The chat will start when you send the first message.
1Nakupenda kwa moyo, Bwana, uliye nguvu yangu.
2Bwana ni ngome yangu na boma langu, tena ni mponya wangu, ni Mungu aliye mwamba wangu, kwa hiyo ninamjetea; ni ngao yangu na pembe ya kunipatia wokovu, tena ni kingo langu.[#5 Mose 32:4.]
3Bwana atukuzwaye ndiye, ninayemwitia; ndipo, ninapookolewa mikononi mwao walio adui zangu.
4Kamba ziuazo zilikuwa zimeniasamia, nayo majito yaangamizayo yalinistusha;[#Sh. 116:3.]
5kamba zivutiazo kuzimuni zilikuwa zimenizunguka, nayo mafungo yauayo yalikuwa mbele yangu.
6Hapo niliposongeka nalimwita Bwana, yeye aliye Mungu wangu nikamlalamikia, akaisikia sauti yangu Jumbani mwake, malalamiko yangu ya usoni pake yakamwingia masikioni mwake.
7Nchi ikatukutika na kutetemeka, nayo misingi ya milima ikatikisika kwa kutukuswa, kwani aliitolea makali yake yenye moto.
8Moshi ukapanda puani mwake, moto ulao ukatoka, kinywani mwake, makaa ya moto yakamulikamulika mbele yake.[#2 Mose 19:18.]
9Akatanda mbingu ya kushukiapo, mawingu meusi yakawa chini ya miguu yake.[#Sh. 144:5.]
10Akapanda gari, nalo likarushwa, likakimbizwa mbiombio mabawani mwa upepo.[#Sh. 99:1.]
11Akatumia giza kuwa ficho lake, limfunike pande zote likiwa kao lake; ndio mawingu meusi yenye mvua kali.[#Yes. 50:3.]
12Kwa nguvu ya kumulika mbele yake mawingu yakatutumka, mvua ya mawe ikanyesha pamoja na kupiga umeme.
13Bwana akapiga ngurumo kule mbinguni, Alioko huko juu akaivumisha sauti yake, mvua ya mawe ikanyesha pamoja na kupiga umeme.
14Alipoipiga mishale yake, akawatawanya, ngurumo zilipozidi kuwa nyingi, wakapigwa bumbuazi.[#1 Sam. 7:10.]
15Ndipo, ilipoonekana mikondo ya maji, nayo misingi ya nchi ikafunuliwa kwa nguvu ya makaripio ya kwako, Bwana, na kwa ukali wa pumzi ya pua yako.
16Akakunjua mkono toka juu, akanikamata, mle mlimo na maji mengi akanichopoa.[#Sh. 69:2-3; 144:7.]
17Akaniponya mikononi mwa adui yangu mwenye nguvu, namo mwao walionichukia kwa kuwa na uwezo kuliko mimi.
18Walikuwa wamenijia mbele ile siku, nilipokuwa nimeshindwa, lakini Bwana akanijia kuwa shikizo.
19Akanitoa kwao, akanikalisha palipo papana; ndivyo, alivyoniopoa kwa kupendezwa nami.[#Sh. 18:37.]
20Yaupasayo wongofu wangu Bwana alinipa, akanipatia tena yaupasayo ung'avu wa mikono yangu.
21Kwani naliziangalia njia zake Bwana, nisifanye kilicho kiovu mbele yake Mungu wangu.
22Kwani maamuzi yake yote yako mbele yangu, nayo maongozi yake sikuyaacha, nisiyafuate.[#5 Mose 17:19.]
23Nikawa naye pasipo kuonywa, nikajiangalia, nisimkosee.[#Sh. 15:2.]
24Bwana akanipatia tena yaupasayo wongofu wangu, kwa kuwa mikono yangu ilikuwa imeng'aa machoni pake.
25Wewe humwia mpole aliye mpole, naye aliye mkweli wote nawe humwia mkweli wote.
26Wewe humwia mng'avu aliye mng'avu, lakini aliye mpotovu nawe humpotokea.
27Kwani walio wanyonge wewe huwaokoa, lakini macho yajivunayo huyanyenyekeza.[#Iy. 22:29; 1 Petr. 5:5.]
28Kwani wewe ndiye anayeiwasha taa yangu, wewe Bwana, Mungu wangu, huliangaza nalo giza langu.
29Kwani nitashambulia vikosi vizima kwa nguvu yako, kwa nguvu ya Mungu wangu narukia napo ukutani.[#Sh. 60:12.]
30Njia yake Mungu haipindiki, Neno lake Bwana limeng'azwa. Yeye ni ngao yao wote wamkimbiliao.[#Sh. 19:9.]
31Kwani yuko nani aliye Mungu, asipokuwa Bwana? Tena yuko nani aliye mwamba, asipokuwa Mungu wetu?
32Ni yeye Mungu aliyenivika nguvu, njia yangu huitengeneza, iwe imenyoka kabisa.
33Hunipatia miguu ikimbiayo kama ya kulungu, anisimamishe kwangu vilimani juu.
34Huifundisha mikono yangu kupiga vita, mpaka mikono yangu iweze kupinda hata uta wa shaba.[#Sh. 144:1.]
35Hunipa ngao ya kuniokoa, kuumeni kwako hunishikiza, napo hapo, unaponinyenyekeza, hunikuza.[#Fano. 15:33.]
36Huipanulia miguu yangu, ipate pa kupitia, viwiko vyangu vya miguu visiteleze.[#Sh. 31:9.]
37Nitawakimbiza adui zangu, mpaka niwakamate; sitarudi, nisipokwisha kuwamaliza.
38Nitawaponda, wasiweze kuinuka tena. Sharti waanguke miguuni pangu.
39Hunivika nguvu ya kupiga vita, huwalaza chini yangu wao waniinukiao.
40Hunipa adui zangu, niwaone migongo, nipate kuwanyamazisha wachukivu wangu.
41Hakuna mwokozi, wanapolalamika, wanapomwitia Bwana, hawaitikii.[#Fano. 1:28.]
42Nitawaponda, mpaka wabunguke kama mavumbi upeponi, niwazoe kama mataka yaliyoko viwanjani.
43Kwenye magomvi ya watu ulinitoa, ukanipa kuwa kichwa chao wao wamizimu, watu, ambao nilikuwa siwajui, wanitumikie.
44Masikio yao yanaponisikia, hunitii, nao watokao mbali hunipongeza.
45Hao watokao mbali walikuwa wamenyauka, walipotoka mabomani kwao na kutetemeka.
46Bwana Mwenye uzima ni mwamba wangu upasao kusifiwa, yeye Mungu aliyeniokoa sharti atukuke!
47Mungu ndiye aliyenipatia malipizi na kuteka makabila ya watu, wanitii.
48Wewe ndiwe uliyeniokoa mikononi mwao walio adui zangu, kwao waniinukiao ukaniweka kuwa mkuu wao, kwao walionikorofisha ukaniponya.
49Kwa hiyo nitakushukuru, Bwana, kwenye wamizimu, nalo Jina lako na niliimbie.[#Rom. 15:9.]
50Mfalme wake alimpatia wokovu mwingi, aliyempaka mafuta humfanyizia yenye upole; huyo ni Dawidi naye aliye wa uzao wake kale na kale.[#2 Sam. 7:12-16.]