Waroma 8

Waroma 8

Kimtu na Kiroho.

1*Sasa hakuna tena kinachowapatiliza walio katika Kristo Yesu, wasioendelea kimtu, ila Kiroho.[#Rom. 5:18; 8:4,31-39.]

2Kwani Maonyo ya Roho inayotupatia uzima katika Kristo Yesu yamenikomboa utumwani mwa maonyo ya ukosaji yaliyoniua.[#Rom. 3:27; 7:23-25.]

3Kwani vile, ambavyo Maonyo hayakuweza kuvimaliza kwa ajili ya unyonge wa miili ya kimtu, Mungu alivifanya alipomtuma Mwana wake mwenyewe; akaja mwenye mwili wa makosa, akakamatwa kuwa kole ya makosa; hivyo ndivyo, alivyoyapatiliza makosa katika mwili ulio wa kimtu,[#Tume. 13:38; 15:10; Ebr. 2:17.]

4wongofu unaotakwa na yale Maonyo utimilizike mioyoni mwetu sisi, tusioendelea kimtu, ila Kiroho.[#Gal. 5:16,25.]

5Kwani walio wa kimtu huyawaza mambo ya kimtu, lakini walio wa Kiroho huyawaza mambo ya Kiroho.

6Kwani mawazo ya kimtu huleta kufa; lakini mawazo ya Kiroho huleta uzima na utengemano.[#Rom. 6:21; Gal. 6:8.]

7Kwa sababu hiyo mawazo ya kimtu humchukia Mungu; kwani hayataki kuyatii Maonyo ya Mungu, wala hayawezi kuyatii;[#Yak. 4:4.]

8kwa hiyo walio wa kimtu hawawezi kumpendeza Mungu.

9Lakini ninyi ham wa kimtu, ila wa Kiroho, kama Roho ya Mungu inawakalia mioyoni; lakini asiye na Roho ya Kristo huyo si wake.[#1 Kor. 3:16.]

10Lakini Kristo akiwakalia mioyoni, kweli miili itakufa kwa ajili ya makosa, lakini roho zitaishi kwa ajili ya wongofu.[#Gal. 2:20.]

11Lakini Roho yake yule aliyemfufua Yesu katika wafu ikiwakalia mioyoni, yuyu huyu aliyemfufua Yesu Kristo katika wafu atairudisha uzimani hata miili yenu, itakapokwisha kufa; atayafanya kwa nguvu ya Roho yake inayowakalia mioyoni.

Roho ya kimwana.

12*Kwa hiyo, ndugu, hatumo tena katika udeni wa miili yetu ya kimtu, tuendelee kimtu;[#Rom. 6:7,18.]

13kwani mnapoendelea kimtu mtakufa. Lakini mnapoyaua matendo ya miili yenu ya kimtu kwa nguvu ya Roho mtapata kuishi.[#Gal. 6:8; Ef. 4:22-24.]

14Kwani wote wanaoongozwa na Roho ya Mungu hao ndio wana wa Mungu.

15Kwani hamkupewa tena roho ya kitumwa, mshikwe na woga, ila mmepewa Roho ya kimwana, ndiyo inayotufundisha kuomba: Ee, Baba yetu![#Gal. 4:5-6; 2 Tim. 1:7.]

16Hiyo Roho yake yenyewe huzishuhudia roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wake Mungu.[#2 Kor. 1:22.]

17Lakini tukiwa watoto, basi, tunakuwa hata warithi, maana warithi wake Mungu watakaopata urithi pamoja na Kristo; tukiwa tunateswa pamoja naye tutapata hata kutukuzwa pamoja naye.[#Gal. 4:7; Ufu. 21:7.]

Utukufu tutakaofunuliwa.

18*Kwani naona, ya kuwa mateso ya siku hizi za sasa si kitu, tukiyafananisha na ule utukufu, tutakaofunuliwa sisi.[#2 Kor. 4:17.]

19Kwani viumbe vyote vinavumilia na kuyachungulia matokeo ya wana wa Mungu.[#Kol. 3:4.]

20Kwani viumbe vimewekwa, vioze, si kwa mapenzi yao wenyewe, ila kwa ajili yake aliyeviweka hivyo; navyo viko na kingojeo chao.[#1 Mose 3:17-19; 5:29; Mbiu. 1:2.]

21Kwani viumbe navyo vitakombolewa katika utumwa wa kuoza, viingie navyo uungwana uliomo katika utukufu wa watoto wake Mungu.[#2 Petr. 3:13.]

22Kwani twajua, ya kuwa viumbe vyote vipo pamoja nasi vikipiga kite kwa kuona uchungu mpaka sasa hivi.

23Tena sivyo hivyo tu, ila na sisi wenyewe tuliokwisha pata malimbuko ya Roho twapiga kite ndani mioyoni tukichungulia kuwa wana, kwani ndipo, miili yetu nayo itakapokombolewa.[#1 Kor. 12:7; 2 Kor. 1:22; 5:2; Gal. 5:22.]

24*Kwani kingojeo, ambacho tuliokolewa, tuwe nacho, hicho ndicho; lakini kingojeo kinachoonekana machoni sicho kingojeo. kwani hilo, mtu analoliona, analingojeaje?[#2 Kor. 5:7.]

25Lakini tusiloliona, tukilingojea, tunalichungulia kwa kuvumilia.

Kuombewa na Roho.

26Hivyo hata Roho hutusaidia sisi tulio wanyonge. Kwani tusipojua maombo yanayopasa, hapo Roho mwenyewe hutuombea, tukipiga kitekite tu kisichosemekana.

27Lakini yeye nayeipeleleza mioyo ameyajua mawazo ya Roho, kwani huwasemea watakatifu Kimungu.*

Nguvu ya kumtegemea Bwana.

28Tunajua, ya kuwa: Kwao wanaompenda Mungu mambo yote husaidiana kuwapatia mema; ndio hao, aliowaita kwa yale, aliyowawekea kale.[#Rom. 9:11-12; Ef. 1:11; 3:11.]

29Kwani aliowatambua kale, ndio, aliowachagua kale, wafanane na Mwana wake wakiwa sura moja naye, yeye apate kuwa Kibwana katika wanduguze wengi.[#Kol. 1:18; Ebr. 1:6.]

30Nao aliowachagua kale, hao ndio, aliowaita; nao aliowaita, hao ndio aliowapa wongofu; nao aliowapa wongofu, hao ndio, aliowatukuza.

31Hayo yote tuyasemeje? Mungu akiwa upande wetu, yuko nani atakayetushinda?[#Sh. 118:6.]

32Hakumwonea Mwana wake mwenyewe uchungu, ila alimtoa kwa ajili yetu sisi sote; kwa hiyo asitupatie sisi magawio yote kwake yeye?*[#Yoh. 3:16.]

33*Yuko nani atakayewasuta waliochaguliwa na Mungu? Mungu yuko anayewashuhudia kuwa waongofu.

34Yuko nani atakayewahukumu? Kristo Yesu yuko aliyekufa kwa ajili yao, na kupita hapo amefufuka, yuko kuumeni kwa Mungu na kutusemea sisi.[#Rom. 8:1; 1 Yoh. 2:1.]

35Yuko nani atakayetutenga na upendo wake Kristo? Maumivu au masongano au mafukuzo au njaa au uchi au maponzo au panga?

36Ndivyo vilivyoandikwa kwamba:

Kumbe ni kwa ajili yako wewe, tukiuawa kila siku

tukihesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa tu!

37Lakini katika mambo hayo yote tunazidi kushinda kabisa kwa nguvu yake yeye aliyetupenda sisi.[#Yoh. 16:33; Ufu. 12:11.]

38Kwani hili nimelitambua kuwa kweli kabisa: Kukiwa kufa au kuishi, wakiwa malaika au wenye nguvu, yakiwa ya leo au ya kale, zikiwa nguvu[#Ef. 6:12.]

39za mbinguni juu au za kuzimuni chini, vikiwa viumbe vyo vyote vingine, hakuna kitakachoweza kututenga sisi na upendo wake Mungu uliotutokea katika Kristo Yesu, Bwana wetu.*

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania