Zakaria 12

Zakaria 12

Mungu atawaokoa Wayerusalemu na Wayuda.

1Tamko zito la Bwana, alilowaambia Waisiraeli. Ndivyo, asemavyo Bwana aliyezitanda mbingu, aliyeuweka msingi wa nchi, aliyeiumba roho ya mtu ndani yake:

2Mtaniona, nikiuweka Yerusalemu kuwa chano cha kuwalevya sana wao wa makabila yote wanaokaa na kuuzunguka; hata Wayuda watapatwa na mambo, Yerusalemu utakaposongwa.[#Yes. 51:17.]

3Siku hiyo ndipo, nitakapouweka Yerusalemu kuwa jiwe zito zaidi lisilochukulika na makabila yote, nao watakaojaribu kulichukua watajiumiza vibaya, ijapo mataifa yote pia ya hapa nchini yaje kukusanyika, yalichukue.[#Zak. 14:2; Yoe. 3:12.]

4Ndivyo, asemavyo Bwana: Siku hiyo ndipo, nitakapowapiga farasi wote, waingiwe na mastuko, nao wawapandao wapatwe na wazimu; juu yao walio mlango wa Yuda nitayafumbua macho yangu, yawatazame, lakini farasi wote wa makabila ya watu nitawapiga, wapofuke.

5Ndipo, wakuu wa Yuda watakaposema mioyoni mwao: Wenyeji wa Yerusalemu ndio nguvu zetu, kwa kuwa tunaye Bwana Mwenye vikosi aliye Mungu wake.

6Siku hiyo ndipo, nitakapowaweka wakuu wa Yuda kuwa kama chetezo cha moto penye kuni na kama mienge ya moto penye miganda mikavu, wapate kuwala kuumeni na kushotoni watu wa makabila yote pia wakaao na kuwazunguka, lakini Yerusalemu utakaa papo hapo mahali pake pa Yerusalemu.[#Oba. 18.]

7Lakini kwanza Bwana atayaokoa mahema ya Yuda, kusudi utukufu wao walio mlango wa Dawidi nao utukufu wao wenyeji wa Yerusalemu usijikuze na kuwabeza Wayuda.

8Siku hiyo ndipo, Bwana atakapowakingia wenyeji wa Yerusalemu, aliye mnyonge kwao siku hiyo awe kama Dawidi, nao walio wa mlango wa Dawidi wawe kama Mungu, kama malaika wa Bwana awaongozaye.[#Yes. 33:24.]

9Siku hiyo ndipo, nitakapowatafuta, niwaangamize wamizimu wote wajao kupigana na Yerusalemu.[#Ufu. 20:9.]

Kiagio cha Roho takatifu. Kumwombolezea, waliyemchoma.

10Wao walio wa mlango wa Dawidi nao wenyeji wa Yerusalemu nitawamiminia Roho ya kuhurumiana na ya kuombeana; ndipo, watakaponitazama, waliyemchoma. Kisha wataniombolezea, kama watu wanavyomwombolezea mwana wa pekee, nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama mtu anavyoona uchungu kwa ajili ya mwana aliyezaliwa wa kwanza.[#Yoe. 2:28; Yoh. 19:37; Ufu. 1:7.]

11Siku hiyo maombolezo yatakuwa mengi mle Yerusalemu, kama maombolezo yalivyokuwa mengi mle Hadadi-Rimoni kule bondeni kwa Megido.

12Nao wenyeji wa nchi hii wataomboleza kila mlango peke yake: Walio wa mlango wa Dawidi peke yao, nao wanawake wao peke yao, walio wa mlango wa Natani peke yao, nao wanawake wao peke yao.

13Walio wa mlango wa Lawi peke yao, nao wanawake wao peke yao; walio wa mlango wa Simei peke yao, nao wanawake wao peke yao.

14Vivyo hivyo milango yote itakayokuwa imesalia, wao wa kila mlango peke yao, nao wanawake peke yao.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania