Yeremia 9

Yeremia 9

1Laiti kichwa changu kingekuwa maji, na macho yangu kuwa chemchemi ya machozi, ili nipate kulia mchana na usiku kwa ajili yao waliouawa wa binti ya watu wangu!

2Laiti ningekuwa na mahali pa kukaa jangwani, kibanda cha wasafiri; nipate kuwaacha watu wangu, na kuondoka kwao! Maana wao ni wazinzi, wote pia, mkutano wa watu wenye hiana.

3Huupinda ulimi wao, kana kwamba ni upinde, ili kusema uongo; nao wamepata nguvu katika nchi, lakini si katika uaminifu; maana huendelea toka ubaya hata ubaya, wala hawanijui mimi, asema BWANA.[#Amu 2:10; 1 Sam 2:12; Mit 1:29; Yer 4:22; Rum 1:28; 1 Kor 15:34]

4Jihadharini, kila mtu na jirani yake, wala msimtumaini ndugu awaye yote; maana kila ndugu atachongea, na kila jirani atakwenda huku na huko na kusingizia.[#Mik 7:5,6]

5Nao watadanganya kila mtu jirani yake, wala hawatasema kweli; wameuzoesha ulimi wao kusema uongo; hujidhoofisha ili kutenda uovu.

6Makao yako ya katikati ya hadaa; kwa hadaa wanakataa kunijua mimi, asema BWANA.[#Mit 1:24]

7Basi, kwa hiyo BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawayeyusha na kuwajaribu; maana nisipotenda hivi, nitende nini kwa ajili ya binti ya watu wangu?[#Isa 1:25; Hos 11:8]

8Ulimi wao ni mshale ufishao; husema maneno ya hadaa; mtu mmoja husema maneno ya amani na mwenzake kwa kinywa chake, lakini moyoni mwake humwotea.

9Je! Nisiwaadhibu kwa mambo hayo? Asema BWANA; na nafsi yangu je! Nisijilipize kisasi juu ya taifa la namna hii?

10Kwa milima nitalia na kulalama,

Na kwa malisho ya nyikani nitafanya maombolezo;

Kwa sababu yameteketea, hata hakuna apitaye,

Wala hapana awezaye kusikia sauti ya ng'ombe;

Ndege wa angani, na wanyama wa mwituni,

Wamekimbia, wamekwenda zao.

11Nami nitafanya Yerusalemu kuwa magofu,

Makao ya mbweha;

Nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa,

Isikaliwe na mtu awaye yote.

12Ni nani aliye na hekima, apate kuelewa haya? Tena ni nani ambaye kinywa cha BWANA kimesema naye, apate kuyatangaza? Nayo ni nini maana yake nchi hii kuharibika, na kuteketea kama nyika, asipite mtu?[#Zab 107:43; Isa 42:23; Hos 14:9]

13Naye BWANA asema, Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu niliyoweka mbele yao, wala hawakuitii sauti yangu, wala kuenda katika hiyo;

14bali wameenda katika ushupavu wa mioyo yao wenyewe, na kuandamana na Mabaali, kama walivyofundishwa na baba zao.[#Gal 1:14]

15Basi, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitawalisha pakanga, naam, watu hawa, nami nitawapa maji yenye sumu wayanywe.[#Zab 80:5; Omb 3:15]

16Nami nitawatawanya kati ya mataifa, ambao wao hawakuwajua; wala baba zao, nami nitatuma upanga nyuma yao, hata nitakapowaangamiza kabisa.[#Law 26:33; Kum 28:64; Eze 5:2]

Watu wanaomboleza katika hukumu

17BWANA wa majeshi asema hivi, Fikirini ninyi, mkawaite wanawake waombolezao, ili waje; mkatume na kuwaita wanawake wenye ustadi, ili waje;[#Mhu 12:5; Amo 5:16; Mt 9:23]

18na wafanye haraka na kutuombolezea, ili macho yetu yachuruzike machozi, na kope zetu zibubujike maji.[#Yer 14:17; Omb 1:16]

19Maana sauti ya maombolezo imesikiwa toka Sayuni,[#Law 18:28]

Jinsi tulivyotekwa!

tulivyofadhaika sana!

Kwa sababu tumeiacha nchi,

kwa kuwa wameangusha makao yetu.

20Lakini lisikieni neno la BWANA, enyi wanawake,

Na masikio yenu yapokee neno la kinywa chake;

Mkawafundishe binti zenu kuomboleza,

Na kila mmoja jirani yake kulia.

21Kwa maana mauti imepandia madirishani mwetu,

imeingia majumbani mwetu;

Ipate kuwakatilia mbali watoto walio nje,

na vijana katika njia kuu.

22Nena, BWANA asema hivi,

Mizoga ya watu itaanguka

kama samadi juu ya mashamba,

Na kama konzi ya ngano nyuma yake avunaye,

wala hapana mtu atakayeikusanya.

23BWANA asema hivi, Mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake;[#Zab 33:16; Mhu 9:11; Isa 5:21; Rum 1:22]

24bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni BWANA, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema BWANA,[#Zab 20:7; Mik 6:8; 1 Kor 1:31; 2 Kor 10:17]

25Tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapowaadhibu wote waliotahiriwa katika hali yao ya kutotahiriwa;[#Amo 3:2]

26Misri, na Yuda, na Edomu, na wana wa Amoni, na Moabu, na wote wenye kunyoa denge, wakaao nyikani; maana mataifa hayo yote hawana tohara, wala nyumba yote ya Israeli hawakutahiriwa mioyo yao.[#Law 26:41; Mdo 7:51; Rum 2:28]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya