The chat will start when you send the first message.
1Basi hawa ndio wale waliomjia Daudi huko Siklagi, alipokuwa akijificha kwa ajili ya Sauli, mwana wa Kishi; nao walikuwamo miongoni mwa wale mashujaa, waliomsaidia vitani.[#1 Sam 27:2,6]
2Walikuwa wenye kupinda upinde, nao walikuwa hodari wa kutumia mkono wa kulia na wa kushoto, kwa kutupa mawe ya teo, na kwa kupiga mishale ya upinde; walikuwa wa nduguze Sauli, wa Benyamini.[#Amu 20:16]
3Mkubwa wao alikuwa Ahiezeri, kisha Yoashi, wana wa Shemaa Mgibeathi; na Yezieli, na Peleti, wana wa Azmawethi; na Beraka, na Yehu Mwanathothi;[#Yos 21:18; 1 Nya 11:28]
4na Ishmaya Mgibeoni, shujaa wa wale thelathini, naye alikuwa juu ya wale thelathini; na Yeremia, na Yahazieli, na Yohana, na Yozabadi Mgederathi;[#Yos 10:2; 18:21,25; 1 Fal 3:4,5; 9:2; Isa 28:21]
5Eluzai, na Yerimothi, na Bealia, na Shemaria, na Shefatia Mharufi;
6Elkana, na Ishia, na Azaleli, na Yoezeri, na Yashobeamu, Wakora;
7na Yoela, na Zebadia, wana wa Yerohamu, wa Gedori.
8Na wa Wagadi wakajitenga kumfuata Daudi ngomeni huko nyikani, wanaume mashujaa, watu waliozoea vita, walioweza kutumia ngao na mkuki; ambao nyuso zao zilikuwa kama nyuso za simba, nao walikuwa wepesi kama kulungu juu ya milima;[#1 Sam 23:14,29; 1 Nya 11:16; 2 Sam 17:10; 23:20; 1 Nya 11:22; Mit 28:1; 2 Sam 2:18]
9Ezeri mkubwa wao, Obadia wa pili, Eliabu wa tatu;
10Mishmana wa nne, Yeremia wa tano;
11Atai wa sita, Elieli wa saba;
12Yohana wa nane, Elzabadi wa tisa;
13Yeremia wa kumi, Makbanai wa kumi na moja.
14Hao Wagadi walikuwa makamanda wa jeshi, yeye aliyekuwa mdogo amelingana na mia moja, na yeye aliyekuwa mkuu, na elfu moja.
15Hao ndio wale waliovuka Yordani katika mwezi wa kwanza, ulipofurika kingo zake zote; nao wakawakimbiza wote wa bondeni kuelekea mashariki na magharibi pia.[#Yos 3:15; Yer 12:5; 49:19]
16Tena wakafika ngomeni kwa Daudi baadhi ya wana wa Benyamini na Yuda.
17Naye Daudi akatoka ili kuwalaki, akajibu, akawaambia, Kama mmenijia kwa amani ili kunisaidia, basi nitawapokea kwa moyo wote; lakini kama mmekuja ili kunisaliti kwa adui zangu, ingawa hamna udhalimu mikononi mwangu, Mungu wa baba zetu na alitazame neno hili, na kulikemea.[#Zek 3:2; Yud 1:9]
18Ndipo roho ikamjia Abishai, mkuu wa wale thelathini, naye akasema,[#2 Sam 17:25; 1 Nya 2:17]
Sisi tu watu wako, Ee Daudi;
Na wa upande wako, Ee mwana wa Yese;
Amani, naam, amani iwe kwako,
Na amani iwe kwao wakusaidiao;
Maana Mungu wako ndiye akusaidiye.
Ndipo Daudi akawakaribisha, akawaweka wawe makamanda wa kile kikosi.
19Baadhi ya wana wa Manase walimwangukia Daudi, alipokwenda pamoja na Wafilisti juu ya Sauli vitani, lakini hawakuwasaidia; kwani wale mabwana wa Wafilisti wakafanya shauri, wakamfukuza, wakisema, tunahatarisha maisha yetu maana atamwangukia bwana wake Sauli.[#1 Sam 29:2,4]
20Naye alipokuwa akienda Siklagi, Manase hawa wakamwangukia, Adna, na Yozabadi, na Yediaeli, na Mikaeli, na Yozabadi, na Elihu, na Silethai, makamanda wa maelfu waliokuwa wa Manase.
21Wakamsaidia Daudi juu ya kile kikosi kilichomshambulia; kwani walikuwa wanaume mashujaa wote, nao wakawa makamanda jeshini.[#1 Sam 30:1]
22Maana siku baada ya siku watu waliomwendea Daudi ili kumsaidia, hadi wakapata kuwa jeshi kubwa, kama jeshi la Mungu.
23Na hizi ni hesabu za vichwa vya watu wenye silaha za vita, waliokuja Hebroni kwa Daudi, ili kumpa ufalme wa Sauli, sawasawa na neno la BWANA.[#2 Sam 2:3; 1 Nya 10:14; 11:10; 1 Sam 16:1]
24Wana wa Yuda, waliochukua ngao na mkuki, walikuwa elfu sita na mia nane, wenye silaha za vita.
25Wa wana wa Simeoni, wanaume mashujaa wa vita, elfu saba na mia moja.
26Wa wana wa Lawi, elfu nne na mia sita.
27Na Yehoyada alikuwa kichwa cha ukoo wa Haruni, na pamoja naye walikuwa watu elfu tatu na mia saba;
28tena Sadoki, kijana shujaa, na wa nyumba ya babaye, makamanda ishirini na wawili.[#2 Sam 8:17; 1 Fal 1:8; 2:25; 1 Nya 6:8; Eze 44:15]
29Na wa wana wa Benyamini nduguze Sauli, elfu tatu; kwani hata sasa walio wengi wao walikuwa wameuhifadhi uaminifu wao kwa nyumba ya Sauli.
30Na wa wana wa Efraimu, elfu ishirini na mia nane, wanaume mashujaa, watu wenye sifa katika koo za baba zao.
31Na wa nusu kabila la Manase, elfu kumi na nane, waliotajwa majina yao, ili waje kumtawaza Daudi awe mfalme.
32Na wa wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao.[#Est 1:13]
33Wa Zabuloni, watu wawezao kwenda pamoja na jeshi, hodari wa kupanga vita, wenye zana za vita za kila namna, elfu hamsini; askari stadi waliolenga tu kumsaidia Daudi.
34Na wa Naftali, makamanda elfu moja, na pamoja nao watu wenye ngao na mkuki elfu thelathini na saba.
35Na wa Wadani, watu hodari wa kupanga vita, elfu ishirini na nane na mia sita.
36Na wa Asheri, watu wawezao kwenda pamoja na jeshi, hodari wa kupanga vita, elfu arubaini.
37Tena, ng'ambo ya pili ya Yordani, wa Wareubeni, na wa Wagadi, na wa nusu kabila la Manase, wenye zana za vita za kupigania za kila namna, elfu mia moja na ishirini.
38Hao wote, watu wa vita, askari stadi, wakaja Hebroni wakiwa na nia moja ya kumtawaza Daudi awe mfalme juu ya Israeli wote; tena wote waliosalia wa Israeli nao walikuwa na moyo mmoja kwamba wamtawaze Daudi.
39Nao walikuwako huko pamoja na Daudi siku tatu, wakila na kunywa; kwani ndugu zao walikuwa wamewaandalia tayari.
40Zaidi ya hayo, wale waliokuwa karibu nao, hata mpaka kwa Isakari, na Zabuloni, na Naftali, wakaleta chakula juu ya punda, na ngamia, na nyumbu, na ng'ombe, vyakula vya unga, mikate ya tini, na vichala vya zabibu kavu, na divai, na mafuta, na ng'ombe, na kondoo tele; kwa kuwa kulikuwa na furaha katika Israeli.