Mwanzo 8

Mwanzo 8

Kupwa kwa gharika

1Na Mungu akamkumbuka Nuhu, na kila kilicho hai, na wanyama wote waliokuwamo pamoja naye katika safina; Mungu akavumisha upepo juu ya nchi, maji yakapungua;[#Mwa 19:29; Kut 2:24; 1 Sam 1:19; Zab 105:42; 136:23; Kut 14:21; 15:10; Zab 104:7]

2chemchemi za vilindi zikafungwa, pia na madirisha ya mbinguni, mvua kutoka mbinguni ikazuiliwa;[#Mwa 7:11; 1 Fal 8:35; Ayu 38:37]

3maji yakadumu kuondoka katika nchi; na mwisho wa siku mia moja na hamsini maji yakapunguka.[#Mwa 7:24]

4Mwezi wa saba, siku ya kumi na saba ya mwezi, safina ikatua juu ya milima ya Ararati.

5Maji yakapungukapunguka hata mwezi wa kumi; mwezi huo wa kumi, siku ya kwanza ya mwezi, vilele vya milima vikaonekana.

6Ikawa baada ya siku arubaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya;[#Mwa 6:16]

7akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huku na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi.[#1 Fal 17:4]

8Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi;

9bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani.[#Kum 28:65]

10Akangoja na siku saba tena; kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili,

11njiwa akamjia jioni, na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo amelichuma, basi Nuhu akajua ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi.[#Lk 2:14]

12Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie tena kamwe.

13Ikawa mwaka wa mia sita na moja, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, maji yalikauka juu ya nchi. Nuhu akaondoa kifuniko cha safina, naye akaona, na tazama, uso wa nchi umekauka.

14Na mwezi wa pili, siku ya ishirini na saba ya mwezi, nchi ilikuwa kavu.

15Mungu akamwambia Nuhu, akisema,

16Toka katika safina, wewe, na mkeo, na wanao, na wake za wanao pamoja nawe.[#Mwa 7:13; Zab 121:8]

17Utoe pamoja nawe kila kilicho hai kilichomo pamoja nawe, chenye mwili, ndege, na mnyama, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi; wajae katika nchi, wawe na uzazi, wakaongezeke katika nchi.[#Mwa 1:22]

18Basi Nuhu akatoka, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye;

19kila mnyama, na kila kitambaacho, na kila ndege, kila kinachokwenda juu ya nchi kwa makabila yao, wakatoka katika safina.

Ahadi ya Mungu kwa Nuhu

20Nuhu akamjengea BWANA madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu.[#Law 11:1-31]

21BWANA akasikia harufu ya kumridhisha; BWANA akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya. 1[#Law 1:9; Kut 29:41; 2 Kor 2:15; Efe 5:2; Mwa 3:17; 6:17; Isa 54:9; Mwa 6:5; Zab 51:5; Ayu 14:4; 15:14; Yer 17:9; Rum 1:21; 3:23; Efe 2:1-3; Mwa 9:15]

22Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa joto, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma.[#Yer 33:20,25]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya