Mashangilio 141

Mashangilio 141

Kumwomba Mungu, atulinde.

1Bwana, nimekuita, unijie upesi! Isikilize sauti yangu, nikikuita!

2Maombo yangu na yapande kufika kwako kama moshi wa uvumba! Kipaji changu cha tambiko cha jioni ni mikono, nikuinuliayo.[#2 Mose 29:39; 30:7.]

3Bwana, ukiwekee mlinzi hiki kinywa changu, angoje penye huu mlango wa midomo yangu![#Sh. 39:2.]

4Usiugeuze moyo wangu kuelekea neno baya, nikijitendea matendo ya kukubeza pamoja nao wafanyao maovu, nisije kula vilaji vyao, ijapo viwe vya urembo![#Sh. 119:36.]

5Mwongofu akinipiga, anichape kwa upole! Hivyo vitakuwa kama mafuta ya kupaka kichwa, nacho kichwa changu hakitayakataa. Nami nimo bado katika kuomba kwa ajili ya mabaya yao wale.[#3 Mose 19:17; Fano. 27:5-6.]

6Waamuzi wao watakapokuwa wameangushwa magengeni, ndipo, watakapoyasikia maneno yangu, ya kuwa ni mazuri.

7Kama vilivyo hapo, mtu alipolima na kuchimbachimba, ndivyo, mifupa yetu ilivyotawanyika kwenye lango la kuzimu.

8Kwani wewe, Bwana Mungu, ndiwe unayetazamiwa na macho yangu, nimekukimbilia wewe, usiimwage roho yangu!

9Niangalie, nisinaswe na tanzi, walilonitegea, wala nisikamatwe na kamba zao wafanyao maovu!

10Wasiokucha sharti wanaswe wote pamoja na nyavu zao wenyewe, lakini mimi nipe, nizipite kabisa![#Sh. 7:16.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania