Zaburi 78

Zaburi 78

Wema wa Mungu na Israeli kukosa shukrani

1Enyi watu wangu, sikilizeni sheria yangu,[#Kut 19:5; Kum 32:29]

Tegeni masikio kwa maneno ya kinywa changu.

2Nitafumbua kinywa changu kwa mithali,[#Zab 49:4; Mt 13:35]

Niyatamke mafumbo ya kale.

3Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu,[#Zab 44:1]

Ambayo baba zetu walituambia.

4Hayo hatutawaficha wana wao,[#Kum 4:9; Kut 12:26; Yos 4:6,7]

Huku tukiwaambia kizazi kingine,

Sifa za BWANA, na nguvu zake,

Na mambo yake ya ajabu aliyoyafanya.

5Maana alikaza ushuhuda katika Yakobo,

Na sheria aliiweka katika Israeli.

Aliyowaamuru baba zetu

Wawajulishe wana wao,

6Ili kizazi kingine wawe na habari,[#Zab 102:18]

Ndio hao wana watakaozaliwa.

Wasimame na kuwaambia wana wao.

7Wamwekee Mungu tumaini lao.

Wala wasiyasahau matendo ya Mungu,

Bali wazishike amri zake.

8Naam, wasiwe kama baba zao,

Kizazi cha ukaidi na uasi.

Kizazi kisichojitengeneza moyo,

Wala roho yake haikuwa amini kwa Mungu.

9Wale Waefraimu, wenye silaha, wapiga upinde,

Walirudi nyuma siku ya vita.

10Hawakulishika agano la Mungu;

Wakakataa kufuata sheria yake;

11Wakayasahau matendo yake,[#Isa 17:10; Yer 2:32]

Na mambo yake ya ajabu aliyowaonesha.

12Mbele ya baba zao alifanya mambo ya ajabu,[#Mwa 32:3; Kut 7:8—12:32; Isa 19:11]

Katika nchi ya Misri, konde la Soani.

13Aliipasua bahari akawavusha;[#Kut 14:21-22]

Aliyafanya maji yasimame kama ukuta.

14Akawaongoza kwa wingu mchana,[#Kut 13:21-22]

Na usiku kucha kwa nuru ya moto.

15Akapasua miamba jangwani;[#Kut 17:1-7; Hes 20:2-13; Zab 105:41; Isa 41:18]

Akawanywesha maji mengi kama maji ya vilindi.

16Akafanya vijito vitokeze katika mwamba,[#Kum 9:21]

Na kufanya maji yatiririke kama mito.

17Lakini wakazidi kumtenda dhambi,[#Ebr 3:16]

Walipomwasi Aliye Juu katika jangwa.

18Wakamjaribu Mungu mioyoni mwao[#Kut 16:2-15; Hes 11:4-23,31-35]

Kwa kutaka chakula kwa tamaa zao.

19Naam, walimwambia Mungu, wakasema,[#Hes 11:4]

Je! Mungu aweza kuandaa meza jangwani?

20Tazama, aliupiga mwamba;[#Kut 17:6; Hes 20:11]

Maji yakabubujika, ikafurika mito.

Pia aweza kutupa chakula?

Atawaandalia watu wake nyama?

21Hivyo BWANA aliposikia akaghadhibika;

Moto ukawashwa juu ya Yakobo,

Hasira nayo ikapanda juu ya Israeli.

22Kwa kuwa hawakumwamini Mungu,[#Ebr 3:10]

Wala hawakuutumainia wokovu wake.

23Lakini aliyaamuru mawingu juu;[#Mwa 7:11; Kum 28:12]

Akaifungua milango ya mbinguni;

24Akawanyeshea mana ili wale;[#Kut 16:14; Neh 9:15,20; Yn 6:31; 1 Kor 10:3]

Akawapa nafaka ya mbinguni.

25Mwanadamu akala chakula walacho malaika;

Akawapelekea chakula cha kuwashibisha.

26Aliuelekeza upepo wa mashariki kuvuma toka mbinguni;

Na kwa uweza wake akauongoza upepo wa kusini.

27Akawanyeshea nyama kama mavumbi,

Na ndege wenye mbawa,

Kama mchanga wa bahari.

28Akawaangusha kati ya matuo yao,

Pande zote za maskani zao.

29Wakala wakashiba sana;

Maana aliwaletea walivyovitamani;

30Lakini kabla ya kuitosheleza shauku yao,

Huku chakula kikiwa bado kinywani mwao,

31Hasira ya Mungu ikapanda juu yao,

Akawaua waliokuwa wanono;

Akawaangusha chini vijana wa Israeli.

32Pamoja na hayo wakazidi kutenda dhambi,

Wala hawakuyaamini matendo yake ya ajabu.

33Kwa hiyo akazikomesha siku zao kama pumzi,

Na miaka yao kwa hofu ya kuwastusha.

34Alipowaua ndipo walipokuwa wakimtafuta;[#Hes 5:15]

Wakarudi wakamtaka Mungu kwa bidii.

35Wakakumbuka kuwa Mungu ni mwamba wao,

Na Mungu Aliye Juu ni mkombozi wao.

36Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao,[#Eze 33:31]

Wakamwambia uongo kwa ndimi zao.

37Kwa maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake,[#Mdo 8:21]

Wala hawakuwa waaminifu katika agano lake.

38Lakini Yeye, kwa kuwa anayo rehema,[#Kut 34:6; Neh 9:17; Zab 86:15; 1 Fal 21:29; Isa 48:9; Mik 7:18; Rum 2:4]

Husamehe uovu wala haangamizi.

Mara nyingi huipishia mbali ghadhabu yake,

Wala haiwashi hasira yake yote.

39Akakumbuka ya kuwa wao ni kiwiliwili,[#Mwa 6:3; Yn 3:6; Yak 4:14; Ayu 7:7,16]

Upepo upitao wala haurudi.

40Walimwasi jangwani mara ngapi?

Na kumhuzunisha nyikani!

41Wakamjaribu Mungu tena na tena;

Na kumkasirisha Mtakatifu wa Israeli.

42Hawakuukumbuka mkono wake,

Wala siku ile alipowakomboa na mtesi.

43Alivyoziweka ishara zake katika Misri,

Na miujiza yake katika uwanda wa Soani.

44Aligeuza mito yao kuwa damu,[#Kut 7:17-21]

Ili wasipate kunywa maji kutoka vijito vyao.

45Aliwapelekea mainzi wakawala,[#Kut 8:1-6,20-24]

Na vyura wakawaharibu.

46Akawapa tunutu mazao yao,[#Kut 10:12-15]

Na nzige matunda ya kazi yao.

47Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe,[#Kut 9:22-25]

Na mikuyu yao kwa mawe ya barafu.

48Akaacha ng'ombe zao wapigwe kwa mvua ya mawe,

Na makundi yao kwa umeme.

49Akawapelekea ukali wa hasira yake,[#Rum 2:8]

Ghadhabu, na uchungu, na taabu,

Kundi la malaika waletao mabaya.

50Akaifanyia njia hasira yake;

Wala hakuziepusha roho zao kutoka kwa mauti,

Bali aliiachia tauni uhai wao;

51Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri,[#Mwa 9:22; Kut 12:29]

Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu.

52Kisha akawaongoza watu wake kama kondoo,[#Kut 13:17-22]

Akawachunga kama kundi jangwani.

53Hao akawachukua salama wala hawakuogopa,[#Kut 14:26-28]

Bali bahari iliwafunika adui zao.

54Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu,[#Kut 15:17; Yos 3:14-17]

Mlima alioununua kwa mkono wake wa kulia.

55Akawafukuza mataifa mbele yao,[#Yos 11:16-23]

Akawapimia urithi kwa kamba,

Na kuwakalisha makabila ya Israeli katika hema zao.

56Lakini walimjaribu Mungu Aliye Juu, wakamwasi,[#Amu 2:11-15]

Wala hawakuzishika shuhuda zake.

57Bali walirudi nyuma, wakahaini kama baba zao;[#Eze 20:27; Hos 7:16]

Wakayumba kama upinde usiofaa.

58Wakamkasirisha kwa mahali pao pa juu,[#Law 26:30; Hes 33:52; Kum 12:2]

Wakamtia wivu kwa sanamu zao.

59Mungu alisikia, akaghadhibika,[#Ebr 4:13]

Akamkataa Israeli kabisa.

60Akaiacha maskani ya Shilo,[#1 Sam 4:11; Yer 7:12; Yos 18:1; Yer 7:12-14; 26:6]

Hema aliyoiweka katikati ya wanadamu;

61Akaziacha nguvu zake kutekwa,[#1 Sam 4:4-22; Amu 4:12]

Na fahari yake mkononi mwa mtesi.

62Akawatoa watu wake wapigwe kwa upanga;

Akaughadhibikia urithi wake.

63Moto ukawala vijana wao,

Wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi,

64Makuhani wao walianguka kwa upanga,[#Ayu 27:15]

Wala wajane wao hawakuomboleza.

65Ndipo Bwana alipoamka kama aliyelala usingizi,[#Isa 42:13]

Kama shujaa apigaye kelele kwa sababu ya mvinyo;

66Akawapiga watesi wake akawarudisha nyuma,

Akawatia aibu ya milele.

67Ila akaikataa hema ya Yusufu;

Wala hakuichagua kabila la Efraimu.

68Bali aliichagua kabila la Yuda,

Mlima Sayuni alioupenda.

69Akajenga patakatifu pake kama vilele,[#1 Fal 6:1]

Kama dunia aliyoiweka imara milele.

70Akamchagua Daudi, mtumishi wake,[#1 Sam 16:11-12; 2 Sam 7:8; 1 Nya 17:7]

Akamwondoa katika mazizi ya kondoo.

71Nyuma ya kondoo wanyonyeshao alimwondoa,[#2 Sam 5:2; 1 Nya 11:2; Mik 5:2-4; Zek 11:4]

Awachunge Yakobo watu wake, na Israeli urithi wake.

72Akawahudumia kwa ukamilifu wa moyo wake,[#1 Fal 9:4]

Na kuwaongoza kwa busara ya mikono yake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya