Mashangilio 83

Mashangilio 83

Kuomba msaada vitani.

1Mungu usijinyamazie tu! Wala usiache kujibu! Usitulie tu, wewe Mungu!

2Kwani tazama, adui zako wanafanya fujo! Wachukivu wako wanainua vichwa!

3Wanakula njama ya kuwaangamiza walio ukoo wako, wanawapigia mashauri mabaya wao, uliowaficha.[#Sh. 27:5; 35:20.]

4Wanasema: Njoni, tuwang'oe, kabila lao life! Jina la Isiraeli lisikumbukwe tena!

5Kweli mioyo yao wote ililipatana neno hili moja, wakafanya maagano, wakupelekee vita.

6Ni wao wakaao katika mahema: Waedomu na Waisimaeli, Wamoabu nao wao walio Wahagri,

7tena Wagebali na Waamoni, nao Waamaleki, Wafilisti pamoja nao wakaao Tiro.

8Katika hilo shauri lao wakajitia nao Waasuri; nao ndio wanaowatumikia wana wa Loti kuwa mikono yao.

9Kama ulivyowafanyizia Wamidiani, wafanyizie nao, au kama ulivyomfanyizia Sisera na Yabini kule mtoni kwa Kisoni![#Amu. 4:15,21,23; 7:22.]

10Kule Endori ndiko, walikoangamizwa, wakawa mbolea tu ya kuotesha mchanga.

11Hivyo, ulivyomfanyizia Orebu na Zebu vifanyizie wakuu wao! Vile vya Zeba na Salmuna, vifanyizie wafalme wao wote![#Amu. 7:25; 8:21.]

12Ndio waliosema: Na tuyateke makao yake Mungu, yawe yetu sisi![#Sh. 74:8.]

13Mungu wangu, wafanye kuwa mavumbi yachukuliwayo na kimbunga au kuwa makapi, yakipeperushwa na upepo,

14wawe kama moto unaochoma mwitu, au kama ndimi za moto ziwashazo milima!

15Vivyo hivyo uwakimbize kwa nguvu zako zilizo za kimbunga! Uwastushe, wazimie kwa nguvu zako zilizo za chamchela!

16Nyuso zao sharti ziwaive kwa kutwezwa, mpaka walitafute Jina lako, wewe Bwana.

17Sharti wapatwe na soni pamoja na mastuko kale na kale! Sharti waumbuliwe, mpaka waangamie!

18Ndivyo, watu watakavyolitambua Jina lako kuwa Bwana, kwa kuwa wewe peke yako u mkuu katika nchi zote.[#Hos. 12:6.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania