The chat will start when you send the first message.
1*Kama kuro anavyolilia maji ya mtoni, ndivyo, roho yangu inavyokulilia wewe, Mungu.[#2 Mambo 20:19.]
2Roho yangu ina kiu ya kunywea kwake Mungu, kwake yeye aliye Mungu Mwenye uzima. Itakuwa lini, nitakapoonekana usoni pake Mungu?[#Sh. 84:3.]
3Machozi yangu ndio chakula changu mchana na usiku, maana watu huniambia kila siku: Mungu wako yuko wapi?[#Sh. 79:10.]
4Ndipo, ninapoumimina moyo wangu ndani yangu kwa kuvikumbuka hivyo, nilivyokwenda na kikosi cha watu nilipowaongoza na kuwapeleka Nyumbani kwa Mungu, wao wakipiga vigelegele vya kumshukuru, wakawa kundi kubwa la watu waliokula sikukuu.[#Sh. 27:4.]
5Mbona unajihangaisha, roho yangu, ukivuma ndani yangu? Mngoje Mungu na kumtazamia! Kwani siku itakuja, nitakapomshukuru kwa kuokolewa nao uso wake.[#Sh. 42:11; 43:5.]
6Roho yangu inajihangaisha humu ndani yangu, kwa sababu hii ninakukumbuka huku, niliko katika nchi za Yordani kwenye Hermoni nako mlimani kwa Misari.
7Maanguko yako ya maji yakinguruma, vilindi vinaitana, kisha mafuriko na mawimbi yako yote huja kunifunika.[#Sh. 88:8.]
8Mchana Bwana na aniagizie upole wake, usiku nipate kumwimbia na kumwomba Mungu anipaye uzima.
9Nitamwambia Mungu aliyemwamba wangu: Mbona umenisahau? Mbona sina budi kwenda na kusikitika, adui anaponisonga?[#5 Mose 32:4; Sh. 43:2.]
10Mifupa yangu inakuwa imepondeka sana, wanisongao wakinitukana, wakiniambia kila siku: Mungu wako yuko wapi?
11Mbona unajihangaisha, roho yangu, ukivuma ndani yangu? Mngoje Mungu na kumtazamia, kwani siku itakuja, nitakapomshukuru kwa kuokolewa nao uso wake.*[#Sh. 42:6.]