The chat will start when you send the first message.
1Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako itakuwa kubwa sana.[#Mwa 46:2; Isa 41:10; Zab 58:11; 84:11; Ebr 11:6]
2Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski?
3Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu.
4Nalo neno la BWANA likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali utakayemzaa ndiye atakayekurithi.[#Mwa 17:16; 2 Sam 7:12]
5Akamtoa nje, akasema, Tazama juu mbinguni kisha uzihesabu nyota, kama unaweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.[#Rum 4:18; Ebr 11:12; Zab 147:4; Kut 32:13]
6Akamwamini BWANA, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki.[#Rum 4:3-6,20-25; Zab 106:31; Gal 3:6; Yak 2:23]
7Kisha akamwambia, Mimi ni BWANA, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi hii ili uimiliki.[#Mdo 7:2]
8Akasema, Ee Bwana MUNGU, nipateje kujua ya kwamba nitaimiliki?[#Amu 6:36-40; 1 Sam 14:9,10; 2 Fal 20:8; Lk 1:18]
9Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo dume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa.
10Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua.
11Na tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza.
12Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia.[#Ayu 4:13,14; Mwa 2:21]
13BWANA akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa kwa muda wa miaka mia nne.[#Kut 1:1-14; 12:40; Mdo 7:6]
14Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali nyingi.[#Kut 6:6; 7:14; Kut 12:40-41; Mdo 7:7]
15Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema.[#Mwa 25:8; Ayu 5:26; Ebr 11:13]
16Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana uovu wa Waamori haujatimia bado.[#Mt 23:32; 1 The 2:16; 2 Pet 3:8,9]
17Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuri ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama.
18Siku ile BWANA akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati,[#Mdo 7:5; Mwa 17:8; Kum 1:7; Hes 34:3; 2 Nya 9:26; Neh 9:8; Zab 105:11]
19Mkeni, na Mkenizi, na Mkadmoni,
20na Mhiti, na Mperizi, na Mrefai,
21na Mwamori, na Mkanaani, na Mgirgashi, na Myebusi.