Zaburi 97

Zaburi 97

Utukufu wa enzi ya Mungu

1BWANA ametamalaki, nchi na ishangilie,

Visiwa vingi na vifurahi.

2Mawingu na giza vyamzunguka,

Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.

3Moto hutangulia mbele zake,[#Dan 7:10; Hab 3:5]

Nao huwateketeza watesi wake pande zote.

4Umeme wake uliuangaza ulimwengu,

Nchi ikaona ikatetemeka.

5Milima iliyeyuka kama nta mbele za BWANA,

Mbele za Bwana wa dunia yote.

6Mbingu zimetangaza haki yake,

Na watu wote wameuona utukufu wake.

7Na waaibishwe wote waabuduo sanamu,[#Kut 20:4; Law 26:1; Isa 37:18,19; Yer 10:14; Ebr 1:6]

Wajivunao kwa vitu visivyofaa;

Enyi miungu yote, msujuduni Yeye.

8Sayuni imesikia na kufurahi,

Binti za Yuda walishangilia,

Kwa sababu ya hukumu zako, Ee BWANA.

9Maana Wewe, BWANA, ndiwe Uliye juu,[#Efe 1:21]

Juu sana kuliko nchi yote;

Umetukuka sana juu ya miungu yote.

10Enyi mmpendao BWANA, uchukieni uovu;[#Zab 101:3; Amo 5:15; Rum 7:15; 1 Sam 2:9; Mit 2:8; Dan 3:28]

Huwalinda nafsi zao watauwa wake,

Na kuwaokoa na mkono wa wasio haki.

11Nuru humwangazia mwenye haki,

Na furaha ni kwa wanyofu wa moyo.

12Enyi wenye haki, mfurahieni BWANA,

Na kulishukuru jina lake takatifu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya