Ufunuo 17

Mji wa Babeli ni mgoni mkubwa wa kike.

1Pakaja mmoja wao wale malaika saba wenye vile vyano saba, akasema nami kwamba: Njoo, nitakuonyesha hukumu yake yule mgoni mkubwa wa kike akaaye juu ya maji mengi.[#Ufu. 15:1.]

2Yeye ndiye, ambaye wafalme wa nchi walifanya ugoni naye, nao wakaao nchini wakijilevya na mvinyo ya ugoni wake.[#Ufu. 14:8; 18:3.]

3Aliponipeleka kiroho nyikani, nikaona mwanamke aliyepanda nyama mwekundu aliyejaa majina yenye matusi, naye alikuwa na vichwa saba na pembe kumi.[#Ufu. 13:1.]

4Yule mwanamke alikuwa amevaa nguo nyekundu za kifalme, tena alikuwa amejipamba na dhahabu na kito chenye kima kikuu na ushanga wa lulu. Mkononi mwake alishika kinyweo cha dhahabu kilichojaa machukizo na machafu ya ugoni wake.[#Yer. 51:7; Ez. 28:13,16.]

5Tena pajini pake palikuwa pameandikwa jina lisilofumbulika: Mji mkubwa wa Babeli, mama ya wagoni na ya machukizo ya nchini.[#Ufu. 14:8; 16:19; Dan. 4:27; 2 Tes. 2:7.]

6Ndipo, nilipomwona yule mwanamke, alivyolewa kwa damu za watakatifu na kwa damu za mashahidi wa Yesu. Nami nilipomwona nikastaajabu mastaajabu makubwa mno.[#Ufu. 18:24.]

Maana yao vichwa saba na pembe kumi.

7Kisha malaika akaniambia: Kwa nini unastaajabu? Nitakuambia fumbo la mwanamke na la nyama mwenye vichwa saba na pembe kumi anayemchukua.

8Yule nyama, uliyemwona, alikuwapo kale, naye sasa hayupo; lakini atatoka tena kuzimuni, aende kwenye maangamizo. Ndipo, wakaao nchini wasioandikwa majina yao katika kitabu cha uzima tangu hapo, ulimwengu ulipoumbwa, watakapostaajabu, watakapomwona huyo nyama aliyekuwapo kale, ya kuwa sasa hayupo, lakini halafu atakuwapo tena.[#Ufu. 3:5; 13:1-3.]

9Hapo ndipo, panapotakwa werevu wa kweli: vile vichwa saba ni milima saba, ndiyo, yule mwanamke anayokalia juu; nayo ni wafalme saba.[#Ufu. 13:1,18.]

10Watano wamekwisha kuanguka; mmoja yuko, naye mwingine hajaja bado. Huyo atakapokuja, sharti akae kidogo.

11Yule nyama aliyekuwapo kale, aliyetoweka sasa, ndiye yeye wa nane. Naye ni mwenye mwenzao wale saba, naye anakwenda kwenye maangamizo.[#Ufu. 17:8; 19:20.]

12Nazo zile pembe kumi, ulizoziona, ni wafalme kumi, wasiopewa bado ufalme, ila watapewa nguvu kama za wafalme saa moja pamoja na yule nyama.[#Ufu. 13:1; Dan. 7:20,24.]

13Hao neno lao ni moja la kumpa yule nyama uwezo wao na nguvu zao.

14Ndio watakaopiga vita na Mwana kondoo, lakini Mwana kondoo atawashinda, kwani yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme, anao waitwao, nao wachaguliwao, nao wamtegemeao.[#Ufu. 19:14,16.]

15Kisha akaniambia: Yale maji, uliyoyaona, yule mgoni wa kike anayoyakalia, ndiyo makabila ya watu na makutano na wamizimu na misemo.[#Ufu. 17:1; Yes. 8:7; Yer. 47:2.]

16Nazo zile pembe kumi, ulizoziona, pamoja na yule nyama ndio watakaomchukia yule mgoni wa kike na kumpokonya yote, uchi wake uonekane. Ndio watakaozila nyama za mwili wake, lakini mwenyewe watamteketeza motoni.[#Ufu. 17:12-13; 18:8.]

17Kwani Mungu aliwatia mioyoni mwao kuyafanya, ayatambuayo yeye, wapatane kumpa yule nyama ufalme wao, mpaka maneno ya Mungu yatakapotimizwa.[#Ufu. 10:7.]

18Tena yule mwanamke, uliyemwona, ndio ule mji mkubwa ulio na ufalme wa wafalme wa nchini.[#Ufu. 18:10.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania