The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose kwamba:[#1 Sam. 1:11.]
2Sema na wana wa Isiraeli na kuwaambia: Mtu mume au mke akitaka kujitenga na kuapa apo la mtu aliyejieua, mtu akitaka kujieua hivyo kuwa wake Bwana,
3na ajieue kuwa mwenye mwiko wa mvinyo na wa vileo vyo vyote, asinywe wala siki ya mvinyo wala siki ya kileo cho chote, tena asinywe maji ya zabibu, asile zabibu wala mbichi wala kavu.[#Luk. 1:15.]
4Siku zote za weuo wake asile cho chote kitokacho kwa mzabibu, wala koko wala maganda.
5Siku zote za maapo ya weuo wake wembe usije kichwani pake; mpaka siku zitimie, alizojieua kuwa wake Bwana, sharti awe mtakatifu na kuziacha nywele za kichwani pake, zikue.[#Amu. 13:5.]
6Siku zote za kujieua kwake kuwa wake Bwana, asiingie mlimo na mfu.
7Asijipatie uchafu kwa baba yake, wala kwa mama yake, wala kwa kaka yake, wala kwa mdogo wake, wala kwa umbu lake, wakifa, kwani weuo wa Mungu wake uko kichwani pake.[#3 Mose 21:11.]
8Siku zote za weuo wake ni mtakatifu wa Bwana.
9Ikiwa, inatukia, asipoviwazia, mara mtu afe hapo alipo, atakuwa amekwisha kukipatia uchafu kichwa chake kilicho na weuo wa Bwana; kwa hiyo sharti azinyoe nywele za kichwani pake siku hiyo, atakapokuwa ametakata, ndio siku ya saba, ndipo azinyoe.
10Siku ya nane na apeleke huwa wawili au makinda mawili ya njiwa manga kwa mtambikaji hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano.[#3 Mose 5:7.]
11Mtambikaji na amtumie mmoja kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, wa pili kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, ampatie upozi, kwa kuwa kosa lilimpata hapo penye yule mfu; siku hiyo sharti aseme tena, ya kama kichwa chake ni kitakatifu.
12Kisha ajieue tena kuwa wake Bwana siku zilezile wa weuo wake na kutoa mwana kondoo wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi; lakini siku zile za kwanza zisihesabiwe, kwa kuwa ule weuo wake ulichafuliwa.
13Nayo haya ndiyo maongozi yake aliyejieua: siku za weuo wake zitakapotimia, ndipo wampeleke hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano.
14Hapo na amtolee Bwana toleo lake: mwana kondoo wa mwaka mmoja asiye na kilema kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima na mwana kondoo jike wa mwaka mmoja asiye na kilema kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo na dume la kondoo kuwa ng'ombe ya tambiko ya shukrani,
15tena kikapu cha mikate isiyochachwa iliyotengenezwa kwa unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta, na maandazi membamba yasiyochachwa yaliyopakwa mafuta pamoja na kutoa vilaji na vinywaji vyao vya tambiko.
16Naye mtambikaji na avipeleke vyote kwa Bwana na kumtolea kwanza ng'ombe yake ya tambiko ya weuo nayo ya kuteketezwa nzima.
17Kisha na amchinje yule dume la kondoo kuwa ng'ombe ya tambiko ya kumshukuru Bwana pamoja na kile kipaji cha mikate isiyochachwa, kisha mtambikaji na avitoe navyo vilaji na vinywaji vyake vya tambiko.
18Kisha huyu aliyejieua na azinyoe nywele za kichwani pake zilizokuwa na mwiko wa kunyolewa, naye azinyoe hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, kisha na azichukue hizo nywele za kichwani pake zilizokuwa na mwiko wa kunyolea, azitie katika moto unaowaka chini ya ng'ombe ya tambiko ya shukrani.[#Tume. 18:18.]
19Kisha mtambikaji na achukue mkono wa dume la kondoo uliopikwa, tena mkate mmoja usiochachwa uliomo kikapuni na andazi jembamba moja lisilochachwa, ayaweke mikononi mwake huyo aliyejieua, atakapokwisha kuzinyoa nywele zake za mwiko.
20Kisha mtambikaji na avipitishe motoni mbele ya Bwana, kwa kuwa vitakatifu ni vyake mtambikaji pamoja na kidari cha kupitishwa motoni na paja la kunyanyuliwa. Kisha huyo aliyejieua atakuwa tena na ruhusa ya kunywa mvinyo.[#3 Mose 7:29-34.]
21Haya ndiyo maongozi ya mtu atakayejieua na kuapa; haya ndiyo matoleo yake, atakayomtolea Bwana kwa ajili ya weuo wake. Kama yako mengine, mkono wake uwezayo kuyafikisha, ayatoe, basi, na ayatoe; lakini hayo, aliyoyaapa, sharti ayamalize vivyo hivyo, kama alivyoapa, na kuyafuata haya maongozi ya weuo wake.
22Bwana akamwambia Mose kwamba:[#3 Mose 9:22-23.]
23Mwambie Haroni na wanawe kwamba: Mkiwabariki wana wa Isiraeli sharti mwaambie hivyo:
24Bwana akubariki, akulinde![#Sh. 121.]
25Bwana akuangazie uso wake, akuhurumie![#Sh. 80:4.]
26Bwana akuinulie uso wake, akupe utengemano![#Sh. 69:17-18.]
27Watakapowatajia wana wa Isiraeli Jina langu hivi, mimi nitawabriki.