Wafilipi 4

Wafilipi 4

Upatanisho.

1Kwa hiyo, ndugu zangu wapendwa, ninaowatunukia, m furaha yangu na kilemba changu; wapenzi, simameni vivyo hivyo kwake Bwana![#2 Kor. 1:14; 1 Tes. 2:19-20.]

2Namwonya Ewodia, naye Sintike namwonya, wapatane kwa kuwa wake Bwana.

3Nawe, mwenzangu wa kweli, nakuomba, uwasaidie wanawake hao, maana waliupigania Utume mwema pamoja nami na pamoja na Klemensi nao wenzangu wengine wa kazi walioandikiwa majina yao katika kitabu cha uzima.[#Sh. 69:29; Luk. 10:20.]

Furaha ya Kikristo.

4*Furahini siku zote kwa kuwa wake Bwana! Nasema tena: Furahini![#Fil. 2:17-18; 3:1; 2 Kor. 13:11.]

5Utu wenu ujulikane kwao watu wote! Bwana yuko karibu.

6Msisumbukie kitu! Ila mambo yo yote, myatakayo, mmjulishe Mungu mkimwomba na kumbembeleza pamoja na kumshukuru![#Sh. 145:18; Mat. 6:25-34; 1 Petr. 5:7.]

7Nao utengemano wa Mungu uyapitao yote, tuyatambuayo, uilinde mioyo yenu na mawazo yenu, mkae mwake Kristo Yesu!*[#Yoh. 14:27; Kol. 3:15.]

8Kisha ndugu, yawazeni yote yaliyo yenye kweli nayo yaliyo yenye macheo nayo yaongokayo nayo yang'aayo nayo yapendezayo nayo yaliyo mazuri kusemwa nayo yafaayo kufanywa nayo yo yote yapasayo kusifiwa![#Rom. 12:17.]

9Ndiyo, mliyofundishwa, mkayapokea, mkayasikia, mkayaona kwangu mimi; sasa yafanyizeni! Ndipo, Mungu mwenye utengemano atakapokuwa pamoja nanyi.[#1 Tes. 5:23.]

Shukrani.

10Hivyo, nilivyo mwake Bwana, nalifurahi sana, ya kuwa siku hizi mmekwisha pata tena kunitunza mimi. Tangu kale mlikuwa mkiyawaza, lakini siku za kati hamkuweza.

11Sisemi hivyo kwamba: Nimekosa kitu. Kwani mimi nimejifunza kutoshewa na hayo, niliyo nayo.[#1 Tim. 6:6.]

12Najua kupungukiwa, najua kufurikiwa. Po pote mambo yo yote si mgeni nayo, kama ni kushiba au kuona njaa, kama ni kufurikiwa au kukosa.[#2 Kor. 6:10.]

13Nayaweza yote kwa nguvu yake yeye anayenitia nguvu.[#2 Kor. 12:10.]

14Lakini mmefanya vizuri mlipojitoa, mwe wenzangu wa maumivu.

15Nanyi Wafilipi mwajua: tangu hapo, nilipoanza kuutangaza Utume mwema, nilipotoka Makedonia, hakuna wateule wengine walionigawia wakiyatoa yaleyale, waliyopewa, msipokuwa ninyi peke yenu.[#2 Kor. 11:9.]

16Hata nilipokuwa Tesalonike, mmetuma mara ya kwanza na mara ya pili, mkanipa vya kunitunza.

17Sivisemi hivyo kwa maana, nayatafuta matunzo, ila nayatafuta matunda kwamba: Mapato yenu yaongezeke.[#1 Kor. 9:11.]

18Kwani nilikuwa nayo yote yanipasayo, nayo yalikuwa mengi. Kisha nikafurikiwa nilipopewa na Epafurodito vitu vile vilivyotoka kwenu; ni manukato yanukayo vizuri kama ng'ombe ya tambiko ifaayo ya kumpendeza Mungu.[#Fil. 2:25.]

19Mungu wangu awape ninyi, yote mkosayo yawafurikie! Maana yeye ni mwenye mali nyingi zilizomo katika utukufu uliotokea katika Kristo Yesu.

20Yeye Mungu aliye Baba yetu atukuzwe kale na kale pasipo mwisho! Amin.

21Nisalimieni kila mtakatifu aliye wake Kristo Yesu! Ndugu walio pamoja nami wanawasalimu.

22Watakatifu wote wanawasalimu, kupita wengine ni wale waliomo nyumbani mwake Kaisari.

23Upole wa Bwana wetu Yesu Kristo uzikalie roho zenu! Amin.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania