Mifano 11

Mifano 11

Mema yao wamchao Mungu nayo mabaya yao wasiomcha.

1Mizani ya kudanganyia humtapisha Bwana,

lakini mawe ya sawasawa ya kupimia humpendeza.

2Majivuno yanapofika, ndipo, matusi yanapofika nayo,

lakini werevu wa kweli huwakalia wanyenyekevu.

3Utawa wao wanyokao mioyo huwaongoza,

lakini waliomwacha Mungu upotovu wao huwaangamiza.

4Mali hazifai kitu siku, makali yanapotokea,

lakini wongofu huponya hata kufani.

5Wongofu wao wamchao Mungu huzinyosha njia zao,

lakini asiyemcha Mungu ataangushwa na uovu wake.

6Wongofu wao wanyokao mioyo utawaponya,

lakini waliomwacha Mungu watanaswa na tamaa zao.

7Mtu asiyemcha Mungu anapokufa, kingojeo chake hupotea,

nayo matumaini yao wapotovu hupotea.

8Mwongofu hutolewa katika masongano,

lakini asiyemcha Mungu hutiwa mahali pake.

9Mpotovu humwangamiza mwenziwe kwa kinywa chake,

lakini waongofu huokolewa kwa ujuzi wao.

10Waongofu wakipata mema, mji huwashangilia,

lakini wasiomcha Mungu wakiangamia, watu huwazomea.

11Kwa mbaraka yao wanyokao mji hutukuka,

lakini kwa ajili ya vinywa vyao wasiomcha Mungu hubomolewa.

12Ambezaye mwenziwe amepotelewa na akili,

lakini mtu mwenye utambuzi hunyamaza.

13Atembeaye na kusingizia hufunua mashauri ya njama,

lakini mwenye moyo mwelekevu huficha mambo kama hayo.

14Pasipo wongozi mwema ukoo mzima wa watu huanguka;

huokoka, wenye mashauri mema wakiwa wengi.

15Aliyejitoa kuwa dhamana ya mgeni atapatwa na mabaya zaidi,

lakini akataaye kumpa mwingine mkono hukaa na kutulia.

16Mwanamke apendezaye kujipatia heshima,

lakini wakorofi hujipatia mali nyingi.

17Mtu mwenye huruma hujifanyizia mema mwenyewe,

lakini asiye na huruma hujiumiza mwili wake.

18Asiyemcha Mungu hujipatia mali za udanganyifu,

lakini apandaye yenye wongofu hujipatia mshahara wa kweli.

19Wongofu unapeleka uzimani kweli,

lakini ayakimbiliaye mabaya huenda kufani.

20Wenye mioyo mapotovu humtapisha Bwana,

lakini washikao njia zisizo za ukosaji humpendeza.

21Ingawa wapeane mikono, mbaya hana budi kupatilizwa,

lakini wazao wao waongofu watapona.

22Mwanamke mzuri asiye na akili

ni pete ya dhahabu puani mwa nguruwe.

23Tamaa za waongofu hutamani mema tu,

lakini wasiomcha Mungu wanayoyangojea, huwapatia makali.

24Mwingine hujipatia mali zaidi kwa kugawia wengine,

lakini mwingine huzidi kukosa mali, ijapo aziweke kupita kiasi.

25Apendaye kugawia hushibishwa mwenyewe,

anyweshaye wengine naye hunyweshwa.

26Anyimaye wenzake ngano watu humwapiza,

lakini mbaraka hukifia kichwa chake aziuzaye.

27Atafutaye mema toka asubuhi hupendeza,

lakini atafuataye mabaya, yayo hayo humrudia mwenyewe.

28Azitumainiye mali zake huangushwa nazo,

lakini waongofu huchapuka kama majani.

29Awavurugaye wa nyumbani mwake hujipatia upepo, uwe fungu lake,

mpumbavu sharti amtumikie mwenye moyo mwerevu wa kweli.

30Mazao ya mwongofu ni mti wa uzima,

mwerevu wa kweli huzishinda roho za watu.

31Tazameni! Mwongofu hupata mshahara wake katika nchi hii,

Tena itakuwaje? Asiyemcha Mungu na mkosaji asilipishwe zaidi?

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania