The chat will start when you send the first message.
1Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme wakuu mia moja na ishirini, wawe juu ya ufalme wote;[#Est 1:1]
2na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili wakuu hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara.[#1 Sam 2:30]
3Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na watawala, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote.[#Mit 3:35; Dan 5:12]
4Basi mawaziri na viongozi wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake.[#Mhu 4:4; Flp 2:15; 1 Pet 2:12]
5Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake.
6Basi wale mawaziri na viongozi wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia hivi, Mfalme Dario, uishi milele.[#Neh 2:3; Dan 2:4]
7Mawaziri wote wa ufalme, na wasimamizi, na viongozi, na washauri, na watawala wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu yeyote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba.
8Sasa, Ee mfalme, piga marufuku, ukatie sahihi maandiko haya, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza kubadilika.[#Est 1:19]
9Basi mfalme Dario akayatia sahihi maandiko yale, na ile marufuku.[#Zab 118:9]
10Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kuelekea Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo.[#Mt 10:32; Yon 2:4; Zab 5:7; 55:17; 95:6; 1 Fal 18:36; Lk 22:41; Mdo 2:1,2,15; 1 The 5:17,18]
11Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, mbele za Mungu wake na kusihi.
12Ndipo wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme kuhusu habari ya ile marufuku ya mfalme; Je! Hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema, Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika.[#Dan 3:8]
13Basi wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku.[#Dan 1:6; 3:12; Est 3:8; Mdo 17:7]
14Basi mfalme aliposikia maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli; akajitaabisha kumwokoa hata jua likachwa.[#Dan 3:13; Mt 27:17-24; Mk 6:26]
15Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lolote lililo marufuku, wala amri yoyote iliyowekwa na mfalme.
16Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya.[#Isa 41:10; 2 Kor 1:10]
17Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia mhuri kwa mhuri wake mwenyewe, na kwa mhuri wa wakuu wake, lisibadilike neno lolote katika habari za Danieli.[#Omb 3:53; Mk 15:46; Mt 27:66]
18Kisha mfalme akaenda nyumbani kwake, akakesha usiku kucha, akafunga; na vinanda havikuletwa mbele yake; na usingizi wake ukampaa.[#Est 6:1; Zab 77:4; Dan 2:1]
19Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba.
20Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danieli, Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa?[#Mwa 18:14; Yer 32:17; Zek 8:6; Mt 19:26; Lk 1:37]
21Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele.[#Dan 2:4]
22Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye amevifunga vinywa vya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nilionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno.[#Dan 3:28; Ebr 1:14; 11:33; 1 Sam 17:37; 2 Tim 4:17]
23Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli akatolewa katika lile tundu, wala halikuonekana dhara lolote mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake.[#Mk 16:18]
24Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu.[#Kum 19:19; 24:16; Est 9:10]
25Ndipo mfalme Dario akawaandikia watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, waliokaa juu ya uso wa dunia; Amani na iongezeke kwenu.[#Dan 4:1]
26Mimi ninaweka amri, ya kwamba katika mamlaka yote ya ufalme wangu watu watetemeke na kuogopa mbele za Mungu wa Danieli; maana yeye ndiye Mungu aliye hai, adumuye milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake itadumu hata mwisho.[#Dan 3:29; 4:34; 2:44; Zab 99:1; Lk 1:33]
27Yeye huponya na kuokoa, hutenda ishara na maajabu mbinguni na duniani, ndiye aliyemponya Danieli na nguvu za simba.[#Dan 4:3]
28Basi Danieli huyo akafanikiwa katika enzi ya Dario, na katika enzi ya Koreshi, Mwajemi.[#Dan 1:21; Ezr 1:1]