1 Samweli 21

1 Samweli 21

Daudi na Mkate Mtakatifu

1Basi Daudi akaenda Nobu kwa Ahimeleki, kuhani. Ahimeleki akaenda kumlaki Daudi, akitetemeka, akamwambia, Kwa nini uko peke yako, wala hapana mtu pamoja nawe?[#Mt 12:3-4; Mk 2:25-26; Lk 6:3; 1 Sam 22:19; Neh 11:32; Isa 10:32; 1 Sam 14:3]

2Daudi akamwambia Ahimeleki, kuhani, Mfalme ameniagiza shughuli, akaniambia, Asijue mtu awaye yote habari ya shughuli hii ninayokutuma, wala ya neno hili ninalokuamuru; nami nimewaagiza vijana waende mahali fulani.[#Mwa 27:20-24; 1 Sam 19:11; 22:22; 1 Fal 13:18; Zab 119:29; 141:3; Mit 29:25; Gal 2:12,13; Kol 3:9]

3Kuna nini basi, chini ya mkono wako? Nipe mkononi mwangu mikate mitano, au chochote ulicho nacho hapa.

4Yule kuhani akamjibu Daudi, akasema, Hapana mikate ya kawaida chini ya mkono wangu, ila mikate mitakatifu; ikiwa wale vijana wamejitenga na wanawake.[#Kut 25:30; Law 24:5; Mt 12:4; Kut 19:15; Zek 7:3]

5Naye Daudi akamjibu kuhani, akamwambia, Hakika tumejitenga na wanawake siku hizi tatu; napo nilipotoka, vyombo vya vijana hawa vilikuwa vitakatifu, ingawa ilikuwa safari ya kawaida; basi leo je! Vyombo vyetu havitakuwa vitakatifu zaidi?[#1 The 4:4; Law 8:26]

6Ndipo kuhani akampa ile mikate mitakatifu; kwa maana hapakuwa na mikate ila ile ya wonyesho, nayo imekwisha kuondolewa mbele za BWANA, ili itiwe mikate ya moto siku ile ilipoondolewa.[#Law 24:5-9; Mt 12:3; Mk 2:25; Lk 6:3]

7Basi siku ile palikuwapo na mtu mmoja wa watumishi wa Sauli, amezuiwa hapo mbele za BWANA jina lake akiitwa Doegi, Mwedomi, mkubwa wa wachungaji wa Sauli.[#1 Sam 22:9]

8Tena Daudi akamwambia Ahimeleki, Na hapa chini ya mkono wako, je! Hapana mkuki, au upanga? Kwa maana sikuleta upanga, wala silaha zangu, kwa sababu ile shughuli ya mfalme ilitaka haraka.

9Yule kuhani akasema, Upanga wa Goliathi, yule Mfilisti, uliyemwua katika bonde la Ela, tazama, upo hapa, umefungwa ndani ya nguo nyuma ya naivera; ukipenda kuuchukua, haya! Uchukue, maana hapa hapana mwingine ila huo tu. Daudi akasema, Hapana mwingine kama ule; haya! Nipe.[#1 Sam 17:51; 31:10]

Daudi akimbilia Gathi

10Basi Daudi akaondoka, akakimbia siku ile, kwa hofu ya Sauli, akamwendea Akishi, mfalme wa Gathi.

11Nao watumishi wa Akishi wakamwambia, Je! Huyu siye yule Daudi, mfalme wa nchi? Je! Hawakuimbiana habari zake katika ngoma zao, kusema,[#1 Sam 18:7; 29:5]

Sauli amewaua elfu zake,

Na Daudi makumi elfu yake.

12Naye Daudi akayatia maneno hayo moyoni mwake, akamwogopa sana Akishi, mfalme wa Gathi.[#Zab 56:1]

13Akaubadilisha mwenendo wake mbele yao, akajifanya mwenye wazimu mikononi mwao, akakunakuna katika mbao za mlango, na kuyaacha mate yake kuanguka juu ya ndevu zake.[#Zab 34:1]

14Ndipo huyo Akishi akawaambia watumishi wake, Angalieni, mnaona ya kuwa mtu huyu ana wazimu; basi, maana yake nini kumleta kwangu?

15Je! Mimi nina haja ya watu wenye wazimu, hata mmemleta kiumbe huyu ili aoneshe wazimu wake machoni pangu? Je! Huyu ataingia nyumbani mwangu?

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya