The chat will start when you send the first message.
1Wakaliingiza sanduku la Mungu, na kuliweka katikati ya hema aliyoipiga Daudi kwa ajili yake; wakatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Mungu.[#2 Sam 6:17-19]
2Na Daudi alipokwisha kuitoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani, akawabariki watu kwa jina la BWANA.
3Kisha akawagawia kila mtu wa Israeli, wanaume kwa wanawake, kila mtu mkate wa ngano, na kipande cha nyama, na mkate wa zabibu.
4Akawaagiza baadhi ya Walawi kwamba watumike mbele ya sanduku la BWANA, wamfanyie ukumbusho, na shukrani, na sifa, BWANA, Mungu wa Israeli;
5Asafu mkuu wao, na wa pili wake Zekaria, na Yeieli, na Shemiramothi, na Yehieli, na Metithia, na Eliabu, na Benaya, na Obed-edomu, na Yeieli, wenye vinanda na vinubi; naye Asafu mwenye kupiga matoazi;
6nao makuhani Benaya na Yahazieli wenye baragumu daima, mbele ya sanduku la Agano la Mungu.
7Ndipo siku hiyo Daudi alipoagiza kwanza kumshukuru BWANA, kwa mkono wa Asafu na nduguze.[#2 Sam 23:1]
8Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake;[#Zab 105:1; 145:1]
Wajulisheni watu matendo yake.
9Mwimbieni, mwimbieni nyimbo za kumsifu;[#Zab 95:1,2; 100:1]
Yatangazeni matendo yake yote ya ajabu.
10Jisifuni kwa jina lake takatifu;[#Zab 34:3; Isa 45:25]
Na ufurahi moyo wao wamtafutao BWANA.
11Mtafuteni BWANA na nguvu zake;[#Amo 5:6,14]
Utafuteni uso wake siku zote.
12Yakumbukeni matendo yake yote ya ajabu aliyoyafanya;[#Zab 103:2; 111:2]
Miujiza yake na hukumu za kinywa chake;
13Enyi wazao wa Israeli, mtumishi wake,
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
14Yeye, BWANA, ndiye Mungu wetu;
Duniani kote kuna hukumu zake.
15Likumbukeni agano lake milele,
Neno lile aliloviamuru vizazi elfu.
16Agano alilofanya na Abrahamu,[#Mwa 15:18; 17:2; 26:3; Neh 9:8; Ebr 6:13-18]
Na kiapo chake kwa Isaka;
17Aliyomthibitishia Yakobo kuwa amri,
Na kwa Israeli kuwa agano la milele.
18Akisema, Nitakupa wewe nchi ya Kanaani,
Iwe urithi wenu mliopimiwa;
19Mlipokuwa watu wawezao kuhesabiwa;[#Mwa 34:30; Ebr 11:13]
Naam, watu wachache na wageni ndani yake.
20Mkitangatanga toka taifa hadi taifa,
Toka ufalme mmoja hadi kwa watu wengine.
21Hakumwacha mtu awaonee;[#Mwa 12:17; 20:3; Kut 7:15-18]
Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao;
22Akisema, Msiwaguse masihi wangu,[#Zab 105:15; 1 Yoh 2:27; #16:22 Au mtiwa mafuta (tazama 1 Sam 2:10).]
Wala msiwadhuru nabii zangu.
23Mwimbieni BWANA, nchi yote;[#Zab 47:1; 96:1]
Tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.
24Watangazieni mataifa habari za utukufu wake,[#Isa 12:4]
Na watu wote habari za maajabu yake.
25Kwa kuwa BWANA ni mkuu mwenye kusifiwa sana;[#Zab 24:8; 89:6-8; Isa 40:25,26]
Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.
26Maana miungu yote ya watu si kitu;[#Law 19:4; Zab 115:4-8; Isa 45:20; Yer 10:3; 1 Kor 8:4]
Lakini BWANA ndiye aliyezifanya mbingu.
27Heshima na adhama ziko mbele zake;[#Zab 8:1]
Nguvu na furaha zipo mahali pake.
28Mpeni BWANA, enyi jamaa za watu,
Mpeni BWANA utukufu na nguvu.
29Mpeni BWANA utukufu wa jina lake;
Leteni sadaka, na mje mbele zake;
Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu;
30Tetemekeni mbele zake, nchi yote.
Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike;
31Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie;[#Isa 35:10; Lk 2:13; Ufu 14:2]
Na waseme katika mataifa, BWANA ametamalaki;
32Bahari na ivume na vyote viijazavyo;[#Zab 96:10]
Mashamba na yashangilie na vyote vilivyomo;
33Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha,
Mbele za BWANA,
Kwa maana anakuja kuihukumu nchi.
34Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema;[#Zab 106:1; 107:1; 118:1]
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
35Nanyi semeni,[#Zab 106:47,48]
Ee Mungu wa wokovu wetu, utuokoe,
Utukusanye kwa kututoa katika mataifa,
Tulishukuru jina lako takatifu,
Tuzifanyie shangwe sifa zako.
36Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, tangu milele hata milele. Na watu wote wakasema, Amina; wakamhimidi BWANA.[#1 Fal 8:15; Zab 72:18,19; Kum 27:15; Neh 8:6]
37Basi akawaacha huko, mbele ya sanduku la Agano la BWANA, Asafu na nduguze, ili watumike mbele ya sanduku daima, kila siku kama ilivyokuwa kazi yake.
38Naye Obed-edomu, pamoja na ndugu zao, sitini na wanane; Obed-edomu na mwana wa Yeduthuni, na Hosa, wawe mabawabu;
39na Sadoki kuhani, na nduguze makuhani, mbele ya maskani ya BWANA katika mahali pa juu palipokuwa huko Gibeoni,[#1 Nya 21:29; 2 Nya 1:3; 1 Fal 3:4]
40ili kumtolea BWANA sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa daima asubuhi na jioni, naam, kulingana na yote yaliyoandikwa katika Torati ya BWANA, aliyowaamuru Israeli;[#Kut 29:38; Hes 28:3]
41na pamoja nao Hemani na Yeduthuni, na wale wengine waliochaguliwa, waliotajwa majina yao, ili kumshukuru BWANA, kwa kuwa fadhili zake ni za milele;[#2 Nya 5:13; 7:3; Ezr 3:11; Neh 9:17; Zab 25:10; 33:5; 100:5; Yer 33:11; Yoe 2:13; Lk 6:36; Yak 5:11]
42na pamoja nao Hemani na Yeduthuni wenye baragumu na matoazi, kwa hao watakaovumisha sauti, na vinanda kwa ajili ya hizo nyimbo za Mungu; na hao wana wa Yeduthuni wawepo mlangoni.
43Kisha watu wote wakaenda zao kila mtu nyumbani kwake; naye Daudi akarudi ili awabariki watu wa nyumbani mwake.[#2 Sam 6:19,20; Mwa 18:19; Yos 24:15]