Zaburi 137

Zaburi 137

Maombolezo juu ya maangamizi ya Yerusalemu

1Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi,[#Eze 1:1; Dan 8:2; Isa 24:8; Omb 5:15; Amo 8:10; Ufu 18:22]

Tukalia tulipoikumbuka Sayuni.

2Katika miti iliyo katikati yake

Tulivitundika vinubi vyetu.

3Maana huko waliotuchukua mateka

Walitaka tuwaimbie;

Na waliotuonea walitaka tuwatumbuize;

Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni.

4Twawezaje kuimba wimbo wa BWANA

Katika nchi ya ugeni?

5Nikikusahau, Ee Yerusalemu,

Mkono wangu wa kulia na upooze.

6Ulimi wangu na ugandamane[#Eze 3:26]

Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka.

Nisipoikuza Yerusalemu

Zaidi ya furaha yangu iliyo kuu.

7Ee BWANA, uwakumbuke wana wa Edomu,[#Omb 4:22; Oba 1:10]

Siku ile Yerusalemu ilipotekwa.

Kwa namna walivyosema, Bomoeni!

Bomoeni hata misingini!

8Ee binti Babeli, uliye karibu na kuangamia,[#Isa 13:1; Ufu 18:6]

Heri atakayekupatiliza, ulivyotupatiliza sisi.

9Heri yeye atakayewakamata wadogo wako,

Na kuwaseta wao juu ya mwamba.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya