu zao wana wa Manase, mwana wa Yosefu, ndio waliolewa nao; kwa hiyo fungu lao likakaa kwake shina la ndugu za baba yao.

13Haya ndiyo maagizo na maamuzi, Bwana aliyowaagiza wana wa Isiraeli kinywani mwa Mose kwenye mbuga za Moabu ng'ambo ya huku ya Yordani, Yeriko ukiwa ng'ambo ya pili.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania