Mashangilio 106

Mashangilio 106

Upole wake Mungu na ugumu wao Waisiraeli.

(1,47-48: 1 Mambo 16:34-36.)

1Haleluya! Mshukuruni Bwana, ya kuwa ni mwema! Ya kuwa upole wake ni wa kale na kale![#Sh. 107:1; 118:1; 136:1.]

2Yuko nani atakayemaliza kuyasimulia matendo ya nguvu ya Bwana? Yuko nani tena atakayeyatanganza matukuzo yake yote?

3Wenye shangwe ndio wayashikao yanyokayo nao wafanyao siku zote yaliyo yenye wongofu.

4Bwana, nikumbuke kwa kupendezwa nao walio ukoo wako! Unijie kunikagua, upate kuniokoa,

5nami nipate kuyatazama mema yao wateule wako, tena niifurahie furaha yao walio kabila lako, tushangilie pamoja nao walio fungu lako!

6Pamoja na baba zetu tulikosa nasi, tulipoacha kumcha Mungu tulikora manza.[#Dan. 9:5.]

7Baba zetu walipokuwako kule Misri, walipoyaona mataajabu yako hawakuerevuka, hawakuyakumbuka yale mema mengi, uliyawagawia, wakakataa kukutii kule baharini, kwenye Bahari Nyekundu.[#2 Mose 14:11-12.]

8Lakini kwa ajili ya Jina lake aliwaokoa, awajulishe uweze wake wenye nguvu.

9Akaikaripia Bahari Nyekundu; ndipo, ilipokupwa, akawapitisha kule vilindini, kama ni nyikani.

10Akawaokoa mikononi mwao waliowachukia, akawakomboa mikononi mwao waliokuwa adui zao.

11Maji yakawafunika wao waliowasonga, kwao hakusalia hata mmoja.

12Ndipo, walipoyategemea maneno yake, wakamwimbia mashangilio ya kumsifu.[#2 Mose 15.]

13Lakini upesi sana wakayasahau matendo yake, aliyoyataka kuwaeleza hawakuyangojea.

14Walipoingiwa na tamaa kule nyikani wakazifuata, wakamjaribu Mungu huko jangwani.[#4 Mose 11:4-6.]

15Akawapa waliyomwomba, akayafurikisha, mpaka yakizichafua roho zao.

16Kisha wakamwonea Mose wivu hapo, walipopanga, hata Haroni aliyekuwa mtakatifu wake Bwana.[#4 Mose 16.]

17Nchi ikaasama, ikammeza Datani, ikawafunika nao akina Abiramu.

18Moto ukawaka kwenye mkutano wao, ndimi zake zikawateketeza wasiomcha Mungu.

19Wakafanya ndama kule Horebu, wakakitambikia hicho kinyago.[#2 Mose 32.]

20Hivyo ndivyo, walivyougeuza utukufu wao kuwa kama wa ng'ombe mwenye kula majani.[#Rom. 1:23.]

21Wakamsahau Mungu aliyewaokoa na kufanya mambo makuu kule Misri.[#5 Mose 32:18.]

22Nayo yaliwastaajabisha walioko katika nchi ya Hamu, nako kwenye Bahari Nyekundu yakawastusha.

23Akawaza kuwamaliza, waishe kabisa, kama Mose, aliyemchagua, asingalijisimamisha mbele yake kwenye ule ufa ulioatuka, ayatulize machafuko yake, asiwaangamize.[#2 Mose 32:11; 5 Mose 9:25-26; Ez. 13:5.]

24Wakaibeza ile nchi iliyo nzuri zaidi. hawakulitegemea Neno lake.[#4 Mose 14:2-4; 5 Mose 8:7-10.]

25Katika mahema yao wakanung'unika, hawakuisikiliza sauti yake yeye Bwana.

26Akauinua mkono wake, awapige, awaue nyikani,

27awatapanye walio wa uzao wao kwenye wamizimu na kuwamwaga katika nchi zilizokuwa za wengine.

28Kisha wakaja kugandamana na Baali Peori, wakala nyama za tambiko la mizimu;[#4 Mose 25:3.]

29Ndivyo, walivyomkasirisha na matendo yao. Kisha kilipotukia kwao kipindupindu,

30ndipo, Pinehasi alipotokea, akawaonya, nacho kipindupindu kikazuiliwa papo hapo.

31Kwa hivyo aliwaziwa kuwa mwenye wongofu kwa vizazi na vizazi kale na kale.[#1 Mose 15:6; 4 Mose 25:12.]

32Kisha wakamchafua moyo tena kwenye maji ya Meriba, Mose naye akapatwa na mabaya kwa ajili yao.[#4 Mose 20:2-13.]

33Kwani walipoibishia roho yake, midomo yake ilisema maneno yasiyompasa.

34Kisha hawakuyamaliza makabila ya watu. Bwana aliyowaagiza kuwaua.[#5 Mose 7:1-2; 12:2-3; Amu. 1:28.]

35Ila walichanganyika nao wamizimu, nayo matendo yao wakayaiga.

36Navyo vinyago vyao wakavitumikia, navyo ndivyo vilivyowanasa.

37Wana wao wa kiume nao wa kike wakawatoa kuwa ng'ombe za tambiko za mizimu.[#3 Mose 18:21.]

38Nazo damu zisizokuwa zenye manza wakazimwaga, ni damu za wana wao wa kiume na wa kike, waliowatoa kuwa ng'ombe za tambiko za vinyago vya Kanaani; ndivyo, walivyoichafua nchi kwa kumwaga damu.

39Hata wenyewe walijichafua kwa hayo matendo yao, kwa kuzifanya hizo kazi zao wakawa wagoni.

40Ndivyo, walio ukoo wake walivyokoleza moto wa makali yake Bwana, wao waliokuwa fungu lake wakamtapisha,

41akawatia mikononi mwao wamizimu, walio wachukivu wao wakawatawala.[#Amu. 2:14.]

42Adui zao wakawatesa, wakashurutishwa kuiinamia mikono yao.

43Mara nyingi aliwaopoa, lakini kwa mashauri yao wakamkataa, wakabanwa kwa ajili ya manza, walizozikora.

44Kisha akawatazama, jinsi walivyosongeka; alipoyasikia malalamiko yao, yalipoingia masikioni mwake,

45akalikumbuka Agano lake, alilolifanya nao, kwa upole wake mwingi akawahurumia,

46akawapatia huruma kwao wote waliowafunga.

47Tuokoe, Bwana, uliye Mungu wetu! Tukusanye na kututoa kwenye wamizimu, tupate kulishukuru Jina lako takatifu, tuzidishe kukusifu na kukushangilia![#5 Mose 30:3; 1 Mambo 16:35.]

48Na utukuzwe, Bwana Mungu wa Isiraeli, tangu kale hata kale!

Nayo makabila yote ya watu sharti yaitikie: Amin! Haleluya!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania