Mashangilio 89

Mashangilio 89

Dawidi aliyoagiwa.

(Taz. 2 Sam. 7:8-16.)

1Magawio ya Bwana nitayaimbia kale na kale,[#1 Fal. 4:31.]

2vizazi na vizazi nitawajulisha kwa kinywa changu welekevu wako.

3Kwani nasema: Upole wako utajengewa kale na kale, mbinguni uliusimika welekevu wako, uwapatie watu nguvu.

4Ukasema: Niliagana naye niliyemchagua, mtumishi wangu Dawidi nikamwapia kwamba:[#Sh. 132:11; Yes. 55:3; Tume. 2:30.]

5Walio uzao wako nitawatia nguvu kale nakale, nikijenge kiti chako cha ufalme, kiwe cha vizazi na vizazi.[#2 Sam. 7:16.]

6Ndipo, mbingu zilipoyatukuza mataajabu yako, Bwana, welekevu wako ukatukuzwa nao kwenye mkutano wa watakatifu.

7Kwani kule mawinguni yuko nani aliye mkuu kama Bwana? Nako kwenye wana wa Kimungu yuko nani afananaye na Bwana?[#Iy. 1:6.]

8Watakatifu wakusanyikapo, Mungu huogopesha, nao wote wamzungukao hushikwa na woga.

9Bwana Mungu Mwenye vikosi, yuko nani aliye hivyo, ulivyo? U Bwana mwenye nguvu, welekevu wako unakuzunguka.[#Sh. 115:3.]

10Unayashinda hata majivuna yake bahari, mawimbi yake yakiumuka, unayatuliza.[#Sh. 65:8; Mat. 8:26; Iy. 38:8,11.]

11Wewe ulimponda Rahabu, akaanguka kama mtu aumizwaye vitani, kwa mkono wako wenye nguvu ukawatapanya adui zako.[#Sh. 87:4; Yes. 30:7.]

12Mbingu ni zako, nchi nayo ni yako, kwani nchi navyo vyote vilivyoko ulivishikiza wewe.[#Sh. 24:1.]

13Vilivyoko kaskazini navyo vilivyoko kusini wewe uliviumba, milima ya Tabori na ya Hermoni inalipigia Jina lako shangwe.

14Mkono wako ni wenye uwezo sanasana, maganja yako nayo ni yenye nguvu, mkono wako wa kuume hutukuka.

15Wongofu unyoshao maamuzi ni msingi wa kiti chako cha kifalme, upole na welekevu huutangulia uso wako.[#Sh. 97:2.]

16Watu wajuao kushangilia ndio wenye shangwe, huendelea katika mwanga wa uso wako, Bwana.[#Sh. 47:6.]

17Jina lako wanalipigia vigelegele siku zote, maana kwa wongofu wako walipata ukuu.

18Kwani utukufu wa nguvu zao ni wewe, Bwana. mapenzi yako ndiyo yatupayo kuyaelekeza mabaragumu yetu juu.

19Kwani aliye mwenye ngao yetu ndiye Bwana, naye mfalme wetu ni wake Mtakatifu wa Isiraeli.[#Sh. 47:9.]

20Kale ulisema katika njozi nao waliokucha, ukawaambia: Yuko mwenye nguvu, niliyempa ushindaji; niliyemchagua nimemkweza, awapite wote ukuu.[#Sh. 89:4; 1 Sam. 13:14; 2 Sam. 7:4.]

21Nimemwona Dawidi, awe mtumishi wangu, nikampaka mafuta yangu yaliyo matakatifu.[#1 Sam. 16:13.]

22Maganja yangu yatamshikiza, kweli mkono wangu utamtia nguvu.

23Hakuna adui atakayemshinda na kumwogopea, wala hakuna mkorofi atakayemtesa.

24Mimi nitawapiga wamsongao, wakimbie watakapomwona, nao wachukivu wake nitawakumba, waanguke.

25Welekevu wangu na upole wangu utamkalia, kwa nguvu ya Jina langu atalielekeza baragumu lake juu.[#Sh. 132:17; 1 Sam. 2:10.]

26Mikono yake nitaifikisha kwenye bahari, mkono wake wa kuume sharti uje kwenye mito mikubwa.[#Sh. 72:8.]

27Yeye ataniita na kuniambia: Baba yangu ni wewe, u Mungu wangu nao mwamba ulio wokovu wangu.[#2 Sam. 7:14.]

28Mimi nami nitampa uzaliwa wa kwanza, na ukuu wa wafalme wa nchini.

29Kale na kale nitamwendea kwa upole wangu, nalo agano tuliloliagana, halitatanguka.[#Yes. 54:10.]

30Mazao ya kuwa ya kale na kale ndiyo, nitakayompa, nazo siku za kiti chake cha kifalme zitakuwa kama za mbingu.

31Watoto wake wakiyaacha Maonyo yangu, wasiendelee na kuyafanya yanyokayo machoni pangu,

32wakiyapinga maongozi yangu, wasiyaangalie maagizo yangu,

33Nitawaonya na kuwapiga fimbo kwa kukataa kunitii, hayo maumivu yawlaipishe manza zao, walizozikora.

34Lakini upole wangu sitawanyima, wala sitageuka kuwa mwongo, welekevu wangu ukiwaacha.

35Wala Agano langu sitalitangua, wala sitayageuzageuza yaliyotoka midomoni mwangu.

36Neno moja nimejiapia kwa utakatifu wangu, nami sitamwongopea Dawidi, ni lile la kwamba:

37Uzao wake utakuwa wa kale na kale, nacho kiti chake cha kifalme kitakuwa kama jua machoni pangu,[#Sh. 72:17; 2 Sam. 7:12-16.]

38kitakaa na nguvu yake kale na kale kama mwezi. Naye shahidi alioko huko juu mawinguni ni mwelekevu.[#1 Mose 9:13.]

39Kisha wewe umemtupa na kumkataa; yeye, uliyempaka mafuta, umemchafukia.[#Sh. 44:10-25; 74; 79.]

40Agano, uliloliagana na mtumishi wako, umeliacha, urembo wake wa kichwani umeuchafua na kuutupa chini.

41Umevivunja vitalu vyake vyote pia, maboma yake yote umeyatoa, yabomolewe.

42Wote wapitao njia wanajipatia mateka papo hapo, naye amegeuka kuwa mtu wakusimangwa tu kwao, aliokaa nao.[#Sh. 80:13.]

43Umeikweza mikono yao ya kuume wao wamsongao, adui zake wote umewafurahisha.

44Hata ukali wa upanga wake umeurudisha nyuma, usipompa kusimama kwenye mapigano.

45Umeukomesha uzuri wake wa kifalme, usiwepo tena, nacho kiti chake cha kifalme umekibwaga chini.

46Siku za ujana wake umezifupiza, ukamtia soni, zimfunike kama nguo.

47Bwana, utajificha hivyo mpaka lini? Moto wa makali yako uwake kale na kale?[#Sh. 85:6.]

48Zikumbuke siku zangu, jinsi zinavyoishia upesi! Mbona wana wa watu wote ulijiumbia, wawe wa bure?[#Sh. 90:9-10.]

49Ni mtu gani anayekuwapo pasipo kuona kufa? Ni mtu gani atakayeiopoa roho yake katika nguvu za kuzimuni?

50Bwana, magawio ya upole wako ya kwanza yako wapi sasa? Tena ulimwapia Dawidi kwa welekevu wako, ayapate![#Sh. 85:2.]

51Wakumbuke, Bwana, watumishi wako, jinsi wanavyosimangwa! Nayavumilia moyoni mwangu mabezo yamakabila yote, nayo ni mengi.

52Bwana, ndivyo, wanavyokusimanga wachukivu wako, tena ndivyo, wanavyozisimanga nazo nyayo zake, uliyempaka mafuta!

53Bwana na atukuzwe kale na kale! Amin. Amin.[#Sh. 41:13.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania