Mashangilio 34

Mashangilio 34

Mungu huwaokoa walio wake katika masumbuko yote.

Wa Dawidi. Ilikuwa hapo, alipojitendekeza kuwa kama mwenye wazimu usoni pa Abimeleki, hata akamfukuza, aende zake.

1*Nitamtukuza Bwana siku zote, mashangilio yake yakae midomoni mwangu pasipo kukoma.[#1 Sam. 21:13-15.]

2Roho yangu inayejivunia, ndiye Bwana, wakiwa na wayasikie, wapate kufurahi.[#Luk. 1:46.]

3Mkuzeni Bwana pamoja nami! Na tulitukuze pamoja jina lake!

4Nilipomtafuta Bwana, akaniitikia, katika woga wangu wote akaniponya.

5Wanaomtazamia huchagamka, maana nyuso zao hazitatwezwa.

6Kama yuko mnyonge aliyeita, Bwana husikia, katika masongano yake yote humwokoa.

7Malaika wa Bwana huwakingia wao wamwogopao, huwa kwao pande zote, apate kuwaponya.[#Sh. 91:11; 1 Mose 32:1.]

8Onjeni, mwone, ya kuwa Bwana ni mwema! Mwenye shangwe ni mtu amkimbiliaye.*[#2 Fal. 6:17; 1 Petr. 2:3.]

9Mwogopeni Bwana, ninyi watakatifu wake! Kwani kwao wamwogopao hakuna ukosefu.[#Sh. 37:19.]

10Wana wa simba hukosa na kuona njaa, lakini hakuna chema, watakachokikosa wamtafutao Bwana.[#Sh. 33:18-19; 37:25; Luk. 1:53.]

11Njoni, ninyi wana, mnisikilize, kumwogopa Bwana ndiko, nitakakowafundisha.

12Mtu apendezwaye na uzima yuko wapi? naye apendaye siku za kuona mema?[#1 Petr. 3:10-12.]

13Uulinde ulimi wako, usiseme mabaya, nayo midomo yako, isiseme madanganyifu!

14Yaliyo mabaya yaepuke, ufanye mema! Tafuta penye utengemano, upakimbilie![#Sh. 37:27.]

15Macho ya Bwana huwatazama walio waongofu, masikio yake huvisikiliza vilio vyao.

16Uso wa Bwana huwapingia wafanyao mabaya, awang'oe, wasikumbukwe tena katika nchi.[#Fano. 10:7.]

17Waongofu wanapoita, Bwana huwasikia, katika masongano yao yote hutaka kuwaponya.

18Bwana yuko karibu kwao waliovunjika mioyo, wapondekao roho huwaokoa.[#Sh. 51:19.]

19Kweli, mabaya mengi humpata aliye mwongofu, lakini katika hayo yote Bwana humponya.[#2 Kor. 1:5.]

20Nayo mifupa yake yote huiangalia, hata mmoja miongoni mwao usivunjike.

21Ubaya utamwua asiyemcha Mungu, nao wachukiao wongofu watakuwa wenye manza;

22lakini roho zao watumishi wake Bwana huzikomboa, wao wote wamkimbiliao, wawe watu wasio wenye manza.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania