Zakaria 8

Zakaria 8

Wokovu wao walio ukoo wake Mungu.

1Neno la Bwana Mwenye vikosi likanijia la kwamba:

2Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Nimeingiwa na wivu mwingi sana kwa ajili ya Sioni, wivu huu ukanitia makali mengi yenye moto kwa ajili yake.[#Zak. 1:14-15.]

3Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Nitarudi Sioni, nikae katikati ya Yerusalemu, nao Yerusalemu utaitwa mji wenye kweli, nao mlima wa Bwana Mwenye vikosi utaitwa mlima mtakatifu.[#Zak. 1:16.]

4Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Itakuwa tena, wazee wa kiume na wa kike wakae katika barabara za Yerusalemu, kila akishika mkongojo mkononi mwake kwa kuwa mzee kabisa.[#Yes. 65:20.]

5Tena barabara za mji huu zitajaa watoto wa kiume na wa kike watakaocheza palepale barabarani.

6Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Je? Yanayokuwa mambo yasiyowezekana machoni pao walio masao ya ukoo huu yawe napo machoni pangu mambo yasiyowezekana? Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi.[#Luk. 1:37.]

7Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Mtaniona, nikiwaokoa walio ukoo wangu na kuwatoa katika nchi ya maawioni kwa jua na katika nchi ya machweoni kwa jua.

8Kisha nitawaleta, wakae katikati ya Yerusalemu, nao watakuwa ukoo wangu, nami nitakuwa Mungu wao kwa kweli na kwa wongofu.[#Yer. 24:7.]

9Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Itieni mikono yenu nguvu, ninyi mnaoyasikia siku hizi maneno haya vinywani mwa wafumbuaji walioyasema siku hiyo, msingi wa Nyumba ya Bwana Mwenye vikosi ulipowekwa, ijengwe kuwa Jumba lake.[#Yes. 35:3.]

10Kwani kabla ya siku hizi hakikuwako kitu, watu walichokipata kwa kazi zao, wala hakikuwako, nyama walichokipata kwa kazi zao, tena kwa ajili ya kupingana hawakupata kutengemana wala aliyetoka wala aliyeingia, maana naliwachochea watu wote, wagombane kila mtu na mwenziwe.

11Lakini sasa mimi sitawaendea walio masao ya ukoo huu, kama nilivyowaendea siku zile za kwanza; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi.

12Kwani watapanda na kutengemana: mizabibu itazaa matunda yao, nayo nchi italeta mazao yake, nazo mbingu zitatoa umande wao, basi, hayo yote nitawapa walio masao ya ukoo huu, yawe fungu lao.

13Kama mlivyokuwa kiapizo kwa wamizimu ninyi mlio mlango wa Yuda nanyi mlio mlango wa Isiraeli, ndivyo, nitakavyowaokoa ninyi, mwe mbaraka; msiogope, ila mikono yenu itieni nguvu![#1 Mose 12:2.]

14Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Kama nilivyowaza moyoni mabaya, nitakayowafanyia ninyi, baba zenu waliponikasirisha, nikaacha kugeuza moyo,

15ndivyo, nilivyowaza moyoni siku hizi mema, nitakayowafanyia wao wa Yerusalemu nao walio mlango wa Yuda; kwa hiyo msiogope! ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi.

16Haya ndiyo maagizo, mtakayoyafanya: Semeni yaliyo kweli kila mtu na mwenziwe, tena kateni malangoni kwenu mashauri yaliyo sawa![#Ef. 4:25.]

17Mtu na mwenziwe msiwaziane mabaya mioyoni mwenu, wala msipende kuapa viapo vya uwongo! Kwani hayo yote ndiyo, ninayochukizwa nayo; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Zak. 7:10.]

18Neno la Bwana Mwenye vikosi likanijia la kwamba:

19Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Mifungo ya mwezi wa nne na wa tano na wa saba na wa kumi itageuka kuwa siku za furaha na za shangwe kwao walio mlango wa Yuda, zitakuwa sikukuu zipendezazo. Lakini sharti myapende mambo ya kweli na matengemano![#Zak. 7:3,5; Yer. 41:1; 52:4-6,12.]

20Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Yako makabila mazima ya watu watakaokuja pamoja na wenyeji wa miji mingi.

21Wenyeji wa mji mmoja watakwenda kwa wenyeji wa mji mwingine kuwaambia: Haya! Twende kujinyenyekeza mbele ya Bwana na kumtafuta Bwana Mwenye vikosi! Mimi nami nitakwenda.

22Ndipo, watakapokuja watu wa makabila mengi, hata wamizimu wenye nguvu, wakimtafuta Bwana Mwenye vikosi mle Yerusalemu, wajinyenyekeze mbele ya Bwana.

23Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Siku hizo itakuwa, watu kumi waliotoka katika misemo yote ya wamizimu wamshike mtu mmoja wa Kiyuda wakikamata pindo la nguo yake, kisha watamwambia: Tunataka kwenda nanyi, kwani tumesikia, ya kuwa Mungu yuko pamoja nanyi.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania